![]() |
Azam FC |
Na Princess Asia
KATIKA
kujiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii, dhidi ya Simba SC Jumanne ijayo, Azam FC
jana walicheza mechi ya kujipima nguvu na timu ya vijana ya klabu yao, Azam
Academy na kuibuka na ushindi wa mabao 4-0.
Mabao ya
Azam katika mchezo huo kwenye Uwanja wa Chamazi, yalifungwa na Abdi Kassim Sadallah
‘Babbi’, Kipre Herman Tcheche na Kipre Michael Balhou.
Kocha wa
Azam Academy, Iddi Cheche alisema kipigo hicho ni kwa sababu alikosa wachezaji
wake 10 wa kikosi cha kwanza, wanane wakiwa na timu ya taifa ya vijana chini ya
umri wa mikaka 17, Serengeti Boys na wawili majeruhi.
Wakati huo
huo, hali ya viungo Ibrahim Mwaipopo na Salum Abubakar ‘Sure Boy Jr.’, Jabir
Aziz na Hamisi Mcha ‘Vialli’ na beki wa kushoto, Salum Waziri ambao ni majeruhi
inaendelea vizuri na kesho wanaweza kuanza mazoezi.
Wachezaji
wote hao watano wanaendelea vizuri na tiba na kuna matumaini wanaweza kuwa fiti
kwa mechi ya Ngao ya Jamii, Septemba 11 dhidi ya Simba, Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Wachezaji hao
wamekuwa wakifanya mazoezi mepesi, wakiongozwa na daktari wa timu hiyo, Dk
Mwanandi Mwankemwa kuanzia gym hadi uwanjani. Dk. Mwanandi anasema wachezaji
hao hali zao zinatia matumaini kwa sasa na wataendelea kuwaangalia hadi
mwishoni mwa wiki ili kujua maendeleo yao.
Azam
inatarajiwa kuivaa Simba katika mechi ya Ngao ya Jamii ya kuashiria kufunguliwa
kwa pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Septemba 11, mwaka huu, Uwanja
wa Taifa, Dar es Salaam, ikiwa ni mchezo wake wa kwanza katika historia ya Ngao
hiyo.
Kihistoria
hiyo itakuwa mechi ya tano ya Ngao ya Jamii kuchezwa nchini na ya pili
kuishirikisha timu nje ya wapinzani wa jadi wa soka ya Tanzania, Simba na
Yanga.
Mtibwa
ilicheza na Yanga mwaka 2009, baada ya Simba kugoma na ikashinda mabao 2-1 na
kutwaa Ngao, wakati kabla ya hapo, mwaka 2001, Ligi Kuu ya Tanzania ikiwa bado
inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Safari Lager,
ilichezwa mechi ya kwanza ya Ngao kihistoria.
Katika mechi
hiyo, Yanga ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Simba na mwaka juzi Yanga iliifunga
tena Simba kwa penali 3-1 kufuatia sare ya 0-0 na mwaka jana, Simba ilitwaa
Ngao ya kwanza katika historia yake, kwa kuifunga Yanga mabao 2-0.
Ikumbukwe
mara ya mwisho Simba SC ilipokutana na Azam FC, katika Robo Fainali ya Klabu
Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame mwezi uliopita Dar es Salaam,
ilifungwa mabao 3-1, yote yakifungwa na Bocco na lile la kufutia machozi kwa
wekundu hao Msimbazi liliwekwa kimiani na beki mahiri Shomari Kapombe,
aliyemajeruhi kwa sasa.
0 comments:
Post a Comment