• HABARI MPYA

    Monday, April 16, 2012

    CHELSEA WAHARAKISHA TEKNOLOJIA KWENYE GOLI ENGLAND

    Spurs wakimlalamikia refa Atkinson
    Ekotto akikzuia shuti la Mata kabla halijavuka mstari
    JARIBIO la mwisho la kutumia teknolojia kwenye mstari wa goli, litafanyika baadaye mwezi huu kabla ya watengeneza sheria wa FIFA kutoa uamuzi Julai, mwaka huu, bongostaz imeipata hiyo kutoka FIFA baada ya utata mwingine mkubwa kujitokeza jana.
    Chelsea imetinga fainali ya Kombe la FA kwa ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Tottenham, huku marudio ya kamera yakionyesha shuti la Juan Mata lililoipatia Chelsea bao la pili halikuvuka mstari.
    ''Tumekuwa tukililia teknolojita kutumika kwenye mstari wa goli kwa muda mrefu sasa,'' alisema beki wa Chelsea, John Terry. ''Acha tutumai sasa watu watachukua uamuzi sahihi.''
    Bodi ya Vyama vya Soka ya Kimataifa, Bodi ya Kutunga Sheria za Mchezo, mwezi uliopita waliafiki mifumo miwili kuingia katika awamu ya pili ya jaribio la teknolojia kabla haijaruhusiwa kutumika katika kikao cha Julai 2.
    ''Kikao cha mwisho kilipangwa kufanyika Ijumaa, na awamu ya pili ya jaribio itafanyika mwishoni mwa Aprili, na itaendelea hadi Mei,'' imesema FIFA katika taarifa yake iliyoifikia bongostaz.   
    IFAB lazima ijiridhishe na kasi na ufasaha wa kifaa cha Hawk-Eye au GoalRef kabla kuamua viwe msaada kwa marefa katika uamuzi juu ya mabao yenye utata wa kuvuka au kutovuka mstari.
    Kamera aina ya Hawk-Eye ya Sony Corp ni kamera inayoendana na kasi ya mpira na inafanya kazi kwa ufanisi mkubwa na kuaminika katika tenisi na Kriketi. GoalRef, inamilikiwa na kampuni ya Mjerumani Denmark, ambayo wataalamu wengi wanaamini inaweza kuwa suluhisho.
    Mifumo yote miwili inatoa jibu kwa refa ndani ya sekunde tu kuhusu mpira kama umevuka mstari wa goli, ambayo itatoa nguvu ya kutoa uamuzi wa mwisho.
    Katika mechi ya Jumapili, Uwanja wa Wembley, marudio ya Televisheni mara moja yalionyesha kwamba shuti la Mata mwanzoni mwa kipindi cha pili, halikuvuka mstari wa goli na lilizuiwa vema na beki wa Tottenham, Benoit Assou-Ekotto kwa umahiri mkubwa.
    Hata wachezaji wa Chelsea, baadaye walikiri bao hilo halikupaswa kukubaliwa.
    FIFA iliamua kuunga mkono teknolojia kwenye mstari wa goli baada ya tukio la kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010 lililoihusisha timu ya Terry, England na kumshawishi rais Sepp Blatter kwamba usumbufu huo ni vema ukaepukwa katika michuano mikubwa.
    Shuti la kiungo wa Chelsea, Frank Lampard katika mechi na Ujerumani kwenye Fainali za Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini liligonga mwamba wa juu na kuangukia ndani ya mstari wa goli, lakini halikuhesabiwa kama bao na England ikatolewa mashindanoni.
    FIFA inatumaini mojawapo ya mifumo hiyo itakuwa tayari kutumika Desemba katika Klabu Bingwa ya Dunia nchini Japan.
    Lakini kwa Ligi Kuu, matumaini ni kwamba itawekeza mfumo huo kwenye viwanja vyake 20 kabla ya kuanza msimu mpya Julai.
    IFAB inaundwa na vyama vitatu vya soka Uingereza jumlisha wajumbe wanne wa FIFA, na kura sita ndizo zitaamua juu ya mabadiliko hayo.
    Martin Atkinson, refa mwenye heshima kubwa FIFA, ambaye alitoa bao hilo la utata jana katika Nusu Fainali ya FA, atakuwa mmoja wa wasaidizi wa Howard Webb katika teknolojia ya bao kwenye michuano ya Kombe la Mataifa Ulaya, Euro 2012 inayoanza Juni 8 hadi Julai 1, mwaka huu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: CHELSEA WAHARAKISHA TEKNOLOJIA KWENYE GOLI ENGLAND Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top