• HABARI MPYA

    Tuesday, July 10, 2012

    TFF YAPATA MSIBA MWINGINE


    Na Prince Akbar
    SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mara (FAM), Fabian Samo kilichotokea leo asubuhi (Julai 10 mwaka huu).
    Ofisa Habari wa TFF, Boniphace Wambura Mgoyo, ameaimbia BIN ZUBEIRY leo mchana kwamba, Samo ambaye Novemba 13 mwaka jana alichaguliwa kwa kipindi cha pili mfululizo kuwa Mwenyekiti wa FAM katika uchaguzi uliofanyika wilayani Rorya alikuwa amelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dar es Salaam akisumbuliwa na maradhi ya figo.
    Wambura amesema taratibu za mazishi ya Samo ambaye alikuwa mjumbe wa Kamati ya Ukaguzi wa Hesabu (Internal Audit Committee) ya TFF ikiwemo siku atakayozikwa bado zinafanywa na familia yake.
    Amesema Samo alitoa mchango mkubwa katika maendeleo ya soka mkoani Mara na Tanzania kwa ujumla, vitu ambavyo vilichangia kuchaguliwa kwake tena kuiongoza FAM.
    Amesema msiba huo ni pigo kwa familia ya Samo, FAM, TFF na mchezo wa mpira wa miguu kwa ujumla nchini kutokana na mchango na mawazo aliyotoa kwa kipindi chote alichokuwa kiongozi.
    Amesema TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Samo, FAM, jamaa na marafiki na kuwataka kuwa na uvumilivu katika kipindi hiki cha msiba huo mzito. Pia TFF itatoa ubani wa sh. 200,000 kwa familia ya marehemu kama rambirambi zake.
    Mungu aiweke roho ya marehemu Samo mahali pema peponi. Amina
    Wakati huo huo: Wambura amesema kwamba, wakati wa mechi za Kombe la Kagame Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia Julai 14-28 mwaka huu, screen kubwa iliyoko uwanjani itatumika kwa matangazo ya biashara na ujumbe mbalimbali kwa washabiki watakaoshuhudia mechi hizo.
    Amesema TFF inakaribisha kampuni na wadau mbalimbali wanaotaka kuweka matangazo yao wakati wa michuano hiyo itakayoshirikisha klabu kumi na moja kutoka ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.
    Amesema muda wa kurushwa matangazo hayo yanayotakiwa kuwa kwenye mfumo wa DVD ni kabla ya mechi kuanza, wakati wa mapumziko na baada ya mechi. Matangazo hayo yanatakiwa kuwa ya sekunde 60 (dakika moja) au sekunde 30 (nusu dakika).
    Aidha, Wambura amesema kwamba Kozi ya makocha wa mpango wa grassroots unaolenga wachezaji mpira wa miguu (wasichana na wavulana) wenye umri kuanzia miaka 6-12 imeanza leo (Julai 10 mwaka huu) kwenye ukumbi wa Msimbazi Center, Dar es Salaam.
    Amesema Wakufunzi kutoka Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) ndiyo wanaoendesha kozi hiyo iliyofunguliwa na Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah.
    Amesema Kozi hiyo itakayomalizika Julai 15 mwaka huu inashirikisha washiriki 35, na mwendelezo wa ile ya awali iliyofanyika Desemba 14-17 mwaka jana jijini Dar es Salaam.
    Amemtaja Gouinden Thandoo kutoka Mauritius ni mmoja wa wakufunzi wa FIFA wanaoendesha kozi hiyo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TFF YAPATA MSIBA MWINGINE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top