• HABARI MPYA

    Sunday, September 16, 2012

    MADUDU HAYA HADI LINI KWENYE SOKA YETU?

    Ofisa Mkuu wa Biashara wa Zantel, Sajid Khan akimkabidhi jezi, Mkurugenzi wa Michezo, Leonard Thadeo kwa niaba ya klabu ya African Lyon ya Dar es Salaam, katika hoteli ya Hyatt Regency (zamani Kilimanjaro), Dar es Salaam wakati wa kutangaza kuingia mkataba wa kudhamini klabu hiyo kwa miaka mitatu. Wanaomfuatia Thadeo ni Meneja Mkuu wa African Lyon, Rahim Kangezi ‘Zamunda’ na Charles Otieno, Mkurugenzi wa Ufundi wa African Lyon. Kulia kabisa ni mchezaji chipukizi wa Lyon, Jarufu Magesa, ambaye anapelekwa na klabu Marekani kusoma na Kocha Muargentina wa African Lyon, Pablo Ignacio Velez. 

    BINAFSI nawaheshimu sana kampuni ya Vodacom Tanzania kwa mchango wao mkubwa katika maendeleo ya soka ya nchi hii, kwani sijui bila ya wao kujitokeza kuichukua Ligi Kuu mwaka 2002, hali ingekuwaje.
    Na Mahmoud Zubeiry 
    Tulipotoka, soka ilikuwa haina thamani kabisa mbele ya makampuni nchini- ulichukuliwa kama mchezo wa vurugu, migogoro ambao ungeharibu hadi sifa ya kampuni, ambayo ingejitokeza kuudhamini.
    Makampuni hayakujali ni mamilioni ya watu wangapi wanavutiwa na soka ya Tanzania, hawakujali ni mamilioni ya watu wangapi wanapenda Simba na Yanga. Hawakujali kama wapo watu hufikia hadi kujiua kwa ajili ya Simba na Yanga, ambazo ndizo zinabeba msisimko wa soka ya nchi hii, waliogopa tu ni mchezo wa vurugu na migogoro, basi- na hawakuutaka.
    Waliona bora kuwekeza kwenye michezo mingine, ambayo hata kama haina wapenzi wengi, lakini tu haina vurugu wala migogoro.
    Ilichukua muda sana, tangu mwaka 1965 ilipoanzishwa Ligi Tanzania hadi mwaka 1996 alipopatikana mdhamini wa kwanza wa ligi hiyo, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Safari Lager.   
    Lakini udhamini huo ulidumu kwa takriban miaka minne tu na hali ilikuwa tete mwaka 2001, baada ya TBL kujitoa kudhamini Ligi Kuu ya Tanzania Bara ghafla. Bingwa wa mwaka 2001, Simba SC alitoka mikono mitupu, baada ya TBL waliokuwa wakiidhamini ligi hiyo kupitia bia ya Safari Lager ‘kuimwaga’.
    Kisa nini? Kapuya huyo! Aliyekuwa Waziri wa iliyokuwa Wizara ya Kazi, Maendeleo ya Vijana na Michezo, Profesa Juma Athumani Kapuya, ‘aliwaboa’ wadhamini hao kwa kujiamulia tu kuongeza timu katika Ligi Kuu, kinyume na makubaliano yao na Chama cha Soka Tanzania (FAT), sasa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
    TBL wakaona ligi haina kanuni, utaratibu wala kuheshimu vipengele vya mikataba ya udhamini, ndiyo yale yale, mchezo wa kihuni, mchezo wa vurugu na usiofaa, wakaitema. Wengi miongoni mwa wapenzi wa soka Tanzania waliingiwa hofu juu ya mustakabali wa ligi hiyo, kwani walijua itarudi kwenye enzi zile za kucheza kwa ajili ya mapato ya milangoni tu.
    Udhamini unaongeza ladha ya ligi kwa sababu timu zinawania zawadi, mbali na kombe, zinapata vifaa vya michezo kutoka wadhamini sambamba na kiasi cha fedha za gharama kama za usafiri na kadhalika, hivyo kujitoa kwa wadhamini- maana yake ligi ingekuwa chungu kwa klabu.
    Akaibuka mkombozi, kampuni iliyokuwa mpya kabisa ya huduma za simu za mikononi Tanzania, Vodacom Tanzania na kuingia mkataba wa udhamini wa ligi hiyo na FAT, kuanzia msimu wa 2002.
