• HABARI MPYA

    Tuesday, August 14, 2012

    SIMBA WAENDA KWA KASI YA USAIN BOLT KUKAMILISHA USAJILI, AZAM WATAKA MILIONI 50 KWA REDONDO

    Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili Simba SC; Zakaria Hanspop

    Na Mahmoud Zubeiry
    MABINGWA wa soka Tanzania, Simba SC, hivi sasa wanakwenda mbio kwa kasi ya Usain Bolt kukamilisha usajili wao, kabla ya dirisha kufungwa kesho.
    Azam FC wanataka Sh. Milioni 50 kabla ya dirisha la usajili kufungwa saa 6:00. usiku kesho ili kumuachia kiungo Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kesho na hivi sasa Simba SC wapo kwenye kikao kizito kujadili namna ya kukamilisha usajili wao, kabla ya dirisha hilo kufungwa.
    Mapema leo, asubuhi BIN ZUBEIRY iliripoti kwamba, Azam imekubali kupokea Sh. Milioni 15 kutoka Simba SC ili kumuuza Redondo wa Ngomati kwa Wekundu hao wa Msimbazi, lakini baada ya kuzama ndani, upande wa pili, imegundua zinatakiwa Milioni 50 za Tanzania.
    BIN ZUBEIRY ilijaribu kumpigia simu, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zakaria Hanspop ambaye ‘amecheza bonge la Pele’ dakika za lala salama kuokoa usajili wa klabu hiyo, ambao ulivurundwa vibaya na ‘Maamuma wa soka’ waliomo ndani ya klabu hiyo, lakini akasema; “Nipo kwenye kikao, nipigie baada ya saa moja,”.
    Habari za ndani ambazo BIN ZUBEIRY imezipata, zimesema kwamba Azam wako tayari kupokea fedha kumuuza Redondo, kufuatia viongozi wa Simba SC kuwaangukia Azam kwa kitendo chao cha kumsajili kiungo huyo bila kuwasiliana nao, wakati bado alikuwa ana mkataba na Wana Lamba Lamba.
    Awali, Azam walikerwa na kitendo hicho hadi wakataka kusitisha dili la kumtoa kwa mkopo kwa Mrisho Khalfan Ngassa Simba SC.
    Azam walimtoa kwa mkopo Ngassa, baada ya kukerwa na kitendo cha mchezaji huyo kubusu jezi ya timu yake ya zamani, Yanga, katika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) mwezi uliopita.
    Alifanya hivyo, baada ya kufunga bao la ushindi akitokea benchi na kuiwezesha Azam kutinga fainali ya michuano hiyo, ambako walifungwa na Yanga 2-0, naye kwa mara nyingine akitokea benchi na kushindwa kufunga, hivyo kutuhumiwa kucheza kinazi.
    Ilielezwa kwamba Simba walitoa Sh. Milioni 25 kumnunua kwa mkopo mchezaji huyo, ingawa baadaye Simba wakasema waliununua mkataba wa mwaka mmoja aliobakiza mchezaji huyo Azam FC, nao wakamuongezea wa mwaka mmoja kwa kumsainisha kwa Sh. Milioni 30, kati ya hizo Milioni 12 akipewa taslimu na 18 akipewa gari.
    Inavyoonekana, Redondo aliwadanganya Simba kwamba amemaliza mkataba na Azam, wakaingia mkenge na kumpa Sh. Milioni 30 wakimsainisha mkataba wa miaka miwili, wakati mkataba wake na Azam unamalizika Juni mwakani.
    Hili ni kosa sawa na ambalo Simba walilifanya katika usajili mwingine wa mchezaji wa Azam, Ibrahim Rajab ‘Jeba’, miezi mitatu iliyopita ambaye alikuwa kwa mkopo Villa Squad wao wakaenda kumsajili bila kuwasiliana na klabu yake kujua kuhusu mkataba wake, matokeo yake baadaye mchezaji huyo akarejea Azam.
    Simba nao wana lalamiko kama hilo, dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga wanaowatuhumu kumsajili beki Kevin Yondan, wakati bado ana makataba na Wekundu hao wa Msimbazi, ingawa TFF iliweka sawa kwa kusema Yondan hakuwa na mkataba na Simba SC.
    Baadaye Simba ilitoa ufafanuzi, kwamba ilimuongezea mkataba Yondan baada ya ule wa awali kumalizika na ikawa inasubiri muda wa usajili ufike wauwasilishe TFF. Lakini katika kesi ya awali, Simba walipoupeleka mkataba wao mpya na Yondan, ulionyesha mchezaji huyo anatakiwa kuanza kuutumikia mkataba huo, Desemba mwaka huu, hivyo TFF ikasema kwa wakati ambao yuko huru, aichezee Yanga.
    Sakata la Yondan litarudi Desemba, wakati ambao atatakiwa kuanza kuutumikia mkataba wake na Simba, wakati yupo ndani ya mkataba wa miaka miwili na Yanga.
    Simba pia inafikiria kuvunja mkataba na kiungo Mganda, Mussa Mudde wakati ikiwa kwenye mazungumzo na wachezaji wanne wengine wa kigeni beki, wawili kutoka Mali, mmoja Tusker ya Kenya na mshambuliaji kutoka Ivory Coast, ambao imeelezwa wanaweza kuwasili leo kujiunga na timu hiyo.
    Tayari Simba imeacha kiungo mmoja wa kigeni, Kanu Mbivayanga kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na kusajili beki Paschal Ochieng kutoka AFC Leopard ya Kenya na mshambuliaji Daniel Akuffo kutoka Hearst Of Oak ya Ghana, ambaye pia raia wa Ivory Coast.
    Habari kutoka Arusha, ambako Simba imeweka kambi kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu, zimesema kwamba katika siku ya kwanza ya mazoezi yao na kikosi hicho leo, wachezaji wote hao wawili wameonyesha viwango vya hali ya juu.
    Imeelezwa kwamba, mshambuliaji Akuffo ni hatari mno na kwa haraka haraka hakuna wa kumfananisha naye kati ya washambuliaji wote waliopo Tanzania kwa sasa.
    Anasifiwa kuwa na uwezo mkubwa wa kumiliki mpira, kasi, nguvu, ufundi na mbinu za kimchezo- maana yake Wekundu wa Msimbazi wamelamba dume. Kama wachezaji wapya wanaotua leo watamridhisha kocha Mserbia, Profesa Milovan Cirkovick, Simba itamtema Mudde na kubaki na idadi ya wachezaji wa kigeni watano kama inavyoelekeza kanuni ya usajili ya Ligi Kuu kuhusu wachezaji wa kigeni.
    Wachezaji wengine wa kigeni kwenye kikosi cha Simba SC ni washambuliaji Mganda Emmanuel Okwi na Mzambia Felix Sunzu.   
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA WAENDA KWA KASI YA USAIN BOLT KUKAMILISHA USAJILI, AZAM WATAKA MILIONI 50 KWA REDONDO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top