• HABARI MPYA

    Monday, April 16, 2012

    CHACHA MARWA AONDOKA KAMBINI YANGA, THEO RUTTA ASAFIRISHWA, KUZIKWA JUMATANO

    Chacha kulia
    KLABU ya Yanga ya Dar es Salaam imezidi kuingia katika wakati mgumu, baada ya beki wake tegemeo, Chacha Marwa kuondoka kambini Mwanza leo baada ya kufiwa na mtoto wake.
    Chacha amepanda ndege leo mjini Mwanza kurejea Dar es Salaam kwa ajili ya msiba wa mwanawe, wakati timu inaelekea Kagera kwa ajili ya mchezo mwingine wa Ligi Kuu ya Vodacom Bara, ikitoka kufungwa 3-2 na Toto African mjini Mwanza jana.
    Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu ameiambia bongostaz.blogspot.com mchana huu kwamba, Chacha anarejea Dar kwa mazishi ya mwanawe na kufanya mwendelezo wa kipindi kigumu kwa klabu yao.
    “Kama inavyofahamika tupo kwenye msiba wa Mjumbe wa Kamati yetu ya Utendaji (Theonist) Rutashoborwa ambaye atazikwa Jumatano Bukoba.
    Hatujamaliza hilo, linakuja na hili na Chacha kufiwa na mwanawe, kwa kweli hiki ni kipindi kigumu kwa klabu yetu,”alisema Sendeu.
    Chacha anaacha pigo kubwa kwenye safu ya ulinzi ya Yanga, ambayo kwa sasa inamkosa beki wake mahiri wa kati, Nadir Haroub Ally ‘Cannavaro’ anayetumikia adhabu.
    Maana yake sasa, zaidi ya Athumani Iddi ‘Chuji’ aliyerejeshwa kwenye ulinzi kutoka kiungo, mabeki wa kati Yanga wanabaki wawili tu na ambao wote si chaguo la kwanza, Bakari Mbega na Job Ibrahim.
    Yanga jana imeliweka rehani taji lake la ubingwa wa Ligi Kuu, kufuatia kipigo cha mabao 3-2 kutoka kwa Toto African mjini Mwanza na hivyo kuziachia Simba SC na Azam FC mbio za ubingwa.
    Simba SC inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 53, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 50 wakati Yanga ni ya tatu kwa pointi zake 43, ingawa iko nyuma kwa mchezo mmoja dhidi ya timu hizo mbili zilizo juu yake.  
    Yanga pia inategemea kushinda rufaa iliyokata kupinga kupokonywa pointi tatu ilizopata kwenye mechi dhidi ya Coastal Union wiki mbili zilizopita mjini Tanga, ili angalau kurejesha matumaini ya kutetea ubingwa.
    Yanga ilipokonywa pointi hizo baada ya kumtumia beki Cannavaro, wakati alikuwa anatumikia adhabu ya kadi nyekundu.
    Lakini klabu hiyo imeikatia rufaa hiyo, kwa sababu inadai iliruhusiwa kumtumia beki huyo na Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu ya TFF, Alfred Tibaigana.
    Wakati huo huo: Mwili wa aliyekuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Theonist Rutashoborwa umesafirishwa leo kwenda Bukoba kwa mazishi yatakayofanyika Jumatano.
    Sendeu alisema baada ya sala na kuagwa kwa mwili huo leo, umesafirishwa na mazishi yatafanyika Jumatano.
    Rutta atakumbukwa sana Yanga, hasa kutokana na jitihada zake zilizoisaidia klabu hiyo kupata ufadhili wa Yussuf Manji mwaka 2006. Mungu aiweke pema peponi roho ya marehemu. Amin.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: CHACHA MARWA AONDOKA KAMBINI YANGA, THEO RUTTA ASAFIRISHWA, KUZIKWA JUMATANO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top