JULAI 14,
mwaka huu, mfanyabiashara maarufu nchini, mwenye asili ya Kiasia, Yussuf
Mehboob Manji aliingia madarakani Yanga, kufuatia uchaguzi mdogo uliofanyika
katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.
Na Mahmoud Zubeiry
|
Manji
alishinda kwa kishindo kwa pamoja na watu wanne kati ya watano aliopendekeza
aingie nao madarakani, Abdallah Ahmed Bin Kleb, George Manyama na Mussa
Katabaro, alikosekana Lameck Nyambaya tu katika timu yake, iliyobatizwa jina
Jeshi la Miamvuli ambaye badala yake aliingia Aaron Nyanda.
Watu hawa
watano hakika walibeba na bado wamebeba matumaini makubwa ya wana Yanga juu ya
taswira mpya ya klabu, kulingana na sera zao wakati wa kampeni- na kwa sababu
wote wanaonekana watu wenye uelewa mkubwa, wenye uwezo wa kifedha na kwa ujumla
wenye dhamira fulani ya kuifanyia kitu klabu.
Wiki hii,
hawa jamaa wametimiza miezi miwili ya kuwa madarakani na katika kipindi hicho
si vibaya kuwapongeza kwa kazi nzuri ya awali waliyofanya ikiwemo kusajili
wachezaji wa gharama, kocha wa gharama na kuboresha baadhi ya mambo ndani ya
klabu, ikiwemo maslahi ya wachezaji.
Jeshi la Miamvuli...Hapa Manni anampigia debe Bin Kleb. Wengine kulia ni Manyama na Nyambaya. Kushoto ni Sanga. |
Lakini kubwa
ni kuiwezesha klabu kutwaa kombe la tano la Klabu Bingwa ya soka Afrika
Mashariki na Kati, Kombe la Kagame- kitu ambacho kwa hakika kimewafariji
wapenzi wa klabu hiyo kwa kuukosa ubingwa wa Bara msimu uliopita na kufungwa
5-0 na wapinzani wao wa jadi, Simba SC.
Lakini bado
pamoja na hayo, kulingana na hali halisi ya klabu hiyo kwa sasa, yapo mambo
ambayo hakika yalitarajiwa kupewa kipaumbele na mabwana wakubwa hawa baada ya
kuingia madarakani.
Natambua
hata Rome haikujengwa siku moja, hivyo sitaki kuamini kwa sababu lipo ‘Jeshi la
Miamvuli’ Yanga, basi ndani ya siku mbili Yanga itakuwa na hadhi sawa na Tout Puissant
Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC)- la hasha, jamaa wanahitaji
muda.
Pamoja na
ukweli huo, lakini yapo baadhi ya mambo madogo madogo yalistahili kupewa
kipaumbele, kama ukarabati wa vyumba vya jengo la klabu, kuweka fenicha mpya
zenye hadhi.
Mambo
mengine kama uboreshaji wa gym, iwe gym kweli ya kimichezo, ukarabati wa jengo na
Uwanja kwa ujumla, kweli hayo yanahitaji muda na hata baada ya miaka miwili
watu wanaweza kufanya subira.
Lakini kutoa
zile fenicha zinzofanana na za gesti za Uwanja wa Fisi na kuweka fenicha za
kisasa, kutengeneza mabomba yaweze kupandisha maji hadi vyumbani, makabati ya
kuhifadhia nguo, Televisheni vyumbani- haya kwa kweli kwa hadhi ya Jeshi la
Miamvuli hayahitaji muda.
Sera kubwa
ya Jeshi la Miamvuli ni kubana matumizi, na ukarabati wa vyumba vya wachezaji
ni njia mojawapo ya kubana matumizi, ili timu iwe inaweka kambi klabuni na
kuepuka gharama za mamilioni ya kulipia hoteli.
Lazima Manji
na jeshi lake wajitofautishe na aina ya viongozi wengine wababaishaji waliowahi
kutokea Yanga kwa kuhakikisha wanafanya mambo ambayo yatabadilisha taswira ya
klabu.
