• HABARI MPYA

    Thursday, August 09, 2012

    AZAM KUWAPOKONYA SIMBA NGASSA WAO, KISA REDONDO

    Ngassa akibusu jezi ya Yanga
    Na Mahmoud Zubeiry
    AZAM FC inafikiria kusitisha mpango wa kumtoa kwa mkopo katika klabu ya Simba SC, kiungo wake Mrisho Khalfan Ngassa, kufuatia kitendo cha Wekundu hao wa Msimbazi, kumsajili ‘kibabe’ kiungo wao mwingine, Ramadhan Chombo ‘Redondo’.
    “Tunapitia sheria na kanuni za usajili wa mkopo kuona kama tunaweza kufanya hivyo, tukigundua tunaweza, tunawapokonya mchezaji wetu, si watu waungwana hawa, na hatutahitaji tena uhusiano wa aina yoyote na wao, labda klabu ipate viongozi wengine, si hawa wa sasa,”alisema kiongozi mmoja wa Azam, alipozungumza na BIN ZUBEIRY jioni hii.
    Azam walimtoa kwa mkopo Ngassa wiki iliyopita, baada ya kukerwa na kitendo cha mchezaji huyo kubusu jezi ya timu yake ya zamani, Yanga, katika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
    Alifanya hivyo, baada ya kufunga bao la ushindi akitokea benchi na kuiwezesha Azam kutinga fainali ya michuano hiyo, ambako walifungwa na Yanga 2-0, naye kwa mara nyingine akitokea benchi na kushindwa kufunga, hivyo kutuhumiwa kucheza kinazi.
    Ilielezwa kwamba Simba walitoa Sh. Milioni 25 kumnunua kwa mkopo mchezaji huyo, ingawa baadaye Simba wakasema waliununua mkataba wa mwaka mmoja aliobakiza mchezaji huyo Azam FC, nao wakamuongezea wa mwaka mmoja kwa kumsainisha kwa Sh. Milioni 30, kati ya hizo Milioni 12 akipewa taslimu na 18 akipewa gari.
    Inavyoonekana, Redondo aliwadanganya Simba kwamba amemaliza mkataba na Azam, wakaingia mkenge na kumpa Sh. Milioni 30 wakimsainisha mkataba wa miaka miwili, wakati mkataba wake na Azam unamalizika Juni mwakani.
    Hili ni kosa sawa na ambalo Simba walilifanya katika usajili mwingine wa mchezaji wa Azam, Ibrahim Rajab ‘Jeba’, miezi mitatu iliyopita ambaye alikuwa kwa mkopo Villa Squad wao wakaenda kumsajili bila kuwasiliana na klabu yake kujua kuhusu mkataba wake, matokeo yake baadaye mchezaji huyo akarejea Azam.
    Simba nao wana lalamiko kama hilo, dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga wanaowatuhumu kumsajili beki Kevin Yondan, wakati bado ana makataba na Wekundu hao wa Msimbazi, ingawa TFF iliweka sawa kwa kusema Yondan hakuwa na mkataba na Simba SC.
    Baadaye Simba ilitoa ufafanuzi, kwamba ilimuongezea mkataba Yondan baada ya ule wa awali kumalizika na ikawa inasubiri muda wa usajili ufike wauwasilishe TFF. Lakini katika kesi ya awali, Simba walipoupeleka mkataba wao mpya na Yondan, ulionyesha mchezaji huyo anatakiwa kuanza kuutumikia mkataba huo, Desemba mwaka huu, hivyo TFF ikasema kwa wakati ambao yuko huru, aichezee Yanga.
    Sakata la Yondan litarudi Desemba, wakati ambao atatakiwa kuanza kuutumikia mkataba wake na Simba, wakati yupo ndani ya mkataba wa miaka miwili na Yanga.
    Ngassa alipotambulishwa Simba; hapa akikabidhiwa jezi na Makamu Mwenyekiti wa Simba SC, Geoffrey Nyange 'Kaburu'

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM KUWAPOKONYA SIMBA NGASSA WAO, KISA REDONDO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top