![]() |
Na Mahmoud Zubeiry |
NILIMSIKIA kwa masikio yangu, Katibu Mkuu wa Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah Malabeja anaisifia Rwanda, timu yao ya
taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, baada ya kuwafunga mara mbili
mfululizo vijana wa Tanzania, Ngorongoro Heroes katika mechi za kujipima nguvu
Dar es Salaam.
Sisi tulianza kucheza mechi za kimataifa miaka ya 1960,
wakati Rwanda walianza mwaka 1998 na mwaka jana timu yao ya taifa ya vijana
chini ya umri wa miaka 17, ilishiriki fainali za vijana wa umri huo za Kombe la
Dunia.
Katika fainali hizo zilizofanyika nchini Mexico, Rwanda
haikuvuka hatua ya makundi, lakini ilipigana kiume, ilifungwa mechi mbili, 2-0
na England U17 na 1-0 na Uruguay U17 kabla ya kutoa sare ya bila kufungana na Canada
U17 katika mechi ya mwisho.
Kwa ujumla hivi sasa Tanzania tumeachwa mbali kisoka na
Rwanda, katika viwango vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) wapo nafasi
ya 125 wakati Desemba mwaka 2008, walipanda hadi nafasi ya 78 na sisi tupo
nafasi ya 128 wakati kupanda zaidi kwetu ilikuwa Desemba 2007, nafasi ya 89 na
Oktoba mwaka 2005 tuliporomoka hadi nafasi ya 175.
Mara kadhaa nimewahi kuandika umuhimu wa kuwekeza kwenye soka
ya vijana na nikaelezea faida za kuomba kuandaa fainali za vijana za Afrika
badala ya haya mabonanza ya Kombe la Challenge la CECAFA, lakini nadhani kwa
wakubwa bado hiyo haina maana kwao na kwa sababu hiyo, tutaendelea kuburuza
mkia.
Sioni sifa za Rwanda hata watuzidi kisoka leo- nchi ndogo na
imeingia kwenye soka ya kimataifa juzi juzi tu na hata Ligi Kuu yao haina ubora
na ushindani kama ligi yetu- lakini kwa sababu ya mipango yao thabiti ya
uwekezaji katika soka la vijana, wametuacha na watatuacha sana iwapo
hatutobadilika.
Mwaka 2011 Rwanda walikuwa wenyeji wa fainali za U17 za
Afrika, ambazo walifanikiwa kuingia fainali na kufungwa mabao 2-1 na Burkina
Faso.
Awali ya hapo, mwaka 2009, Rwanda walikuwa wenyeji wa fainali
za Afrika za U-20 na japokuwa hawakufanikiwa kutoka kwenye kundi lao, A, lakini
walionyesha soka ya kuvutia, nachoweza kusema bahati haikuwa yao.
Walishika nafasi ya tatu nyuma ya Ghana na Cameroon zilizosonga
mbele, na wao wakawa juu ya Mali iliyoshika mkia. Walishinda mechi moja (2-1
dhidi ya Mali) na kutoa sare mechi moja, (1-1 na Cameroon) wakati moja
walifungwa (2-0 na Ghana), iliyokwenda kuchukua hadi Kombe la Dunia, ikiifunga
Brazil kwa penalti 4-3 nchini Misri, baada ya sare ya bila kufungana ndani ya
dakika 120.
Faida ya uwekezaji huo ni timu imara ya taifa tuliyoishuhudia
mwaka jana ikicheza soka safi katika Kombe la Challenge na kufika fainali,
ambako ilifungwa kwa taabu na Uganda.
Kikosi cha Rwanda katika fainali za U20 mwaka 2009, kiliundwa
na akina Jean-Luc Ndayishimiye, Aimable Rucogoza, Annuar Kibaya, Arafat
Serugendo, Michel Hitimana, Jean-Claude Iranzi, Jean Mugiraneza, Haruna Niyonzima,
Elias Uzamukunda, Herman Ngoma, Ernest Kwizera, Yussuf Ndayishimiye, Jean Bosco
Ngaboyisibo, Robert Muvunyi, Aboubakar Nshimiyimana, Bonfils Christian Twahirwa,
Eric Habimana na Emery Mvuyekure ambao wengi wao wanaibeba Amavubi hivi sasa.
Wakati huo huo, vijana waliocheza Kombe la Dunia la U17
Mexico mwaka jana wanakuja vizuri kueleeka kuunda timu bora ya kizazi kipya cha
Rwanda.
Msingi wa mwisho mzuri wa soka ya vijana Tanzania uliokaribia
kuzaa matunda ulikuwa ni timu ya mwaka 2004, enzi za Muhiddin Ndolanga pale
TFF, timu ambayo ilikuwa inaundwa na akina Athumani Iddi ‘Chuji’, Nizar
Khalfan, Juma Jabu, Amir Maftah, Omary Matuta, Nurdin Bakari, Adam Matunga na
wengineo, ambao sasa hivi wakicheza wanaitwa ‘babu’.
Timu hiyo ilifuzu kucheza fainali za vijana Afrika
zilizofanyika Gambia, lakini ikaenguliwa kutokana kashfa ya kufoji umri wa
Nurdin Bakari na nafasi wakapewa Zimbabwe ambao kwa pamoja na Rwanda na Zambia,
walitolewa na Serengeti Boys yetu iliyokuwa chini ya makocha Abdallah ‘King’
Kibadeni na Sylvester Marsh.
Baada ya hapo, kwa muda mrefu chini ya utawala wa Leodegar
Chilla Tenga, hatukushiriki mashindano ya vijana hadi mwaka 2010 kama sikosei
tulipoanza kurudi taratibu, tena baada ya kelele nyingi za wadau.
