![]() |
Wachezaji wa Simba SC |
AL Ahly Shandy ina fungu la kutosha na mikakati mizito kuhakikisha inaing'oa Simba katika mechi ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho, lakini kwenye Ligi Kuu Sudan bado inapepesuka. Al Ahly inayoshiriki kwa mara ya kwanza michuano ya kimataifa tangu ianzishwe ikiwa ni timu changa kama Azam, itacheza na Simba jijini Dar es Salaam katika mechi ya kwanza Aprili 29 kabla ya kurudiana jijini Khartoum Mei 11. Mwandishi Mwandamizi wa Redio Sudan, Yousif Mohamed Yousif, aliiambia Mwanaspoti jana Ijumaa kwa njia ya simu kwamba timu hiyo ni changa kwenye ligi ya Sudan na sasa inashikilia nafasi ya tano ikiwa na pointi 10, ingawa iko makini. "Wamejipanga kifedha na wana bajeti ya kutosha, wana wachezaji wazuri chipukizi na wazoefu, ni timu ya watu wenye fedha ndiyo maana nakwambia wana nafasi kubwa ya kusonga mbele," alisema. "Maandalizi yao ni mzuri, ninavyoongea na wewe wanaendelea na ligi ya hapa Sudan. Wanacheza kwa ushirikiano mkubwa ingawa bado wako kwenye nafasi za chini. "Bado hawajataka kuzungumzia sana mambo ya Simba, wanajipanga vizuri wenyewe kwanza katika maandalizi ya ndani. "Lakini nadhani wiki ijayo watakapoingia kambini rasmi kujiandaa na Simba tutajua mambo mengi zaidi." Mtangazaji huyo ni miongoni mwa wachambuzi wanaosifika sana jijini Khartoum na hakosekani katika safari yoyote ya timu ya taifa ya Sudan. Katika msimamo wa Ligi Kuu ya Sudan yenye timu 14, timu zote zimecheza mechi saba mpaka sasa na wapinzani hao wa Simba wapo kwenye nafasi ya tano wakiwa na pointi 10. Wameshinda michezo miwili na kutoka sare minne huku wakipoteza mmoja. Wamefunga mabao saba na kufungwa matano. Al Hilal inaongoza msimamo kwa pointi 19, ikifuatiwa na El Merreikh yenye pointi 15. Katika raundi ya awali ya Kombe la Shirikisho, timu hiyo iliifunga Ferroviario bao 1-0 mjini Maputo na katika marudiano ikaisulubu mabao 2-0. |
GAZETI LA MWANASPOTI LEO |
0 comments:
Post a Comment