• HABARI MPYA

    Thursday, July 12, 2012

    CECAFA YATAJA VIINGILIO KAGAME


    Mashabiki wa Yanga

    Na Princess Asia
    KIINGILIO cha chini katika mashindano ya Kombe la Kagame yanayoanza Jumamosi (Julai 14 mwaka huu) vitakuwa sh. 5,000 kwa mechi za Yanga na Simba, na sh. 2,000 kwa mechi ambazo hazihusishi timu hizo. Yanga ni bingwa mtetezi wakati Simba ni makamu bingwa mtetezi.
    Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniphace Wambura Mgoyo ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, mechi zinazohusisha Yanga na Simba viingilio vitakuwa ni viti vya bluu na kijani sh. 5,000, viti vya rangi ya chungwa sh. 7,000, viti vya VIP C sh. 10,000, viti vya VIP B sh. 15,000 na viti vya VIP A ni sh. 20,000.
    Wambura amesema kwamba, siku ambazo Simba na Yanga hazichezi, viingilio vitakuwa sh. 2,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, bluu na kijani, sh. 5,000 kwa viti vya VIP C, sh. 10,000 kwa viti vya VIP B na sh. 15,000 kwa viti vya VIP A. Mshabiki akikata tiketi moja anaona mechi zote mbili; mechi ya saa 8 na ile ya saa 10.
    Amesema timu za El Salam Wau ya Sudan Kusini na Atletico ya Burundi zimewasili Dar es Salaam jana usiku (Julai 11 mwaka huu) tayari kwa mashindano hayo wakati nyingine zote zilizobaki kutoka nje zinawasili leo katika muda tofauti.
    CECAFA leo imetangaza marekebisho madogo ya ratiba ya michuano hiyo na mechi ya Simba na URA ya Uganda iliyokuwa ichezwe Jumatatu (Julai 16 mwaka huu) sasa itafanyika Jumapili (Julai 15 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    CECAFA imefanya mabadiliko hayo kutokana na fainali ya Copa Coca-Cola 2012 iliyokuwa ichezwe kwenye uwanja huo kuhamishiwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.
    Kutokana na mabadiliko hayo, mbali ya mechi ya Simba na URA itakayoanza saa 10 kamili jioni, mechi nyingine Jumapili itakuwa kati ya Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) dhidi ya Ports ya Djibouti itachezwa saa 8 kamili mchana Uwanja wa Chamazi.
    Pia siku hiyo hiyo ya Jumapili kwenye Uwanja wa Chamazi kutakuwa na mechi nyingine itakayoanza saa 10 kamili jioni. Mechi hiyo itazikutanisha timu za Azam ya Tanzania Bara na Mafunzo kutoka Zanzibar.
    Mechi za ufunguzi wa mashindano hayo Jumamosi (Julai 14 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam zitabaki kama zilivyopangwa awali. Mechi ya kwanza saa 8 mchana itakuwa kati ya APR ya Rwanda na El Salam Wau ya Sudan Kusini wakati saa 10 kamili jioni Yanga itaoneshana kazi na Atletico ya Burundi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: CECAFA YATAJA VIINGILIO KAGAME Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top