Na Mahmoud Zubeiry
WAKATI michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati,
maarufu kama Kombe la Kagame inatarajiwa kuanza Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam, mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo, Simba SC wamepania kutwaa
taji la saba.
Simba wanataka taji la saba na kwa sababu hiyo wako kwenye
maandalizi ya uhakika ili michuano hiyo ikianza wawe imara waweze kutimiza
ndoto zao, ambazo mwaka jana zilishindikana.
Mwaka jana, michuano hiyo ikifanyika Dar es Salaam, Simba
ilimkosakosa kidogo tu mwali wa Kagame, baada ya kufungwa 1-0 katika fainali na
watani wao wa jadi, Yanga katika fainali, ambayo huwezi kukosea kusema walitawala
mchezo, lakini kama ilivyo ada ya soka, bahati haikuwa yao.
Simba SC imeweka kambi Zanzibar ambako pia wanashiriki
michuano ya kukipima kikosi chake, Kombe la Urafiki.
Chini ya kocha wake Mserbia, Profesa Milovan Cirkovick,
Simba SC imeimarisha kikosi chake kwa kusajili nyota wapya kadhaa, wakiwemo
nyota kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Patrick Kanu Mbivayanga
anayecheza nafasi ya kiungo na beki wa kati Lino Masombo.
Simba pia imemsajili kiungo bora Afrika Mashariki na Kati,
Mussa Mudde ambaye pia anaweza kucheza kama beki wa kati, wakati imesajili
wazawa kama Juma Jebba kutoka Azam FC, Abdallah Juma kutoka Ruvu Shooting,
Kiggi Makassy kutoka Yanga, Salim Kinje aliyekuwa anacheza Kenya sambamba na
kuwarudisha kikosini wachezaji wake iliyowatoa kwa mkopo msimu uliopita Haruna
Shamte na Amri Kiemba.
Kuchanganya na nyota wake wa msimu uliopita kama kipa bora
Afrika Mashariki na Kati, Juma Kaseja, mwanamichezo Bora Tanzania, Shomary
Kapombe, viungo wenye vipaji vya hali ya juu Mwinyi Kazimoto, Haruna Moshi,
Uhuru Suleiman na washambuliaji tishio Felix Mumba Sunzu kutoka Zambia na
Emmanuel Okwi kutoka Uganda, Wekundu wa Msimbazi wana uwezo wa kutimiza ndoto
zao.
SIRI YA JEURI YA SIMBA SC:
Simba SC inajivunia udhamini wa Kampuni ya Bia Tanzania
(TBL), kupitia bia yake, Kilimanjaro Premeum Lager, ambao ni wa kwanza tangu
wapoteze udhamini wa Mohamed Enterprises Limited.
Ikumbukwe, Kilimanjaro Premium Lager ilianza kuidhamini Simba
Agosti 18, mwaka 2008, katika mkataba uliosainiwa kwenye hoteli ya Movenpick
(sasa Serena), mjini Dar es Salaam.
Kilimanjaro Premium Lager, ambao ni wadhamini wakuu wa
wapinzani wa jadi wa Simba, Yanga SC, imekuwa ikihakikisha udhamini wake
unafika maeneo yote muhimu katika shughuli za uendeshwaji wa klabu.
Na inaaminika udhamini huo ndiyo chachu ya mafanikio ya
miaka ya karibuni ya klabu hiyo, ikiwemo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara mbili
katika kipindi cha miaka mitano (2010 na 2012) sambamba na kufika Fainali ya
Klabu Bingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame mwaka jana.
Hadi sasa kwenye kabati la mataji la Simba SC, pale makao
makuu ya klabu yao, kuna mataji sita ya Kombe la Kagame, ikiwa ni idadi kubwa zaidi kuliko klabu nyingine
yoyote kwenye historia ya michuano hiyo, je ilitwaa vipi mataji hayo?
MWAKA 1974:
Hizi zilikuwa fainali za kwanza rasmi za michuano hiyo na
zilichezwa kwa mtindo wa ligi mjini Dar es Salaam.
Simba iliipiku timu tishio enzi hizo Afrika Mashariki na
Kati, Abaluhya FC ya Kenya, sasa AFC Leopards kwa kumaliza na pointi tano dhidi
ya tatu za vigogo hao wa soka ya Kenya.
Ilikusanyaje pointi hizo? Ilianza kwa kuifunga 1-0 Abaluhya
kabla ya kuifunga 1-0 Navy FC ya Zanzibar, kabla ya kuifunga 1-0 Abaluhya na
kumaliza kwa sare ya bila kufungana na Simba FC ya Uganda.
