![]() |
Simba SC |
Na Mahmoud Zubeiry
SIMBA SC,
mabingwa wa soka Tanzania Bara, leo watamenyana na waliowahi kuwa mabingwa wa
Kenya, Sofapaka FC, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanazia saa 10:00 jioni.
Katika mchezo
wa leo, mashabiki wa Simba SC wa Dar es Salaam, yalipo maskani ya klabu hiyo
katika Mtaa wenye pilika nyingi, Msimbazi, watawashuhudia wachezaji wapya wa
kigeni, mabeki Paschal Ochieng, Komabil Keita na mshambuliaji kutoka Ghana,
Daniel Akuffo.
Ochieng amesajiliwa
kutoka AFC Leopard ya Kenya, Keita kutoka Stella Abidjan ya Ivory Coast na
Akuffo kutoka Hearts Of Oak ya Ghana na wote hawajawahi kucheza Uwanja wa
Taifa, hivyo leo itakuwa mara ya kwanza kwao na mashabiki wa Simba wana hamu sana
ya kuona silaha hizo mpya.
Lakini kikubwa
ni kushuhudia mseto mpya wa timu yao kuanzia safu ya ulinzi, kiungo hadi
ushambuliaji na namna timu yao ilivyoiva baada ya kujifua kwa zaidi ya siku 40,
ikijiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu.
Simba,
ambayo mara ya mwisho Simba ilicheza Dar es Salaam Agosti 8, na kufungwa mabao
3-1 na City Stars ya Nairobi, Kenya Uwanja wa Taifa, kwa zaidi ya mwezi mmoja
ilikuwa kambini Arusha ikijifua vikali kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara, ambao wao ni mabingwa watetezi.
Kwa sasa
kiwango cha Simba, inayofundishwa na Mserbia, Profesa Milovan Cirkovick,
akisaidiwa na Mganda, Richard Hamatre, kipo vizuri na timu inaonekana iko
tayari kwa Ligi Kuu.
Pamoja na Jumapili
kulazimishwa sare ya 1-1 na Sony Sugar ya Kenya, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid
mjini Arusha, lakini Simba ilicheza soka safi na washambuliaji wake walikosa
mabao ya wazi zaidi ya matano.
Lakini hata
hali mbaya ya Uwanja wa Sheikh Amri Abeid katika eneo la kuchezea inachangia
kupunguza idadi ya mabao kwa Simba. Katika mechi tatu ambazo Simba imecheza
kwenye Uwanja huo, imevuna mabao matano na kufungwa matatu, na kikwazo kimekuwa
kikionekana ni hali ya eneo la kuchezea.
Katika
mchezo wa Jumapili, bao la Simba lilifungwa na Daniel Akuffo, wakati Komabil
Keita alijifunga katika jitihada za kuokoa na kuwapa Wakenya bao la kuongoza. Awali,
Simba ilicheza mechi mbili Arusha, dhidi ya Mathare United ya Kenya na JKT
Oljoro ya Arusha, ambazo zote ilishinda 2-1, mshambuliaji mpya Daniel Akuffo
kutoka Ghana akifunga bao moja kila mechi, Kiggi Makaasy na Mrisho Ngassa
wakifunga mabao mengine.
Kitu kimoja
tu ambacho Milovan anapaswa kuendelea kufanyia kazi ni makosa ya safu ya ulinzi
na mawasiliano duni na makipa wao.
Ilivyo sasa
kipa yeyote anayesimama kwenye lango la Simba SC, kabla ya kuchunga wachezaji
wa timu pinzani, anakuwa na jukumu la kwanza la kujihadhari na mabeki wake
wasimfunge, kwani mabeki wawili wa kati wa timu hiyo wamekwishaonyesha
‘kipaji cha kujifunga’ katika mechi za
karibuni, Juma Nyosso na Komabil Keita.
Simba
inajiandaa na mechi ya Ngao ya Jamii Septemba 11, mwaka huu, Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam dhidi ya Azam FC, ambayo kihistoria hiyo itakuwa mechi ya tano ya
Ngao ya Jamii kuchezwa nchini na ya pili kukutanisha timu nje ya wapinzani wa
jadi wa soka ya Tanzania, Simba na Yanga.
Mtibwa
ilicheza na Yanga mwaka 2009, baada ya Simba kugoma na ikashinda mabao 2-1 na
kutwaa Ngao, wakati kabla ya hapo, mwaka 2001, Ligi Kuu ya Tanzania ikiwa bado
inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Safari Lager,
ilichezwa mechi ya kwanza ya Ngao kihistoria.
Katika mechi
hiyo, Yanga ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Simba na mwaka juzi Yanga iliifunga
tena Simba kwa penali 3-1 kufuatia sare ya 0-0 na mwaka jana, Simba ilitwaa
Ngao ya kwanza katika historia yake, kwa kuifunga Yanga mabao 2-0.
MABINGWA WA MECHI ZA NGAO YA JAMII:
Mwaka Mshindi Matokeo
2001 Yanga 2-1 Simba
2010 Yanga 0-0 Simba (3-1penalti)
2011 Simba 2-0 Yanga
0 comments:
Post a Comment