• HABARI MPYA

    Sunday, September 16, 2012

    SIMBA SC YAMCHEZEA LIGI SUNZU

    Straika wa Simba, Mzambia Felix Sunzu.
    MWANDISHI WETU
    BINGWA wa Ligi Kuu Bara inayoanza leo Jumamosi anapata Shilingi 70 milioni ambazo ni sawa na mshahara wa mwaka mzima wa straika wa Simba, Mzambia Felix Sunzu.
    Kampuni ya Simu za Mkononi ya Vodacom imeingia mkataba wa miaka mitatu na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wa kudhamini ligi hiyo ikiwa imepanga kutumia kiasi cha Sh 1.7 bilioni.
    Mshindi wa pili wa ligi hiyo atajizolea, Sh 50 milioni wakati Sh 30 milioni zitakwenda kwa mshindi wa tatu.
    Sunzu analipwa Dola 3,500 kwa mwezi ambazo ni sawa na Sh 5.4 milioni ambazo ukizidisha kwa miezi 12 anapata Sh 65.1 milioni na ukiongeza na posho za mechi na gharama ndogondogo ambazo klabu inaingia, zinazidi Sh 70 milioni za bingwa wa ligi.
    Klabu zimekuwa zikilalamikia ufinyu wa zawadi huku TFF ikitangaza kwamba mkataba mpya na mdhamini umeshasainiwa ingawa hakuna picha zozote za ushahidi zilizoonyesha wahusika wakianguka wino.
    Ligi Kuu inashirikisha timu 14 ambazo zitacheza mechi 26 kuzunguka mikoa mbalimbali kila timu ikiwa na usajili wa wachezaji wasiopungua 25.
    Huku udhamini wa Tanzania ukiwa kiduchu huko Afrika Kusini ambako kampuni za huko zimewekeza Tanzania katika sekta za madini, fedha na mawasiliano zinatoa zawadi za kufa mtu.
    Mathalan bingwa wa Ligi Kuu Afrika Kusini inayodhaminiwa na Benki ya ABSA, ambayo ina hisa kubwa katika Benki ya Biashara ya Tanzania (NBC), bingwa anaondoka na kiasi cha Sh 1.9 bilioni.
    Mshindi wa pili wa ligi hiyo anaondoka na kiasi cha Sh 926 milioni huku mshindi wa tatu akiweka kibindoni Sh 370 milioni.
    Kinachoshangaza ni kuwa kampuni za kigeni zilizowekeza nchini zinamwaga mamilioni huko makwao lakini linapokuja suala la kudhamini michezo ya Tanzania, zinatoa zawadi ndogo wakati wanafaidi rasilimali mbalimbali kupitia uwekezaji wao. GAZETI LA MWANASPOTI
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC YAMCHEZEA LIGI SUNZU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top