Kikosi cha Simba wakati huo, kilikuwa kinaundwa na wakali
kama Athumani Mambosasa (sasa marehemu), Shaaban Baraza, Mohamed Kajole
‘Machela’ (sasa marehemu), Aloo Mwitu/Mohamed Bakari ‘Tall’, Omar Choggo (sasa
marehemu), Athumani Juma Kalomba (sasa marehemu), Khalid Abeid, Martine Kikwa,
Willy Mwaijibe, Haidari Abeid ‘Muchacho’, Adam Sabu (sasa marehemu), Abdallah
Kibadeni, Saad Ally na Abbas Dilunga.
Ni wakali hawa hawa ambao pia waliifikisha Simba SC Nusu
Fainali ya Klabu Bingwa Afrika, mwaka 1974 na kutolewa na Mehallal El Kubra ya
Misri, wakitoka kuitoa timu ngumu na tishio barani enzi hizo, Hearts Of Oak ya
Ghana.
MWAKA 1991
Simba ilishindwa kutetea taji hilo mwaka 1975 baada ya
kufungwa na wapinzani wao wa jadi, Yanga katika fainali visiwani Zanzibar na
wakalazimika kusubiri hadi mwaka 1991 ili kupata taji la pili la michuano hiyo
katika fainali nyingine zilizofanyika Dar es Salaam.
Walibebaje taji? Simba ilianzia Kundi A mjini Dar es Salaam ambako
waliongoza na kufanikiwa kuingia Nusu Fainali, ambako walikutana na Gor Mahia
ya Kenya na kushinda 1-0, hivyo kutinga fainali.
Katika fainali, Wekundu wa Msimbazi walikutana na SC Villa
ya Uganda, iliyokuwa tishio ikiongozwa na mshambuliaji bora zaidi kuwahi
kutokea Uganda, Majjid Musisi Mukiibi na kushinda mabao 3-0, Zamoyoni Mogella ‘Golden
Boy’ na Kocha Mchezaji Hassan Afif waking’ara mno na kuwa chachu ya ushindi.
Siku hiyo, Jamhuri Mussa Kihwelo ‘Julio’ alikuwa ana kazi moja
tu- kumdhibiti Musisi (sasa marehemu), asilete madhara na akafanikiwa. Ilikuwa
hadi Musisi anakunywa maji, Julio anamsubiri arudi uwanjani aanze kutembea naye
tena.
Kikosi cha Simba kilichotwaa taji hilo, kilikuwa kinaundwa
na wakali kama Iddi Pazi ‘Father’, Mavumbi Omar, Raphael Paul (sasa marehemu),
Twaha Hamidu ‘Noriega’, Jamhuri Kihwelo, Method Mogella (sasa marehemu), Iddi
Suleiman ‘Meya, Issa Kihange, Bakari Iddi, Ayoub Mzee/Hassan Afif, Zamoyoni
Mogella, Itutu Kiggi ‘Road Master’/Khalfan Ngassa, Hamisi Thobias Gaga ‘Gaga
Rhino’, Frank Kasanga ‘Bwalya’ na Gebo
Peter.
MWAKA 1992:
Simba ilifanikiwa kutetea taji hilo katika fainali
zilizofuata visiwani Zanzibar, ikiwa imeboresha zaidi kikosi chake kwa kuingiza
nyota wapya kama kipa Mwameja Mohamed, beki George Masatu na kiungo Hussein
Aman Marsha.
Simba iliyokuwa katika Kundi B, katika mechi ya kwanza
iliifunga 1-0 Bata Bullets FC ya Malawi, mechi ya pili iliifunga 2-0 Jamhuri SC
ya Pemba kabla ya kumalizia kwa sare ya bila kufungana na El Hilal ya Sudan,
hivyo kuingia Nusu Fainali.
Katika Nusu Fainali, Simba ilikutana na Small Simba SC ya Zanzibar
na kushinda 1-0, hivyo kutinga Fainali, ambako ilikwenda kukutana na watani wao
wa jadi, Yanga SC na kushinda kwa penalti 5-4 kufuatia sare ya 1-1 ndani ya
dakika 120 Uwanja wa Amaan.
MWAKA 1995:
Simba ilishindwa kutetea taji mjini Kampala, Uganda ingawa
bahati nzuri Kombe lilipakizwa kwenye ndege kurudishwa Dar es Salaam na watani
wao, Yanga. Kutoka hapo, Wekundu wa Msimbazi walilazimika kusubiri hadi mwaka
1995 kutwaa taji lingine la michuano hiyo.
Ilikuwa ni katika michuano mingine iliyofanyika Dar es
Salaam na Simba tena walipangwa Kundi A na katika mechi ya kwanza walitoka sare
ya 1-1 na Express FC ‘Red Eagles ’ ya Uganda, mechi ya pili waliichapa 3-1
Morris Supplies ya Somalia kabla ya
kuitandika 4-1 Adulis ya Ethiopia na kukata tiketi ya kuingia Nusu Fainali.
