![]() |
Jerry Santo |
KIUNGO wa kimataifa wa Kenya, Jerry Santo amesema yuko
tayari kurejea klabu yake ya zamani ya Simba, iwapo itafuzu kuingia hatua ya
makundi ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Katika mahojiano maalum (online) na bongostaz, Santo amesema
kutoka Nairobi kwamba aliondoka Simba ili akacheze Albania lakini hakufanikiwa
na wakati huo usajili wa Bara ulikuwa umekwishafungwa.Alisema aliondoka Simba vizuri Novemba mwaka jana, baada ya kumaliza mkataba wake akiwa na lengo la kwenda kujiendeleza zaidi kisoka, lakini kwa bahati mbaya hakufanikiwa.
“Yalitokea mabadiliko ya uongozi katika klabu ambayo nilikuwa nakwenda, wale viongozi walionitaka waliondolewa madarakani, kwa hiyo ikashindikana mimi kucheza.
Nikarudi Nairobi, kwa bahati nzuri usajili wetu ulikuwa haujafungwa na mimi nikasajiliwa na timu yangu ya zamani, Tusker na nipo nacheza hapa sasa,” alisema.
Alipoulizwa kama uongozi wa Tusker utamruhusu kuondoka, alisema hilo halina tatizo kabisa kulingana na makubaliano na klabu hiyo wakati anasaini mwaka huu.
Aidha, Santo aliipongeza Simba kwa kufanikiwa kutinga hatua ya 16 Bora ya Kombe la Shirikisho, ikiitoa timu ngumu ya ES Setif ya Algeria katika hatua ya 32 Bora.
Alisema atafurahi kuungana tena na wachezaji aliokuwa nao Simba kama mshambuliaji Emmanuel Okwi, kipa Juma Kaseja na wengine wote.
“Simba ni timu nzuri ambayo niliitumikia kwa uaminifu mkubwa na haikuwa na tatizo kuniruhusu kuondoka nilipopata nafasi Albania. Sioni kwa nini nisirudi wakinihitaji,”alisema kiungo huyo ambaye wakati anaondoka ‘aliwaliza’ Simba wengi.
Nafasi ya Santo kurejea Simba ipo kwa sababu hivi sasa klabu hiyo japokuwa ina wachezaji watano wa kigeni wanaokamilisha idadi kulingana na kanuni za usajili wa wachezaji wa kigeni Tanzania, lakini ni watatu tu wanaoingia kwenye kikosi cha kwanza chini ya kocha Mserbia, Milovan Cirkovic ambao ni Okwi kutoka Uganda, Patrick Mafisango kutoka Rwanda na Mzambia Felix Sunzu.
Mganda Derrick Walullya anayecheza nafasi ya ulinzi hana nafasi kabisa, wakati Gervais Kago kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati anayecheza nafasi ya ushambuliaji, zaidi hutokea benchi na wakati mwingine huishia kuwa mtazamaji dakika zote 90.
Lakini pia Simba inasumbuliwa mno na nidhamu ya Mafisango anayecheza nafasi moja na Santo na mapema mwezi huu ilimsimamisha kabla ya safari ya kwenda Algeria kurudiana na Setif.
Na japokuwa ilielezwa Mafisango aliomba radhi akasamahewa na kusafiri na timu Algeria, lakini ukweli ni kwamba uongozi wa Simba ulimsamehe kwa kuzingatia umuhimu wake katika nafasi hiyo.
Santo hucheza nafasi ya kiungo wa ulinzi, lakini utapenda umakini wake uwanjani- utoaji wa pasi za uhakika hasa ndefu- na zaidi anapoamua kusaidia mashambulizi.
Kiungo hodari, mwenye kipaji, anayejituma- ndivyo unavyopaswa kumzungumzia Santo ambaye kwa sasa anaibeba klabu iliyomuinua kisoka, Tusker.
0 comments:
Post a Comment