![]() |
| Na Bin Zubeiry |
BUSARA ni uamuzi wa kuzingatia maslahi ya wengi, wenye lengo la kuweka hali shwari. Busara hutumika wakati mwingine bila hata kuzingatia sheria, ili mradi tu kuhakikisha mambo yanakuwa sawa.
Naam, Mh. Alhaj Ismail Aden Rage (Mbunge wa Tabora Mjini, CCM) wakati anapambana na maradhi ya mgongo India, anakabiliwa pia na jukumu la kutumia busara ili kuinusuru klabu yake aipendayo, Simba SC.
Huyu ni Mwenyekiti wa Simba SC, ambayo kwa sasa ipo katika mgogoro. Huwezi kuuita mgogoro mkubwa, lakini unaweza kuwa mkubwa wakati wowote, iwapo hatua za kuuzima hazitachukuliwa mapema.
Viongozi wawili wa Kamati ya Utendaji, Makamu Mwenyekiti, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Zacharia Hans Poppe wamejiuzulu wiki hii.
Wote wamejiuzulu kwa sababu ya kuukwepa mgawanyiko uliopo ndani ya uongozi, ambao umekuwa chanzo cha timu kwenda mrama kwa sasa.
Simba SC kwa sasa haifanyi vizuri katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na tayari imekwishatolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kufungwa jumla ya mabao 5-0 na Recreativo de Libolo ya Angola katika raundi ya kwanza tu.
Ubingwa wa Ligi Kuu ni kama umekwishaota mbawa, kwani hadi sasa Wekundu hao wa Msimbazi wanashika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 31, sawa na Coastal Union ya Tanga na Mtibwa Sugar ya Morogoro, nyuma ya Azam FC yenye pointi 37 na Yanga inayoongoza kwa pointi zake 45, zote za Dar es Salaam.
Mambo mengi yanapigiwa kelele kwa sasa ukiachilia mbali timu kufanya vibaya, lakini usajili mbovu, matumizi mabaya ya fedha, ubadhirifu na ahadi ambazo hazijatekelezeka, ikiwemo ya ujenzi wa Uwanja wa kisasa.
Na yamekuwa mambo ambayo kwa hakika hayana majibu, zaidi zimekuwa zikitumika siasa kutuliza jazba za wanachama pale wanapokuja juu.
Kwa kweli, kwa hali ilivyo ndani ya Simba SC hivi sasa, uongozi umeshindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo na kwa sababu wanachama wamekosa subira, japo kuwapa muda wajitazame upya na kurekebisha makosa yao katika kipindi kilichobaki, ipo haja ya busara kutumika.
Katiba inamlinda Rage kuendelea kuwa madarakani hadi amalize muda wake wa uongozi na akisimamia kwenye Katiba, wanaweza kumuondoa kinyume cha utaratibu tu, kitu ambacho hakitakubaliwa na TFF (Shirikisho la Soka Tanzania).
Katikati ya wiki hii wakati Rage yupo wadini India, Simba wameunda Kamati Maalum ya kusimamia timu katika kipindi hiki ambacho uongozi wa klabu hiyo unaonekana kukutwa na mgawanyiko mkubwa, ambayo itakuwa chini ya Mwenyekiti Rahma Al Kharoos, maarufu kama Malkia wa Nyuki.
Katika kikao kilichofanyika juzi mjini Dar es Salaam baina ya Uongozi, Baraza la Wazee pamoja na Baraza la Wadhamini, pande hizo zilikubaliana kuunda Kamati hiyo isimamie timu katika wakati huu mgumu.
Katika kamati hiyo, mbali na Malkia wa Nyuki kupewa Uenyekiti, Makamu Mwenyekiti aliteuliwa Geoffrey Nyange ‘Kaburu’, Katibu Joseph Itang’are ‘Kinesi’ na Wajumbe Zacharia Hans Poppe, Swedi Nkwabi na Musley Ruwey wakati wengine wawili wataongezwa baadaye. Hata hivyo, baada ya Hans Poppe na Kaburu kujiuzulu, wameondolewa kwenye Kamati hiyo na sasa Kinesi ndiye Makamu Mwenyekiti.
Wiki mbili zilizopita, Rage aliahidi kuitisha Mkutano Mkuu wakati wowote kujadili hali ya mambo ndani ya klabu, lakini kutokana na shinikizo liliopo sasa, ipo haja kwake kufikiria mara mbili kama anahitaji kuandaa Mkutano au kuchukua hatua zitakazorejesha amani ndani ya klabu kwa haraka?
Achukue hatua akizingatia hali ya afya yake pia kwa sasa, haihitaji purukushani. Anahitaji utulivu wa nafsi na mwili kuzingatia afya yake.
Lakini kikubwa, hamkani si shwari Simba SC na watu wanaonekana kuchoka, tena kuanzia ndani ya Kamati yake Utendaji. Kaburu ni mtu mmoja mvumilivu sana, lakini naye safari hii ameshindwa.
Kinachoonekana hapa, wanachama wa Simba wamepoteza imani na uongozi wao na wanachokihitaji ni mabadiliko tu. Nani anaweza kuwatuliza ikiwa hata timu haina matokeo mazuri?
Inawezekana yanayotokea Simba SC si matarajio ya Rage pia, lakini wakati mwingine mipango hugoma na Mwenyekiti huyo anatakiwa kukubaliana na hali halisi.
Atalaumiwa hakujenga Uwanja, lakini bado kuna mambo mengine atajivunia kwa kipindi chake cha kuwa Mwenyekiti wa Simba, ikiwemo kuifunga Yanga 5-0.
Lakini kwa sasa, Rage atumie busara tu kwa kujiuzulu Uenyekiti wa Simba SC, kupisha hatua nyingine za kurejesha hali shwari ndani ya klabu hiyo.
Nimalizie kwa kumpa pole mzee wetu huyo na kumtakia ahueni ‘inshaallah’, Mwenye Mungu amjaalie apone na kurejea nyumbani salama, kuendelea na majukumu mengine, ikiwemo kuwatumikia wanananchi wa Tabora, lakini kwa Simba SC, Rage sasa ang’atuke.



.png)