Katika Nusu Fainali, Simba ikiwa inaundwa na idadi kubwa ya
nyota wake walioifikisha timu Fainali za Kombe la CAF mwaka 1993, iliifunga 1-0
El Mourada ya Sudan na kuingia Fainali.
Katika Fainali, Simba ilikutana na Express ‘Red Eagles’ na
kushinda kwa penalti 5-3 kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 120, siku hiyo
George Magere Masatu akijifunga na kuwasawazishia bao Tai Wekundu dakika ya 53,
yaani dakika mbili tu tangu Hussein Amaan Marsha aifungie Sijmba bao la
kuongoza dakika ya 51.
MWAKA 1996:
Simba ilifanikiwa kwa mara ya pili na ya mwisho kihistoria
kutetea taji hilo, mwaka 1996 katika fainali zilizofanyika Tanzania tena,
kwenye miji ya Mwanza na Dar es Salaam.
Simba ilipangwa tena katika Kundi A mjini Dar es Salaam na
katika mechi ya kwanza, iliifunga 2-0 Small Simba ya Zanzibar, kabla ya kulala
1-0 mbele ya APR FC ya Rwanda na kumaliza kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Al Hilal
ya Sudan.
Kwa matokeo hayo, Simba ilishika nafasi ya pili katika kundi
hilo kwa pointi zake sita, ikizidiwa pointi moja tu APR iliyoongoza kundi hilo,
hivyo kutinga Nusu Fainali.
Katika Nusu Fainali, Simba ilishinda 1-0 dhidi ya Gor Mahia,
bao pekee la Bitta John hivyo kutinga
fainali, ambako ilikutana na APR na kulipa kisasi kwa ushindi wa 1-0, bao pekee
la George Magere Masatu dakika ya 115.
MWAKA 2002:
Mwaka 1997 michuano hiyo haikufanyika na mwaka 1998, Simba
ilishindwa kutetea taji, baada ya kuchukuliwa na Rayon Sport ya Rwanda visiwani
Zanzibar. Mwaka 1999, taji lilichukuliwa na Yanga mjini Kampala, Uganda na 2000
na 2001 Simba hawakupata tiketi ya kucheza michuano hiyo, hadi 2002 katika
fainali zilizofanyika visiwani Zanzibar.
Naam, Simba waliandika historia ya kuwa timu inayoongoza
kutwaa taji hilo, ilikuwaje?
Simba ilipangwa Kundi B na katika mchezo wa kwanza,
ililazimishwa sare ya bila kufungana na vibonde Elman ya Somalia, kabla ya
kuzinduka kwenye mechi ya pili na kuifunga Prince Louis ya Burundi, mabao 2-1,
wafungaji wake Emmanuel Gabriel dakika ya 27 na Yussuf Macho dakika ya 78, na
baadaye kuirarua Forodha ya Zanzibar mabao 3-1, wafungaji Joseph Kaniki ‘Golota’
dakika ya 22, Steven Mapunda ‘Garrincha’ dakika ya 65 na Macho ‘Musso’ dakika
ya 90 na mechi ya mwisho, bao la kujifunga la Kevin Malumbe dakika ya 88
liliwapa Wekundu wa Msimbazi ushindi wa 1-0 dhidi ya Tusker ya Kenya.
Kwa matokeo hayo, Simba iliongoza Kundi hilo kwa pointi zake
10, ikifuatiwa na Prince Louis iliyovuna pointi saba, Tusker pointi tano sawa
na Elman, wakati Forodha ilitoka patupu kabisa.
Katika Nusu Fainali, Simba ilikutana na mabingwa wa Zanzibar
enzi hizo, Mlandege na kushinda 2-0, mabao ya Yussuf Macho ‘Musso’ dakika ya 37,
na Shekhan Rashid Abdallah kwa penalti dakika ya 90.
Katika fainali, Simba ilikutana tena na Prince Louis na bao
pekee la Nteze John Lungu dakika ya sita, lilitosha kuwafanya Simba waitwe
mabingwa wa Kombe la Kagame mara nyingi zaidi hadi sasa.
Kikosi cha Simba siku hiyo kilikuwa; Mohamed Mwameja, Said
Sued, Ramadhan Wasso/Majuto Komu dk 35, Amri Said, Boniface Pawasa, Suleiman
Matola, Stephen Mapunda ‘Garrincha’/Joseph Kaniki dk 74, Shekhan Rashid, Yussuf
Macho, Nteze John/Emmanuel Gabriel dk 6 na Mark Sirengo.
Naam, hivyo ndivyo namna ambavyo Simba SC walivyobeba ndoo
sita za Kombe la Kagame na katika fainali za mwaka huu, wanaingia kusaka ndoo
ya saba ili kudhihirisha umwamba wao katika soka ya Afrika Mashariki na Kati,
nani atawazuia, Yanga tena? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona.
0 comments:
Post a Comment