    Taratibu hali imekwenda ikibadilika na sasa makampuni yanajitokeza kuwekeza kwenye soka, baada ya kuuelewa vema mchezo huo, kwamba unafaa na zaidi hicho wanachoogopa wao, vurugu na migogoro ni msisimko wa kishabiki na demokrasia, mambo ambayo ni ya kawaida katika vitu vinavyogusa hisia za watu wengi. Hiyo ndiyo soka.
    Kujitokeza kwa wawekezaji kwenye soka, kumesababisha hadi vyama na klabu zianze kuondokana na woga na sasa haki zaidi inatafutwa.
    Tazama, timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ambayo haikuwahi kuwa na mdhamini tangu soka ianze kuchezwa nchi hii, kabla ya Uhuru hadi mwaka 2006, lakini mwaka huu imegombewa na kampuni mbili katika kutaka kuidhamini na mwishowe TBL waliizidi kete Kampuni ya Bia ya Serengti (SBL) iliyokuwa ikiidhamini timu hiyo. Tumetoka mbali.
    Lakini pamoja na yote, soka sasa ni mchezo ambao umewekewa misingi mizuri ya sheria na kanuni chini ya Shirikisho la Kimataifa la mchezo huo (FIFA) na ina mfumo bora wa utawala wenye mamlaka yenye kujitosheleza.
    Masuala ya soka sasa hayafiki Mahakamani, kutokana na huo mfumo bora wa kiutawala, sheria na kanuni na hilo limepitishwa na wanachama wake dunia nzima na yeyote atakayethubutu kupeleka suala la soka kwenye dola, kwanza atakuwa amejiengua kwenye familia ya kandanda, mengine yatafuata, ikiwa ni pamoja na FIFA kupambana naye kizimbani. 
    Lakini pamoja na ukweli huo, kwa Tanzania bado usimamizi wa sheria na kanuni ni tatizo jambo ambalo limesababisha sasa hakuna nidhamu kabisa katika mfumo wa utawala na uendeshwaji wa soka katika nchi hii kwa ujumla.
    Ushabiki wetu wa Simba na Yanga umepita kiwango na hatujali unaathiri vipi maendeleo ya soka ya nchi hii, ambayo mara ya kwanza na ya mwisho ilicheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 1980.
    Wizi, rushwa na kwa ujumla kuweka mbele maslahi binafsi kwa pamoja na upeo wetu mdogo na ujuaji, hawa ni maadui wakubwa wa soka yetu. Siku zote nasema, tuna safari ndefu sana kufikia matamanio, maana hatuna malengo, zaidi ya kuwamezea mate wenzetu na kutamani siku moja tuwe kama wao.
    Jana kimetokea kituko Uwanja wa Taifa, ambacho ni mwendelezo wa hayo mapungufu niliyoyaelezea hapo juu.
    Klabu ya African Lyon ilizuiwa kuweka mabango yake kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wala kuvaa jezi zenye nembo ya mdhamini wao, kampuni ya simu ya Zantel katika mchezo wa leo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Simba SC.
    Mapema jana mchana, Lyon ilitangaza kuingia mkataba wa udhamini na Zantel wa miaka mitatu na ilitarajiwa kuanza kuutumikia katika mchezo wa jana wa ufunguzi wa Ligi Kuu dhidi ya Simba.
    Meneja Mkuu wa Lyon, Rahim ‘Zamunda’ Kangezi, alisema msimamo huo wa kuzuiwa kuvaa jezi za mdhamini wao na kuweka mabango kama ungeendelea, basi wao wasingecheza mechi hiyo. Nilijuwa hawawezi kuacha kucheza na walicheza wakafungwa mabao 3-0.
    “Katika maboresho ya mkataba wa udhaimini wa Ligi Kuu wa Vodacom, hili limekwishazungumzwa na limerekebishwa kwamba klabu zitaruhusiwa kuingia mkataba na kampuni nyingine za simu.
    Pia, leo (jana) katika kikao cha kabla ya mechi tulipeleka jezi hizi na zikapitishwa, sasa iweje tunaambiwa hatuwezi kuvaa, sisi hatukubali, kama hatuvai na hatuchezi,”alisema Zamunda.
