• HABARI MPYA

    Thursday, August 16, 2012

    MATOLA ASEMA MTIBWA SUGAR WATAANGUKIA PUA KAMA AZAM

    Suleiman Matola

    Na Mahmoud Zubeiry
    KOCHA wa timu ya vijana ya Simba SC, Suleiman Abdallah Matola amesema kwamba hawahofii kabisa Mtibwa Sugar kuelekea fainali ya michuano ya Bank ABC Sup8R na anaamini atabeba Kombe mbele yao keshokutwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana baada ya mechi Uwanja wa Taifa, Matola ambaye ni Nahodha wa zamani wa Simba SC, alisema kwamba Mtibwa ni timu nzuri aliiona vizuri wakati ikiifunga 5-1 Jamhuri ya Pemba, lakini bado kwa Simba B wataangukia pua.
    “Itakuwa mechi ngumu hilo naamini kabisa, lakini nataka nikuambie, kama nilivyosema kabla ya kucheza na Azam, nasema tena kabla ya kucheza na Mtibwa Sugar, tutawafunga bila kuongezewa nguvu ya wachezaji wa timu A,”alisema Matola.
    Simba jana ilitinga Fainali ya michuano ya BankABC Sup8R baada ya kuifunga Azam FC, mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Jumamosi itamenyana na Mtibwa Sugar, ambayo katika mechi ya kwanza imeifunga Jamhuri ya Pemba mabao 5-1, uwanja huo huo.
    Katika mchezo huo, hadi mapumziko, Simba B walikuwa mbele kwa bao 1-0, lililotiwa kimiani na Rashid Ismail aliyeunganisha krosi ya Edward Christopher dakika ya pili tu ya mchezo huo.
    Kipindi cha pili ‘Watoto wa Matola’ walirudi na moto na kulisakama kama nyuki lango la Azam, wakigongeana pasi za uhakika ndefu na fupi na kuwafunika kabisa mabingwa wa Kombe la Mapinduzi.
    Christopher Edward aliifungia Simba bao la pili kwa penalti dakika ya 56, baada ya yeye mwenyewe kuangushwa ndani ya eneo la hatari na Luckson Kakolaki.
    Azam walipata bao la kufutia machozi dakika ya 71, mfungaji Zahor Pazi aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Gaudence Mwaikimba, baada ya kutokea purukushani kwenye lango la Simba B. 
    Christopher Edward amezidi kujiimarisha katika mbio za kusaka kiatu cha dhahabu kwa kutimiza mabao matano, akifuatiwa na Shaaban Kisiga ‘Malone’ mwenye mabao manne.
    Simba iliingia Nusu Fainali, baada ya kuongoza Kundi A, kwa pointi zake saba, baada ya kutoa sare moja na kushinda mechi mbili, wakati Mtibwa inayofundishwa na Nahodha pia na Nahodha wake wa zamani, Mecky Mexime, iliongoza Kundi B kwa pointi zake tisa baada ya kushinda mechi zote tatu.
    Kanuni za mashindano haya ni kushirikisha timu zilizoshika nafasi tatu za juu katika Ligi Kuu za Bara na visiwani na mbili zilioongoza katika kupanda Ligi Kuu zote mbili, lakini kwa Bara, Yanga waliokuwa washindi wa tatu msimu uliopita, walijitokea na nafasi yao ikachukuliwa na Mtibwa Sugar ambayo ilishika nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu.
    Bingwa wa michuano hiyo mipya itakayokuwa ikifanyika kila mwaka, ataondoka na Sh. Milioni 40, mshindi wa pili Sh. Milioni 20, wa tatu Sh. Milioni 15 sawa na wa nne, wakati washiriki wengine wataondoka na Sh. Milioni 5 kila moja.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MATOLA ASEMA MTIBWA SUGAR WATAANGUKIA PUA KAMA AZAM Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top