![]() |
Oliech |
MWENYEKITI wa Shirikisho la Soka Kenya (FKF) amesikitishwa
na kitendo cha Nahodha wa Harambee Stars, Dennis Oliech kustaafu soka ya
kimataifa.
Oliech alitangaza kustaafu kupitia facebook, lakini watu
walio karibu na mchezaji huyo, wameiambia SuperSport.com na bongostaz.blogspot.com
ikatufikia kwamba mshambuliaji huyo wa Auxerre ya Ufaransa amekasirishwa na
kitendo cha Kampuni ya Bia Afrika Mashariki (EABL) kutumia picha yake kwenye
tangazo bila ridhaa yake. Nyamweya pia amejipa matumaini ya kumaliza mgogoro huo kwa kutaka pande zote zitulie suluhu ikitafutwa.
"Kama unavyofahamu, hatuwezi kuchukua hatua bila kusubiri majibu ya wanasheria, ambao wamekuwa wakijadili suala lililowasilishwa na Oliech na tumeamua kutulia juu ya hili tangu mkataba umesainiwa tukiwa hatupo ofisini," alisema Nyamweya.
"Sitaki kuzungumzia zaidi, lakini tutasubiri hadi tukipata mawasiliano rasmi na mchezaji mwenyewe, kabla ya kuamua kuchukua hatua," alisema.
Oliech amekuwa hana furaha tangu picha yake kutumika kwenye tangazo bila kuhusishwa kwa lolote, japokuwa katika mkataba wa udhamini, Bodi ya Utawala ya Harambee Stars, imeipa EABL haki zote za kutumia picha za timu ya taifa katika promosheni zao.
“Ni siku ya machungu kwa soka ya Kenya,” aliandika kwenye ukurasa wake wa facebook mshambuliaji huyo wa zamani wa Nantes.
“Kwa moyo mzito, natangaza kustaafu kwangu timu ya taifa mara moja. Ingawa nahisi sijatimiza malengo yangu katika kiwango hiki kwangu binafsi na kwa timu, imekuwa heshima ya juu kuvaa jezi ya timu ya taifa na kuiwakilisha nchi yangu. Pamoja na hayo, naitaikumbuka heshima hiyo.”
“Ningependa kuwashukuru wachezaji wenzangu na viongozi kwa sapoti waliyonipa miaka iliyopita. Siwezi kusahau hasa sapoti niliyokuwa ninapewa na mashabiki kwangu na kwa timu.
Nawashukuru kwa mchango wao na ninaungana nao kuwa nyuma ya timu na kuiombea dua Harambee Stars katika changamoto zilizo mbele yao,”alisema.
Tangu aanze kuichezea Stars akiwa kinda mwaka 2002, Oliech amekuwa tegemeo la safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.
Alifunga bao la ushindi lililoipa Kenya taji la michuano ya CECAFA Challenge akiwa ana umri wa miaka 19 mwaka 2002, Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, Harambee ikiwafunga wenyeji Tanzania Bara 3-2.
Alifunga pia bao la ushindi, Stars ikiifunga Cape Verde 1-0 na kukata tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2004 nchini Tunisia. Oliech alipewa Unahodha wa timu mwaka 2010.
Hatua hii inakuja kiasi cha miezi kama miwili tangu MacDonald Mariga naye aisuse timu ya taifa kwa kutolipiwa gharama zake za kujiunga na timu kwa ajili ya mechi ya kuwania kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani, dhidi ya Togo.
Mapema mwaka huu, kipa Arnold Origi alitangazaa kustaafu kuchezea timu hiyo kabla ya kurejea baada ya mazungumzo na kocha Francis Kimanzi na anatarajiwa kuichezea tena Stars Juni.
0 comments:
Post a Comment