![]() |
Irene Uwoya, mmoja wa masupa staa wa bongo muvi |
TIMU ya taifa ya soka ya
wanawake, Twiga Stars itacheza mechi ya kirafiki na timu ya wasanii wa filamu
ya Bongo Movie itakayofanyika Jumamosi (Aprili 14 mwaka huu) Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam.
Ofisa Habari wa Shirikisho la
Soka Tamnzania (TFF), Boniface Wambura Mgoyo amesema lengo la mechi hiyo ya
maonesho (exhibition) ni kuichangia Twiga Stars ambayo hivi sasa iko kwenye
mashindano ya mchujo ya Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) ambayo fainali zake
zitafanyika Novemba mwaka huu nchini Equatorial Guinea.
Pia asilimia mbili ya mapato
yatakayopatikana kwenye mechi ya Twiga Stars na Bongo Movie yatakwenda kwenye
familia ya mwigizaji nguli wa filamu Tanzania, Stephen Kanumba aliyefariki
dunia Aprili 7 mwaka huu.
Kiingilio katika mechi hiyo
kitakuwa sh. 10,000 kwa VIP A, sh. 5,000 kwa VIP C na B na sh. 2,000 kwa viti
vya rangi ya chungwa, kijani na bluu. Mechi itaanza saa 10 kamili jioni.
Twiga Stars itacheza mechi ya
kwanza ya mchujo dhidi ya Ethiopia jijini Addis Ababa. Mechi hiyo itachezwa Mei
26 mwaka huu na wiki mbili baadaye timu hizo zitarudiana jijini Dar es Salaam.
Twiga Stars ilifuzu raundi hiyo baada ya kuitoa Namibia kwa jumla ya mabao 7-2.
Machi 10 mwaka huu, Naibu Waziri
wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara alizindua
akaunti ya Twiga Stars kupitia Tigo Pesa kuichangia timu hiyo ambayo inashiriki
michuano ya AWC. Wachangiaji wanatakiwa kutuma mchango wao kwenda namba 13389.
0 comments:
Post a Comment