![]() |
Mbuyu Twite |
Na Mahmoud Zubeiry
KLABU
za Simba na Yanga zimeshindwa kufikia suluhu mbele ya Kamati ya Sheria, Maadili
na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), chini ya Mwenyekiti
wake Alex Mgongolwa, katika kikao cha leo, juu ya wachezaji Kevin Yondan na Mbuyu
Twite.
Katika
kikao hicho kilichoanza majira ya saa 7:00 mchana, hoja ya kwanza kuwasilishwa
mezani ilikuwa ni suala la beki Twite na upande wa Yanga uliwakilishwa na
Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga na Katibu, Celestine Mwesigwa wakati kwa Simba
walikuwepo Makamu Mwenyekiti, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ na Mwenyekiti wa Kamati
ya Usajili, Kapteni wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Zacharia
Hans Poppe.
Ikumbukwe,
Simba iliwasilisha malalamiko ya kufanyiwa mchezo usio wa kiungwana na Yanga kwa
Twite. Ilidai Twite alisaini mkataba na klabu yao Agosti 1, mwaka huu mbele
yao, viongozi wa Shirikisho la Soka Rwanda (FERWAFA) na APR na kulipwa dola za
Kimarekani 30,000 na nyingine 2,000 za nauli ya kuja Dar es Salaam kujiunga na
klabu hiyo. Hata hivyo, mchezaji huyo akahamia Yanga.
Katika
mjadala huo, Simba ilikubali kurudishiwa fedha zao, lakini viongozi wa Yanga
wakasema hawawezi kutoa hadi waombwe radhi na Mwenyekiti wa Simba, Alhaj Ismail
Aden Rage, ambaye alisema viongozi wa klabu hiyo yenye maskani yake makutano ya
mitaa ya Twiga na Jangwani wana ‘fedha chafu za EPA’.
Simba
wakasema kauli yake ya Rage ilikuwa sehemu ya utani wa jadi, kama ambavyo Yanga
walimvalisha jezi Twite yenye jina la Rage.
Kufikia
hapo, Simba wakasema hawawezi hata kujadili suala la Kevin Yondan na Kamati ya
Mgongolwa ikasema itapitia maelezo ya pande zote, watatoa majibu kwa mujibu wa
kanuni na sheria Septemba 10, mwaka huu.
Katika
kesi ya Yondan, walalamikaji ni Simba, ambao wanadai beki huyo alisaini Yanga
akiwa bado ana mkataba na klabu yao.
Awali,
Kamati ya Mgongolwa ilikutana Jumapili asubuhi hadi usiku, bila kupata
suluhisho la pingamizi hizo na kuamua kutumia busara ya kuzikutanisha pande zinazopingana
kujaribu kupata suluhu leo.
Pingamizi
nyingine zilikuwa ni, Azam inayopinga usajili wa Ramadhan Chombo ‘Redondo’
kwenda Simba kwa maelezo bado ina mkataba naye unaomalizika Juni 11 mwakani na
inaelezwa tayari klabu hizo zimekwishamalizana juu ya kiungo huyo.
Yanga
inapinga Simba kuwaacha wachezaji Dan Mrwanda, Haruna Shamte, Kanu Mbiyavanga
na Lino Masombo kwa maelezo walishapatiwa leseni za kucheza Ligi ya Tanzania
walizozitumia kwenye mashindano ya Kombe la Kagame. Pia inapinga Ramadhan
Chombo ‘Redondo’ kujiunga Simba kwa vile ana leseni ya kuchezea Azam kwa msimu
wa 2012/2013.
Pingamizi
lingine la Yanga kwa Simba ni kuwa imezidisha idadi ya wachezaji wa kigeni
wanaotakiwa kusajiliwa kwa maelezo inao wanane wakati wanaoruhusiwa ni watano.
Imewataja wachezaji hao kuwa ni Lino Masombo, Felix Sunzu, Emmanuel Okwi, Mussa
Mude, Kanu Mbiyavanga, Pascal Ochieng, Komalmbil Keita na Daniel Akuffor.
Pingamizi
nyingine ambazo jumla zinahusu wachezaji 17 walioombewa usajili katika timu za
Ligi Kuu ni Toto Africans ya Mwanza imewawekea pingamizi wachezaji Enyinna
Darlington aliyeombewa usajili Kagera Sugar, na Mohamed Soud anayekwenda
Coastal Union kwa maelezo kuwa bado ina mikataba na wachezaji hao.
Pia
Flamingo ya Arusha inapinga usajili wa wachezaji wake Kelvin Friday Iddy katika
timu za Azam na Salim Walii (Polisi Mara) kwa vile taratibu za kuwahamisha bado
hazijafanywa. Nayo Kagera Sugar inapinga usajili wa beki David Charles Luhende
kwenda Yanga kwa vile ada ya uhamisho haijalipwa.
Super
Falcon ya Chanjamjawiri, Chakechake, Pemba inapinga wachezaji wake wanne;
Edward Christopher Shija, Samir Said Luhava (Simba), Robert Joseph Mkhotya
(African Lyon) na Sultan Juma Shija (Coastal Union) kusajiliwa katika timu hizo
kwa maelezo taratibu halali za uhamisho hazikufuatwa.
Mchezaji
Othman Hassan aliyeombewa usajili Coastal Union anapingwa na Oljoro JKT kwa
vile bado ana mkataba na timu hiyo unaomalizika Mei 24, 2013. Nayo Rollingstone
Multipurpose Ateclass Foundation ya Arusha inapinga usajili wa Kigi Makassy
kutoka Yanga kwenda Simba hadi itakapolipwa fidia ya kumlea mchezaji huyo kwa
vile bado hajafikisha umri wa miaka 23.
0 comments:
Post a Comment