![]() |
Mafisango katika picha iliyoambatanishwa na gari yake aliyopata nayo ajali |
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha mchezaji wa Simba na timu ya Taifa ya Rwanda (Amavubi), Patrick Mafisango kilichotokea leo alfajiri (Mei 17 mwaka huu) kwa ajali ya gari Dar es Salaam.
Ofisa Habari wa TFF, Bonipahce Wambura Mgoyo ameiambia BIN ZUBEIRY mchana huu kwamba, msiba huo ni mkubwa kwa familia ya mpira wa miguu kwani Mafisango kwa kipindi chote alichocheza mpira hapa nchini akiwa na timu za Azam na baadaye Simba, aliifanya kazi yake (kucheza mpira) kwa bidii.
Wambura amesema kifo chake ni pigo kubwa si tu kwa familia yake na timu alizochezea, bali ukanda mzima wa Afrika Mashariki na Kati ambapo changamoto zake zilikuwa dhahiri uwanjani.
Amesema wakati mauti inamkuta, Mafisango alikuwa ameitwa Amavubi kwa ajili ya mechi za mchujo za Kombe la Dunia, Kanda ya Afrika zinazochezwa mapema mwezi ujao.
Amesema TFF inatoa pole kwa familia ya Mafisango, klabu ya Simba, Shirikisho la Mpira wa Miguu Rwanda (FERWAFA) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
0 comments:
Post a Comment