Juzi, Kocha
Mkuu wa Yanga SC, Mbelgiji Tom Saintefiet alilalamikia kulala kwenye hoteli
mbaya, mjini Mbeya yenye vitanda vichache na vidogo, vilivyosababisha watu
wakalala mzungu wa nne, na chakula kibaya wakati wa mechi yao ya kwanza ya Ligi
Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, dhidi ya wenyeji Prisons, ambayo iliisha kwa sare
ya bila kufungana.
Alisema yeye
alilala kitanda kimoja na Louis Sendeu na Mbuyu Twite alibanana na Didier
Kavumbangu na hoteli haikuwa na mabomba vyooni wala bafuni, hivyo kulazimika
kuingia na ndoo na kuogea kata.
Alisema pia
hoteli hiyo ilikuwa katikati ya mji na karibu na stendi ya mabasi, kila
alfajiri kelele nyingi na kwa ujumla timu iliingia uwanjani ikiwa haiko vizuri.
“Mimi kwa
mfano sijaoga siku mbili, kwa kweli tulikuwa katika mazingira magumu na
wapinzani wetu walicheza soka ya kuudhi tangu mwanzo, kupoteza muda, na marefa
hawakuchukua hatua, tulipoteza nafasi kupitia kwa Kiiza (Hamisi) na Msuva
(Simon), siwezi kulaumu mchezaji wangu yeyote, lakini hiyo ndiyo hali
halisi,”alisema Saintfiet.
Baadhi ya
watu wanaweza kuchukulia kauli za Mtakatifu Tom kama visingizio baada ya
kushindwa kuanza na ushindi katika Ligi Kuu, huku wapinzani wake wakuu, Simba
na Azam wakibeba pointi, lakini ukweli ni kwamba tangu anafika Mbeya, Mbelgiji
huyo alikerwa na hali hiyo.
Binafsi
nilipofanya naye mahojiano baada ya kufika Mbeya alinielezea hali hiyo, nami
nilimfariji tu kwamba hiyo ni hali halisi ya nchi yetu na anapaswa kuvumilia
huku akiwaelewesha taratibu viongozi wake.
Ubingwa wa Kagame ni matunda ya Jeshi la Miamvuli |
Lakini
ukweli ni kwamba, Saintfiet alikuwa ana hoja hasa pale aliposema huwezi
kusajili mchezaji kwa dola za Kimarekani 60,000 halafu ukamlaza kwenye chumba
cha Sh. 15,000.
Lazima Yanga
iendane na hadhi ya viongozi wake- sitaki kuamini akina Seif Ahmad Magari na
Abdallah Ahmad Bin Kleb waliopkwenda kwenye mechi hiyo nao walilala katika
hoteli hiyo za kuoga na kata.
Dharau ni
neno lenye maana pana sana- na wakati mwingine hata kupuuza ni dharau na mara
nyingi dharau husababisha madhara na hii inaonekana kama kuwa desturi ya Yanga
kwa miaka ya karibuni.
Mwaka jana,
Yanga walichukua Kombe la Kagame, wakajiona wao ndio wao, wakashindwa kuiandaa
timu yao vizuri kwa ajili ya ligi, matokeo yake mwakani hawatashiriki michuano
ya Afrika.
Mwaka huu
pia wamechukua Kombe la Kagame, kweli timu ilikuwa na maandalizi ya muda mrefu
na ilikwenda kucheza mechi mbili za kujipima nguvu Rwanda- lakini bado kuna
mambo madogo madogo ambayo viongozi wanapaswa kuyatilia mkazo na kuacha
kudharau.
Katabaro peke yake akiamua anabadilisha fenicha Yanga nusu saa tu |
Naweza
kusema dharau ndiyo iliyosababisha hali iliyotokea Mbeya- na kama wataendelea
nayo, Yanga wajue kabisa haitakuwa tofauti na msimu uliopita kwa sababu ligi ya
sasa si ile ya bingwa akiwa Simba, Yanga atakuwa wa pili- hapana. Ligi ya sasa
ina Azam na washindani wengine wanaonekana kuibuka msimu huu.
Haya
nilikuwa natolea mfano tu, lakini hoja yangu ya msingi leo ni kwamba, yapo
mambo ambayo Manji na Jeshi lake la Miamvuli wanaweza kupewa muda, ila baadhi
ya mambo hakika hayahitaji muda kama kubadilisha vile vitende vya Uwanja wa
Fisi. Alamsiki!
0 comments:
Post a Comment