• HABARI MPYA

    Saturday, April 18, 2015

    YANGA SC WAISHINDWA ETOILE, PENGO LA TELELA NJE NJE

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    YANGA SC imejiwekea mazingira magumu ya kusonga mbele kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, baada ya kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Etoile du Sahel ya Tunisia jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Sasa, sare ya kaunzia 2-2 au ushindi wa ugenini kabisa ndiyo utaivusha Yanga SC katika kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo, ambako itacheza na moja ya timu zitakazotolewa katika Ligi ya Mabingwa.
    Yanga SC waliuanza vizuri mchezo wa leo kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la mapema dakika ya pili, mfungaji Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kwa penalti, baada ya winga Simon Msuva kuangushwa kwenye boksi.
    Kiungo mshambuliaji wa Yanga SC, Mrisho Ngassa kulia akiwania mpira dhidi ya beki wa Etoile Boughatas Zied

    Yanga ilishambulia kwa dakika mbili zaidi baada ya bao hilo, lakini kutoka hapo, Etoile wakauteka mchezo kutokana na kutawala sehemu ya kiungo.
    Yanga SC walikuwa wakipitishia mashambulizi yao pembeni kupitia kwa mawinga wake, Msuva na Mrisho Ngassa, lakini mshambuliaji Amissi Tambwe leo hakuwa katika ubora wake.
    Kipa Ally Mustafa ‘Barthez’ alifanya kazi nzuri kipindi cha kwanza kuokoa michomo kadhaa ya hatari.
    Mwishoni mwa kipindi cha kwanza, Yanga SC ilipata pigo baada ya Nahodha wake, Cannavaro kuumia mguu, jambo ambalo lilimlazimu kutorejea uwanjani kipindi cha pili, nafasi yake ikichukuliwa na Said Juma Makapu.
    Baada ya mabadiliko hayo, Mbuyu Twite alikwenda kucheza beki ya kati pamoja na Kevin Yondan, Makapu akienda kucheza kama kiungo mkabaji.
    Dakika mbili tu baada ya kuanza kipindi cha pili, Etoile waliata bao la kusawazisha kupitia kwa Ben Amor Med Amine aliyefumua shuti kali akiwa nje ya boksi baada ya kumsoma Barthez aliyekuwa amezubaa langoni.      
    Bao hilo la mapema kipindi cha pili liliwachanganya Yanga SC na kuvuruga kabisa mipango yao uwanjani, hivyo kuwapa fursa Etoile kutawala zaidi mchezo.
    Cannavaro aliifungia Yanga SC kwa penalti, lakini hakurudi kipindi cha pili baada ya kuumia
    Amisi Tambwe akiwatoka mabeki wa Etoile Uwanja wa Taifa leo

    Mrisho Khalfan Ngassa aliyekuwa mtengenezaji wa mashambulizi yote ya Yanga SC leo, alimpa pasi nzuri ndani ya boksi Msuva dakika ya 60, lakini akampasia kipa Mathlouthi Aynen mikononi.   
    Kocha Mholanzi, Hans van de Pluijm alifanya mabadiliko akimtoa kiungo Hassan Dilunga katikati ya kipindi cha pili na kumuingiza mshambuliaji Mliberia, Kpah Sherman.
    Dakika ya 87 Tambwe aliukwamisha mpira nyavuni akimalizia pasi ya Ngassa, lakini wakati anataka kuanza kushangilia akakutana na mkono wa refa Samuel Chirindiza wa Msumbiji akimuambia alikuwa ameotea.
    Baada ya tukio, hilo wachezaji wa Etoile wakaanza kujiangusha kupoteza muda.
    Awali ya hapo, dakika ya 85 Yanga ilipata pigo lingine baada ya beki wake wa kulia, Juma Abdul kuumia na kutoka akimpisha Rajab Zahir, aliyekwenda kucheza katikati, Mbuyu Twite akihamia pembeni kulia.
    Pamoja na pengo la kiungo majeruhi, Salum Telela kuonekana dhahiri leo, lakini wachezaji wa Yanga SC walizidiwa nguvu na wenzao wa Etoile uwanjani. 
    Kiungo Mcameroon Kon Franck ndiye alikuwa mwiba leo kwa Yanga SC kutokana na kutawala vizuri sehemu hiyo na kuwa chanzo kizuri cha mashambulizi ya Etoile. 
    Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul/Rajab Zahir dk85, Oscar Joshua, Kevin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’/Said Juma dk46, Mbuyu Twite, Hassan Dilunga/Kpah Sherman dk77, Haruna Niyonzima, Amisi Tambwe, Mrisho Ngassa na Simon Msuva.
    Etoile du Sahel; Mathlouthi Aymen, Nagwez Hamdi, Boughatas Zied, Bedoui Rami, Jemal Ammar, Ben Amor Amine, Kom Franck, Bangoura Alkhaly, Brigui Alaya, Mouhib Youssef/Saad Mehdi dk82 na Bounedjah Baghdad/Moussa Soufien dk90+.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC WAISHINDWA ETOILE, PENGO LA TELELA NJE NJE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top