Na Princess Asia, Gaborone
KIKOSI cha timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars
kikiwa na wachezaji 17 kimewasili leo asubuhi jijini Gaborone tayari kwa mechi
ya kirafiki ya kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA)
dhidi ya wenyeji Botswana 'Zebras' itakayochezwa kesho.
Stars ilitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sir
Seretse Khama saa 5.45 asubuhi kwa saa za hapa ambapo nyumbani ni 6.45 na
kupokewa na viongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu Botswana (BFA) na Watanzania
wanaoishi hapa Botswana.
Baadhi ya wachezaji walioko kwenye kikosi hicho ni Frank
Domayo, Ramadhan Singano na Simon Msuva ambao walijiunga na Stars saa chache
baada ya kurejea kutoka Nigeria ambapo walikuwa na timu ya vijana wenye umri
chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes) ambayo Jumapili ilicheza mechi ya
mashindano ya Afrika dhidi ya Nigeria (Flying Eagles).
Wachezaji wengine kwenye kikosi kilichoko Botswana ni Aggrey
Morris, Amir Maftah, Athuman Idd, Erasto Nyoni, Haruna Moshi, Juma Kaseja,
Kelvin Yondani, Mrisho Ngassa, Mwadini Ally, Mwinyi Kazimoto, Ramadhan Chombo,
Salum Abubakar, Said Bahanuzi na Shabani Nditi.
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imefikia
kwenye hoteli ya Oasis ambayo pia ndipo Zebras imepiga kambi kwa ajili ya mechi
hiyo. Mechi itaanza kesho saa 1 kamili usiku kwa saa za hapa na itafanyika
kwenye Uwanja wa Molepolole Sports Complex. Uwanja wa Taifa wa Botswana hivi
sasa uko kwenye matengenezo.
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen amesema mechi hiyo ni
muhimu kwa vile timu yake bado inakabiliwa na mechi za Kombe la Dunia Kanda ya
Afrika, na michuano ya Kombe la Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN)
inayotarajia kuanza baadaye mwaka huu.







.png)
0 comments:
Post a Comment