    Mapema jana mchana, Ofisa Mkuu wa Biashara wa Zantel, Sajid Khan alitangaza kampuni yake kuingia mkataba wa miaka mitatu kuidhamini Lyon, mbele ya Mkurugenzi wa Michezo, Leonard Thadeo katika hoteli ya Hyatt Regency (zamani Kilimanjaro), Dar es Salaam.
    Hadi sasa haieleweki kama mkataba mpya wa udhamini wa Ligi Kuu umesainiwa au la, maana yake pamoja na TFF kusema umesainiwa, lakini hakuna picha inayoonyesha utiwaji saini wa mkataba mpya, baada ya ule wa awali kumalizika msimu uliopita.
    Na kumekuwa na mgogoro kabla ya utiwaji saini wa mkataba huo, kubwa klabu zikitaka sasa kama ilivyo kwa nchi nyingine nyingi wanachama wa FIFA, ziendeshe zenyewe ligi na hilo lilipitishwa katika mkutano Mkuu uliopita wa shirikisho hilo, ingawa utekelezwaji wake rasmi bado.
    Klabu zinadai, wakati wa matayarisho ya mkataba mpya, waliomba baadhi ya vipengele vya mkataba huo, viboreshwe, ikiwemo kuziruhusu kampuni za simu kudhamini klabu na inaelezwa hilo lilikubaliwa na TFF.
    “Klabu zilikubaliana kwa pamoja kuwa kipengele cha exclusivity kiondolewe kweye mkataba na kiliondolewa... nakumbuka nilimuuliza swali Mjumbe wa Kamati ya Ligi, Yahya kuwa, je endapo JKT Ruvu itampata Tigo kama mdhamini, je itaruhusiwa kucheza ligi na jezi zenye nembo ya Tigo? jawabu lilikuwa ni YES... sasa kilichotokea uwanja wa Taifa leo (jana) ni kichefuchefu,”alisema Meneja wa Azam FC, Patrick Kahemele akilizungumzia sakata hilo.
    Ukichukua maelezo ya Kahemele na Zamunda, unaweza kugundua tatizo katika hili, lipo TFF. Inakuwaje makubaliano yafikiwe halafu yasitekelezwe? Hizi ni vurugu zisizo za lazima.
    Nilisema, tulipotoka mbali na tulipofikia klabu zimeanza kujiamini na zinataka haki zaidi, ndio kama hivyo wanaomba kampuni nyingine za simu ziruhusisiwe kudhamini klabu.
    Mwaka 2002, wakati Vodacom wanaingia mkataba wa kudhamini ligi hiyo kwa mara ya kwanza, Yanga ilikuwa inadhaminiwa na Mobitel (sasa Tigo) na kwa sababu hiyo, Vodacom wakaiondoa Yanga kwa Mobitel na kuipa udhamini wa kampuni ya Shivacom, waliokuwa mawakala wao.
    Hata hivyo, inaonekana ule ulikuwa mkataba wa ujanja ujanja tu wa kuifanya Yanga iachane na Mobitel na ndiyo maana haukudumu, lakini hali imebadilika sasa na watu wanahoji, kama Ligi Kuu ya England mdhamini wake ni Barclays na bado Liverpool inadhaminiwa na Standard Charter, zote benki, iweje hapa Tanzania isiwe hivyo?
    African Lyon katika mechi ya jana bila ya jezi za wadhamini wao
    Inaweza kuwa hivyo, lakini pia si lazima iwe hivyo- ni suala la makubaliano tu na maamuzi yake yazingatie maslahi ya pande zote.
    Hatuhitaji kupiga kura tu katika kuamua Kevin Yondan acheze timu gani, bali hata katika suala la udhamini, klabu zingepiga kura kuamua Vodacom iendelee kudhamini Ligi Kuu kwa kuruhusu kampuni nyingine za simu zidhamini klabu, au ijitoe.
    Sasa klabu ambazo hazina ndoto za kuwa na wadhamini na zinauhitaji udhamini wa Vodacom zingeamua sakata hilo- lakini kitendo cha klabu kukubaliwa ziingie mikataba ya udhamini na kampuni nyingine za simu, halafu zinazuiwa kuutumikia ni vurugu ambazo zinaepukika. Lakini kwa nini madudu haya katika soka yetu? Inakera!
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MADUDU HAYA HADI LINI KWENYE SOKA YETU? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top