TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars jana ilichapwa bao 1-0 na Niger pungufu katika mchezo wa Kundi E kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2026 Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Bao pekee la Niger lilliloizamisha Taifa Stars limefungwa na mshambuliaji wa Aktobe FC ya Kazakhstan,Daniel Sosah mzaliwa wa Ghana dakika ya 58 akimalizia kazi nzuri ya beki wa kushoto wa Zira FC ya Azerbaijan.
Haukuwa ushindi mwepesi kwa Niger, kwani walilazimika kucheza pungufu tangu dakika ya 79 baada ya kiungo wake, Boureima Abdoulaye Katakore Amadou anayechezea klabu ya AS Niameyys kwao kutolewa kwa kadi nyekundu kufuatia kuonyeshwa kadi ya pili ya njano.
Kwa matokeo hayo, Niger inafikisha pointi tisa katika mchezo wa sita na kusogea nafasi ya tatu ikizidiwa pointi moja na Tanzania ambayo pia imecheza mechi moja zaidi.

Tayari Morocco imekwishafuzu Fainali za Kombe la Dunia 2026 zinazoandaliwa kwa pamoja na nchi za Canada, Mexico na Marekani baada ya kujihakikishia uongozi wa Kundi E.
Tanzania itakuwa mwenyeji wa Zambia mwezi Oktoba katika mechi yake ya mwisho ya kufuzu ikihitaji lazima ushindi kujaribu kuipiku Niger katika vita ya nafasi ya pili Kundi E.
Niger mechi za mbili za mwisho itacheza na Kongo nyumbani, kabla ya kusafiri kuifuata Zambia.
Tanzania, Niger na Zambia yenye pointi sita za mechi sita pia zinawania kumaliza nafasi ya pili ili ziende kwenye mchujo wa kuwania nafasi ya ziada ya kufuzu michuano hiyo, wakati Kongo inacheza kukamilisha ratiba.
Timu tisa zitakazoongoza makundi zitafuzu moja kwa moja kuiwakilisha kwenye Fainali za Kombe la Dunia, wakati washindi wa pili bora wanne wa makundi watamenyana katika Nusu Fainali na Fainali na mshindi atakwenda kushiriki mchujo wa Mabara kuwania nafasi ya kwenda Kombe la Dunia pia.
Mchujo wa Mabara, unaojulikana kama Inter-Confederation Play-Offs ni michuano mingine midogo inayoshirikisha timu sita za Mabara manne duniani, kasoro UEFA kutafuta timu mbili za mwisho za kushiriki michuano hiyo.
Kutokana na Eritrea kujitoa katika Kundi E kabla ya kucheza mechi hata moja — FIFA imesema timu za makundi mengine nane zitakazomaliza nafasi ya pili zitapokonywa pointi zilizovuna kwenye dhidi ya timu zilizoshika mkia ili kujenga uwiano sawa katika kufuzu kwenye mchujo.
0 comments:
Post a Comment