Kwa kuwa tuna misingi mizuri ya awali ya uibuaji wa vipaji
vya vijana, mara zote hatukosi timu, tatizo letu ni kukosa programu nzuri
endelevu na kwa ujumla namna ya kuandaa timu. Hapo bado tuna ‘0’ mbaya.
Kwa sasa, Serengeti Boys imefuzu katika Raundi ya Pili
kuwania kucheza fainali za mwakani nchini Morocco na itacheza na Misri, baada
ya kupita bila jasho kutoka Raundi ya kwanza, kufuatia kujitoa kwa Kenya.
Serengeti ilikuwa icheze mechi ya kwanza na Kenya Septemba 9,
mwaka huu mjini Dar es Salaam, hata
hivyo, Shirikisho la Soka Kenya (FKF) likatuma taarifa Shirikisho la Soka
Afrika (CAF) ya kujitoa kwenye michuano hiyo.
Serengeti Boys sasa itaanzia nyumbani Oktoba 14, mwaka huu na
Misri, wakati mechi ya marudiano itachezwa nchini Misri kati ya Oktoba 26 na 28
mwaka huu. Mshindi baada ya mechi hizo mbili ataingia raundi ya tatu ambayo
ndiyo ya mwisho kabla ya kuelekea Morocco.
Katika raundi ya tatu ambayo mechi zake zitachezwa katikati
ya Novemba na ya marudiano mwishoni mwa mwezi huo, Serengeti ikiitoa Misri itacheza
na mshindi kati ya Kongo Brazzaville na ama Msumbiji au Zimbabwe ambazo
zinapambana katika raundi ya kwanza.
Wachezaji wanaounda kikosi cha Serengeti Boys ya sasa chini
ya Kocha Mdenmark, Jakob Michelsen ni makipa Abdallah Bakar (Mjini Magharibi),
Hamad Juma (Azam) na Peter Manyika (JKT Ruvu), mabeki ni Abdallah Salum (Mjini
Magharibi), Basil Seif (Morogoro), Hassan Mganga (Morogoro), Ismail Gambo
(Azam), Mgaya Abdul (Azam), Miraji Selemani (Polisi Morogoro), Miza Abdallah
(Kinondoni), Mohamed Hussein (Azam), Pascal Matagi (Dodoma) na Paul James
(Kinondoni).
Viungo ni Farid Musa (Kilimanjaro), Hussein Twaha (Coastal
Union), James Mganda (Kipingu Academy), Mbwana Ilyasa (Simba), Mohamed Haroub
(Zanzibar), Mohamed Kapeta (Kinondoni), Mudathiri Yahya (Azam), Mzamiru Said (Morogoro)
na Selemani Bofu (JKT Ruvu) na washambuliaji ni Abdallah Kisimba (Mwanza),
Calvin Manyika (Rukwa), Dickson Ambunda (Mwanza), Joseph Lubasha (Azam), Kelvin
Friday (Azam) na Salvatory Nkulula (Kipindu Academy).
Kulingana na msingi mzuri wa kuibua vipaji vya wanasoka
chipukizi uliopo nchini hivi sasa, kuanzia Copa Coca Cola, Airtel Rising Star,
mashindano ya shule za msingi na sekondari na hata akademi, au vituo kadhaa vya
soka tulivyonavyo kwa sasa Tanzania- hakuna shaka juu ya timu hii ni nzuri.
Lakini je, tujiulize tuna dira mwafaka ya kutufikisha Morocco
mwakani? Jana TFF wametoa taarifa timu hiyo imekwenda Mbeya kuweka kambi kwa
sababu ya mwaliko wa Chama cha Soka Mbeya Mjini (MUFA), ambacho, kitaihudumia
kwa malazi, chakula na huduma nyingine ndogondogo na itacheza mechi kadhaa za
majaribio ikiwemo dhidi ya Mbeya City na Tanzania Prisons.
Sawa- kambi Mbeya sawa. Lakini tunaona nini hapa? Kwa kuwa
MUFA wamejitolea kuihudumia timu ndiyo maana imepelekwa Mbeya, au ni programu
ya maandalizi ndiyo imeipeleka timu Mbeya? Sioni nini kinaendelea hapa, zaidi
ya maandalizi ya zimamoto tu ambayo miaka nenda, rudi yametufanya tumekuwa
wasindikizaji na tunapitwa na vi- nchi vidogo vidogo kama Rwanda.
Naamini, huu ni wakati mwafaka sasa kuwekeza katika maandalizi
ya kisayansi kwa Serengeti Boys, ambayo inaundwa na vijana wasio na majukumu
kwa klabu yoyote, ambao kuwandaa ni jambo jepesi mno.
Kambi ya muda mrefu yenye tija ndiyo inayohitajika na si
kambi kwa sababu mtu kajitolea kuhudumia timu. Tuna Idara ya Ufundi, timu ina
kocha wa kigeni, anayesaidiwa na kocha mzoefu tu, Jamhuri Kihwelo, tunahitaji
programu ya maandishi ya maandalizi, ipelekwe kwa sekretarieti, ambayo
itatakiwa kuandika mependekezo ya bajeti, watafutwe wadhamini wa kugharamia.
Au ikishindikana, tukumbuke mafanikio ya Serengeti ya akina
Chuji na Nizar- harambee ya wananchi iliiwezesha, basi TFF ishirikiane na
vyombo vya habari kuanzisha kampeni ya kuichangia timu, iweze kupata maandalizi
mazuri, dira yetu ikiwa ni kucheza Fainali za Kombe la Dunia za vijana wa umri
huo mwakani Falme za Kiarabu (UAE). Nawasilisha.
0 comments:
Post a Comment