• HABARI MPYA

    Saturday, April 14, 2012

    YANGA WAPIGA DILI LIKIFELI WAMEUMIA

    YANGA inacheza penalti ya mwaka nje ya uwanja na ikiikosa hiyo basi itafunga hesabu na kukabidhi kila kitu kwa Simba na Azam, lakini Fred Minziro amesisitiza Yaw Berko amerudi uwanjani vizuri kujiunga na makipa wenzake, Shabaan Kado na Said Mohammed.
    Uongozi pia umetoa tamko zito kwamba kocha Kosta Papic haendi kokote na atakaa kwenye benchi la ufundi mpaka msimu wa Ligi Kuu Bara umalizike Mei 5, 2012.
    Simba inaongoza Ligi Kuu Bara kwa pointi 50 ikifuatiwa na Azam yenye 47 na Yanga 43. Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ambaye pia ni bosi wa Kamati ya Fedha na Mipango wa Yanga, Salum Rupia, amesema: "Hii rufaa tuliyokata kwa Kamati ya Nidhamu ya TFF ni kama penalti, tukikosa hapo ubingwa basi.
    "Ni kitu cha wazi kabisa, Simba watakuwa mabingwa. Pengo la pointi litakuwa kubwa watakuwa wametuzidi mbali, lakini tukishinda rufaa tutakuwa na tofauti ya pointi nne ambazo ni rahisi kuzifuta, kwa sababu tukikutana nao tutawapiga.
    "Simba hawawezi kutufunga, kwani safari hii tuko fiti sana na huwa wanatuzidi vitu vidogo tu, tulishawajulia na kuwadhibiti siku nyingi ndiyo maana siku hizi hawatuwezi."
    Rupia anakiri kuwa uwezekano wa Simba kushinda mechi tatu kati ya nne ilizobakiza ni mkubwa ndiyo maana wao wanategemea rufaa waliyokata kupinga kupokwa pointi tatu kwenye mechi dhidi ya Coastal Union walipomchezesha Nadir Cannavaro aliyekuwa na kadi nyekundu.
    Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema: "Kamati ya Nidhamu ya TFF iliyokuwa ikutane Jumamosi (leo) kujadili rufaa ya Yanga, imeahirisha mkutano wake hadi Jumanne ya Aprili 17."
    Kamati hiyo iko chini ya uenyekiti wa Kamishna Mstaafu wa Polisi, Alfred Tibaigana.
    Yanga inapiga hesabu kwamba endapo ikirudishiwa pointi tatu itafikisha 46 na kubakiza pengo la pointi nne na Simba ambao wamedai wataifunga watakapocheza nayo Mei 5.
    Rupia alisema: "Kama mambo yatashindikana inabidi kutafuta nafasi ya Kombe la Shirikisho, lakini tutashinda mechi zote tano tulizonazo mkononi, ikiwemo Simba, hilo halina mjadala, tunajiamini kwa kusema hivyo na tunajua tutapataje hizo pointi."
    Katibu Mkuu wa Yanga, Selestine Mwesigwa amesema: "Kuhusu suala la Papic, ninakuhakikishia haendi kokote, mkataba wake nimeusaini mimi una kipengele kinachoeleza atakuwa kocha wa Yanga mpaka mwisho wa msimu wa Ligi hata kama ikimalizika mwakani.
    "Kila kitu kipo kwenye maandishi na nakala anayo, yeye anajua haya ninayosema."
    Papic, ambaye amesisitiza kwamba mkataba wake unamalizika Aprili 24, hayupo na Yanga iliyopo Mwanza kujiandaa na mechi ya kesho Jumapili dhidi ya Toto Africa kwa maelezo kuwa ni mgonjwa na Mwesigwa amethibitisha anatibiwa.
    Kocha Msaidizi Fred Minziro alizungumza na Mwanaspoti jana Ijumaa kutoka Mwanza na kusema: "Wachezaji wote wako safi, tunataka kushinda kwanza hizi mechi mbili dhidi ya Toto na Kagera huku ugenini halafu mambo mengine yaendelee.
    "Tumeshazungumza na wachezaji kwamba sisi tunacheza mechi zetu zote tushinde, hatuangalii mambo ya Simba, Azam wala timu nyingine. Mwisho wa siku tukimaliza kazi na pointi zetu mkononi ndiyo tutajua nani mbabe."
    Minziro amethibitisha kuwa Berko anaendelea vizuri na kwamba ana uwezo wa kucheza kama wenzake baada ya kuwa nje muda mrefu.
    GAZETI LA MWANASPOTI LEO
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA WAPIGA DILI LIKIFELI WAMEUMIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top