![]() |
| Malkia wa Nyuki katika picha kubwa, Hans Poppe juu kulia, Rage chini yake na Kaburu kushoto. |
Na Mahmoud Zubeiry
KLABU ya Simba imeunda Kamati Maalum ya kusimamia timu katika kipindi hiki ambacho uongozi wa klabu hiyo unaonekana kukutwa na mgawanyiko mkubwa, ambayo itakuwa chini ya Mwenyekiti Rahma Al Kharoos, maarufu kama Malkia wa Nyuki.
Katika kikao kilichofanyika juzi mjini Dar es Salaam baina ya Uongozi, Baraza la Wazee pamoja na Baraza la Wadhamini, pande zilikubaliana kuunda Kamati hiyo isimamie timu katika wakati huu mgumu.
Katika kamati hiyo, mbali na Malkia wa Nyuki kupewa Uenyekiti, Makamu Mwenyekiti aliteuliwa Geoffrey Nyange ‘Kaburu’, Katibu Joseph Itang’are ‘Kinesi’ na Wajumbe Zacharia Hans Poppe, Swedi Nkwabi na Musley Ruwey wakati wengine wawili wataongezwa baadaye.
Hata hivyo, siku moja baada ya kuundwa kwa Kamati hiyo na hata kabla haijatangazwa, Wajumbe wawili walioteuliwa walitangaza kujiuzulu nyadhifa zao za Kamati ya Utendaji ya Simba SC.
Hao ni Kaburu aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa klabu na Zacharia Hans Poppe aliyekuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, ambao waliwasilisha barua zao jana.
Bado haijafahamika kama wawili hawa watakubali wito wa kushiriki kwenye Kamati hiyo maalum ya kuinusuru timu kwa sasa ikiwa katika hali mbaya au la.
Simba SC kwa sasa haifanyi vizuri katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na tayari imekwishatolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kufungwa jumla ya mabao 5-0 na Recreativo de Libolo ya Angola katika raundi ya kwanza tu.
Ubingwa wa Ligi Kuu ni kama umekwishaota mbawa, kwani hadi sasa Wekundu hao wa Msimbazi wanashika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 31, sawa na Coastal Union ya Tanga na Mtibwa Sugar ya Morogoro, nyuma ya Azam FC yenye pointi 36 na Yanga inayoongoza kwa pointi zake 42, zote za Dar es Salaam.
Wakati Kaburu na Hans Poppe wanajiuzulu, Mwenyekiti wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage yuko India kwa matibabu ya mgongo. Rage anasumbuliwa na maradhi ya mgongo na sasa ni takriban mara ya tatu anakwenda nchini humo kwa tiba tangu mwishoni mwa mwaka jana.
Habari zaidi zinasema, hata Rage yuko tayari kujiuzulu ili uitishwe uchaguzi mpya, lakini alipanga kufanya hivyo katika Mkutano Mkuu ambao alipanga kuuitisha wakati wowote tangu wiki iliyopita.
Wakati hayo yanaendelea, kikosi cha Simba SC kiliingia kambini jana katika hoteli ya Sapphire Court, Kariakoo, Dar es Salaam kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Jumapili dhidi ya Coastal Union ya Tanga.
Mchezo huo utakaofanika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, unatarajiwa kuwa na upinzani mkali kwani timu zote hazipishani sana viwango kwa sasa na ndio washindani wakuu wa nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu.



.png)