![]() |
Kikosi cha Azam kilichochecheza mechi ya mwisho na Coastal Chamazi |
Na Princess Asia
CHUMBA cha
majeruhi cha klabu ya Azam kimepokea wageni watatu na sasa kufanya idadi ya
wachezaji watano.
Mbali na
viungo Ibrahim Mwaipopo na Salum Abubakar ‘Sure Boy Jr.’, majeruhi wengine wa
Azam ni viungo Jabir Aziz na Hamisi Mcha ‘Vialli’ na beki wa kushoto, Salum
Waziri. Wachezaji wote hao watano wanaendelea vizuri na tiba na kuna matumaini
wanaweza kuwa fiti kwa mechi ya Ngao ya Jamii, Septemba 11 dhidi ya Simba,
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Wachezaji hao
wanafanya mazoezi mepesi, wakiongozwa na daktari wa timu hiyo, Dk Mwanandi
Mwankemwa kuanzia gym hadi uwanjani. Dk. Mwanandi anasema wachezaji hao hali
zao zinatia matumaini kwa sasa na wataendelea kuwaangalia hadi mwishoni mwa
wiki ili kujua maendeleo yao.
Wachezaji
wote hao hakuwemo kwenye mechi ya kirafiki Jumapili dhidi ya Coastal Union ya
Tanga, kwenye Uwanja wa Chamazi, kujiandaa na mechi hiyo dhidi ya Simba.
Katika mechi
hiyo iliyokuwa tamu, mabao mawili ya John Raphael Bocco ‘Adebayor’ katika
dakika za 15 na 44, yaliipa Azam FC ushindi wa mabao 2-0 Uwanja wa Chamazi.
Bocco
alikuwa mwiba mchungu kweli siku hiyo kwa safu ya ulinzi ya Coastal, kwani
pamoja kufunga mawili, lakini alikosa mabao matatu ya wazi mno katika mechi
ambayo, kiungo Abdulhalim Humud alitolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 32
kwa rafu na lugha chafu.
Hiyo ni
mechi ya tano Coastal inafungwa kati ya sita za kujipima nguvu ilizocheza kabla
ya Jumamosi kufungwa 2-1 na Yanga, awali ilifungwa 3-2 na Bandari mjini
Mombassa, baadaye 2-0 Tanga, ilifungwa 2-1 na Polisi mjini Morogoro na yenyewe
iliifunga JKT Oljoro 1-0.
Kwa Azam hiyo
ni mechi ya tatu mfululizo ya kujipima nguvu wanashinda, awali walizifunga 1-0
Prisons ya Mbeya na Transit Camp 8-0.
Azam
inatarajiwa kuivaa Simba katika mechi ya Ngao ya Jamii ya kuashiria kufunguliwa
kwa pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Septemba 11, mwaka huu, Uwanja
wa Taifa, Dar es Salaam, ikiwa ni mchezo wake wa kwanza katika historia ya Ngao
hiyo.
Kihistoria
hiyo itakuwa mechi ya tano ya Ngao ya Jamii kuchezwa nchini na ya pili
kuishirikisha timu nje ya wapinzani wa jadi wa soka ya Tanzania, Simba na
Yanga.
Mtibwa
ilicheza na Yanga mwaka 2009, baada ya Simba kugoma na ikashinda mabao 2-1 na
kutwaa Ngao, wakati kabla ya hapo, mwaka 2001, Ligi Kuu ya Tanzania ikiwa bado
inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Safari Lager,
ilichezwa mechi ya kwanza ya Ngao kihistoria.
Katika mechi
hiyo, Yanga ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Simba na mwaka juzi Yanga iliifunga
tena Simba kwa penali 3-1 kufuatia sare ya 0-0 na mwaka jana, Simba ilitwaa
Ngao ya kwanza katika historia yake, kwa kuifunga Yanga mabao 2-0.
Ikumbukwe
mara ya mwisho Simba SC ilipokutana na Azam FC, katika Robo Fainali ya Klabu
Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame mwezi uliopita Dar es Salaam,
ilifungwa mabao 3-1, yote yakifungwa na Bocco na lile la kufutia machozi kwa
wekundu hao Msimbazi liliwekwa kimiani na beki mahiri Shomari Kapombe,
aliyemajeruhi kwa sasa.
0 comments:
Post a Comment