• HABARI MPYA

    Friday, April 17, 2015

    SIMBA SC WAMSAKA RAIS WA ETOILE ALIPE BURUNGUTU LA OKWI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    RAIS wa Simba SC, Evans Eliza Aveva atakutana na Rais wa Etoile du Sahel, Ridha Charfeddine kuzungumzia juu ya mustakabali wa malipo yao, dola za KImarekani 300,000 (zaidi ya Sh. 540 za Tanzania) kutokana na mauzo ya mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi.
    Charfeddine ameongozana na kikosi cha Etoile kilichowasili Dar es Salaam Alfajiri ya leo kwa ajili ya mchezo wa kwanza, Raundi ya Pili Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya wenyeji Yanga SC kesho Uwanja wa Taifa.
    Na Simba SC inataka kutumia fursa hiyo kujua mustakabali wa malipo yao hayo. Kazi ya mazungumzo na Rais wa Etoile, ilikuwa ifanywe na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu ya Msimbazi, Zacharia Hans Poppe, lakini kwa bahati mbaya amepata udhuru.
    Hans Poppe (kulia) akiwa na Okwi wakati anarejea Simba SC Agosti mwaka jana

    “Nimepata safari ya kikazi, kwa hiyo jukumu hilo nimemkabidhi Rais (Aveva) na tayari ameanza harakati za kukutana na Rais wao (Etoile) ili tupate mustakabali wa malipo yetu,”amesema Poppe akizungumza na BIN ZUBEIRY leo Dar es Salaam.
    Okwi alinunuliwa na Etoile Januari mwaka 2013 kwa dau la rekodi kwa klabu za Tanzania, dola 300,000, ingawa baada ya muda akaingia kwenye mgogoro na klabu hiyo ya Tunisia.
    Mtafaruku ulianza baada ya Okwi kuchelewa kurejea mjini Sousse mkoani Sahel baada ya ruhusa ya kwenda kuichezea timu yake ya taifa, Uganda.
    Okwi naye akadai Etoile walikuwa hawamlipi mishahara na kufungua kesi FIFA (Shirikisho la Soka la Kimataifa), ambayo mwisho wa siku alishinda kwa kuruhusiwa kutafuta timu nyingine ya kuchezea kulinda kipaji chake, wakati wa mgogoro wake na klabu ya Tunisia.
    Okwi akajiunga na SC Villa ya kwao, Kampala katikati ya mwaka 2013 na Desemba mwaka huo, akahamia Yanga SC. 
    Hata hivyo, Okwi akavunja Mkataba na Yanga SC Agosti waka jana, baada ya timu hiyo ya Jangwani kushindwa kumlipa dola za Kimarekani 60,000 kama ilivyokuwa katika Mkataba baina yao na kurejea klabu yake ya zamani, Simba anakoendelea kucheza hadi sasa.
    Pamoja na hayo, Simba SC iliendelea na madai ya fedha zake kiasi cha kufungua kesi hadi FIFA, ambako walishinda na Etoile ikaamriwa kulipa, ingawa haijafanya hivyo hadi leo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC WAMSAKA RAIS WA ETOILE ALIPE BURUNGUTU LA OKWI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top