• HABARI MPYA

    Monday, May 04, 2015

    MAYWEATHER ANAVYONIKUMBUSHA MASHABIKI MAANDAZI WA MUZIKI

    JUMAPILI saa 1 asubuhi (kwa saa za kibongo) dunia ikashuhudia mpambano wa karne wa masumbwi kati ya Floyd Mayweather na Manny Pacquiao.
    Mmarekani Mayweather akamshinda Mfilipino Pacquiao kwa wingi wa pointi na hapo ndipo tulipoanza kushuhudia maoni ya mashabiki maandazi.
    Wanasema Mayweather kabebwa kwa vile tu eti majaji walikuwa Wamarekani, wanasahau kuwa Mayweather alicheza kwa malengo.
    Wengi wanaosema Mayweather kabebwa ni wale waliohitaji bondia huyo apigwe na si tu kwasababu wana mapenzi na Manny Pacquiao la hasha, ni kwasababu wanataka Mayweather apigwe …apigwe tu!
    Apigwe kwa sababu wamechoka na mafanikio yake, apigwe kwasababu jamaa ana pesa na anajua kuzitumia pesa, apigwe kwasababu jamaa ni ‘bishoo’.
    Hii ni aina ya ushabiki maandazi, ni aina ya chuki binafsi, ni aina ya uchafu wa nafsi …hii utaikuta kwenye kila kitu, siasa, michezo, muziki, uongozi na kadhalika.
    Leo kuna watu wanataka Diamond Platnumz ashuke kimuziki, watamshabikia yeyote anayetishia ufalme wake, watafurahi kila baya litakalotokea upande wake.
    Sababu? Sababu ni ile ile “kuchoka mafanikio” ya mtu bila kujali kama yanakupunguzia chochote au kukuongezea chochote.
    Upo usemi mmoja wa hekima kuwa kumchukia msomi hakupunguzi ujinga wako, au kumchukia tajiri hakupunguzi umasikini wako. Kama tungezingatia semi kama hizi basi hakungekuwa na kitu “chuki binafsi”.
    Kwa zaidi ya miaka mitano wako watu wanaojaribu kuuporomosha umaarufu na mafanikio ya Mzee Yussuf, sababu? Eti kwanini yeye tu miaka yote hiyo! Kwanini Khadija Kopa yupo juu miaka na miaka?, vipi Isha Mashauzi atawale soko kwa muda mrefu? Zote hizi ni aina ya ushabiki maandazi.
    Ushabiki maandazi siku zote unaongozwa na chuki badala ya kuongozwa na wivu wa maendeleo, pambano la Floyd Mayweather na Manny Pacquiao linapambanua vizuri aina ya mashabiki maandazi. 
    Wakati fulani kuna watu walikuwa na kiu ya kuiona bendi ya African Stars “Twanga Pepeta” ikiporomoka, wengine wakaanzisha bendi kwa lengo la kuhitimisha uhai wa Twanga Pepeta, mashabiki wenye roho za kutu wakawa wakifurahia kila jaribio la kuiangamiza bendi hiyo, sababu? Eti iko juu kwa muda mrefu!
    Christian Bella ni aina ya wasanii wengine ‘wanaopigwa mawe’ kwasababu tu ya mafanikio yake, wanakerwa na namna anavyoitumia sauti yake tamu kupenya katika kila aina muziki unaohitajika sokoni, wanaumia na namna anavyotumia fursa na badala ya kujifunza kupitia yeye, wanaona njia nzuri ni kumuombea dua mbaya aanguke …ushabiki maandazi huo.
    Mashujaa Band kwa mwaka wa tatu mfululizo wanatinga kwa kishindo kwenye tuzo za Kilimanjaro Tanzania Music Awards na sasa baadhi watu wale wale aina ya mashabiki maandazi wanaanza kuhoji kwa nini Mashujaa kila mwaka, wanaanza kusema labda kwa sababu mtu fulani yupo kwenye kamati flani …yale yale ya Mayweather kashinda kwa sababu ya majaji wanatoka Marekani.
    Watu wanapaswa kujua kuwa kila kitu na zama zake, kulikuwa na enzi za Mohamed Ali, zikaja zama za Mike Tyson. Wala haihitaji kutumia nguvu nyingi kuporomosha zama za mwenzako, kama ipo ipo na kama hakuna ni hakuna.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAYWEATHER ANAVYONIKUMBUSHA MASHABIKI MAANDAZI WA MUZIKI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top