• HABARI MPYA

    Sunday, May 03, 2015

    YANGA SC WASIPOJIFUNZA KUTOKANA NA MAKOSA, WATAISHIA KUFA KIUME!

    REKODI ya timu za Tanzania kutolewa mapema katika michuano ya Afrika imeendelea jana, baada ya Yanga SC kuhitimisha safari yake mbele ya Etoile du Sahel ya Tunisia.
    Hiyo inafuatia Yanga SC kufungwa bao 1-0 na wenyeji Etoile du Sahel katika mchezo wa marudiano hatua ya 16 Bora Kombe la Shirikisho Afrika Uwanja wa Olimpiki mjini Sousse, Tunisia.
    Etoile sasa watacheza na timu moja zilizotolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika kuwania nafasi ya kupangwa katika makundi ya Kombe la Shirikisho, wakati Yanga SC wanarudi nyumbani kusubiri mwakani.
    Etoile walipata bao hilo kipindi cha kwanza, mfungaji Ammar Jemal, kwa kichwa akimalizia krosi ya Alkhali Bangoura dakika ya 24.

    Jemal aliurukia mpira uliompita kipa Deo Munishi ‘Dida’ akiwa peke yake pembezoni mwa lango na kuutumbukizia nyavuni kiulaini.
    Etoile ndiyo walioanza kulitia misukosuko lango la Yanga SC, baada ya Soussi Zied kushindwa kumalizia kwa kichwa mpira wa adhabu uliopigwa na Tej Marouen dakika ya saba.
    Kevin Yondan alifanya kazi nzuri dakika ya tisa baada ya kuokoa mpira ambao tayari ulikuwa umempita kipa wake, Dida uliopigwa na Soussi dakika ya tisa.
    Dakika ya 18 Mouhbi Youssef alipoteza nafasi baada ya shuti lake kutoka nje kidogo kufuatia krosi ya Naguez Hamdi.
    Yanga SC ilifanya shambulizi la kwanza dakika ya 26, lakini mpira wa kichwa uliopigwa na mshambuliaji Amissi Tambwe uligonga mwamba kufuatia krosi ya Juma Abdul.
    Mshambuliaji Mliberia, Kpah Sherman alipiga juu ya lango dakika ya 33 baada ya kupokea krosi nzuri ya Mrisho Ngassa.
    Etoile ilipata pigo dakika ya 42, baada ya kiungo wake tegemeo, Mcameroon Frank Kom kuonyeshwa kadi ya pili ya njano na kutolewa kwa kadi nyekundu.
    Kom alionyeshwa kadi hiyo na refa Dennis Batte wa Uganda baada ya kumchezea rafu winga Simon Msuva, wakati tayari alikuwa ana kadi ya njano aliyoonyeshwa mapema dakika ya tisa kwa kumchezea rafu Ngassa.
    Kipindi cha Yanga SC walikianza vizuri wakipeleka mashambulizi mfululizo langoni mwa Etoile, ambayo ilionekana dhahiri kuathiriwa na kupoteza mtu mmoja, tena muhimu, Kom.
    Katika kuhakikisha wanaulinda ushindi, Etoile wakaanza kucheza mchezo wa kujihami na kufanya mashambulizi ya kushitukiza.
    Hiyo iliwapa Yanga nafasi ya kutawala mchezo, lakini hawakuwa na madhara kwenye eneo la hatari la wapinzani wao hao.
    Yanga SC wanarudi nyumbani wakijifariji kwa matokeo ya kufungwa 1-0 tu, tofauti na miaka ya nyuma ilipokuwa inarejea na kapu la mabao inapokwenda Kaskazini mwa Afrika.
    Kitu kimoja tu nilikumbuka baada ya mchezo ule, namna ambavyo Yanga SC walicheza kwa woga mchezo wa kwanza Dar es Salaam, tofauti na walivyocheza jana.
    Jana wachezaji wa Yanga SC walijitoa kwa asilimia zote uwanjani na walipambana kiasi cha kuwatia woga wenyeji.
    Vurugu za mara kwa mara zilizokuwa zikitokea uwanjani jana wachezaji wa Etoile wakitaka kupigana na wa Yanga zilikuwa kielelezo tosha cha ugumu wa mchezo huo.
    Mchezo wa jana ulikuwa wa pande zote mbili, Etoile walitumia nafasi moja tu kati ya zisizopungua tano walizotengeneza kufunga baio muhimu.
    Yanga SC walitengeneza nafasi mbili nzuri n azote wakashindwa kutumia. Na mbaya zaidi, wakashindwa kutumia mwanya wa Etoile kucheza pungufu kuweza kujipatia bao, kama si mabao.
    Lakini matokeo ya jana si ya kujutia sana, bali matokeo ya mchezo wa kwanza. Yanga SC ilipoteza nafasi ya kusonga mbele katika mchezo wa Dar es Salaam.
    Kitendo cha kukubali kulazimishwa sare nyumbani ndicho kiliwaathiri jana. 
    Lakini, kwa vyovyote historia ya Yanga mwaka huu imefungwa. Inaishia 16 Bora Kombe la Shirikisho.
    Ni mwaka huu tu Yanga haitaonekana tena katika michuano ya Afrika. Lakini mwakani watarudi tena, wakishiriki Ligi ya Mabingwa kutokana na kuwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Bara.
    Mapungufu ya wazi yameonekana katika kikosi cha Yanga SC ili kufikia ubora wa kucheza katika kiwango cha ushindani michuano ya Afrika kwa mfano ubora wa wachezaji.
    Kuna aina ya wachezaji wanatakiwa katika kikosi cha Yanga ili timu iwe na ubora wa kushindana katika michuano mikubwa. Je, benchi la Ufundi la klabu chini ya Kocha Mkuu, Mholanzi Hans van der Pluijm limeliona hilo?  
    Kuna aina ya maandalizi ambayo Yanga SC wanastahili kufanya ili kufikia ubora wa kushindana kwenye michuano ya Afrika. Kwa ujumla, Yanga SC inahitaji kuwa aina ya timu ambazo inashindwa kuzitoa katika michuano ya Afrika.
    Tofauti na hivyo wataendelea kupongezwa kwa kuonyesha ushindani wakipewa sifa za kijinga; Yanga yafa kiume na nyingine kibao. Alamsiki. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC WASIPOJIFUNZA KUTOKANA NA MAKOSA, WATAISHIA KUFA KIUME! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top