Na Mahmoud Zubeiry
Komabil Keita, pia hajawahi kuonekana Dar |
SIMBA SC
ilitua Dar es Salaam jana jioni na leo asubuhi inatarajiwa kufanya mazoezi
kwenye Uwanja wa Sigara, Chang’ombe, kabla ya kushuka dimbani kesho kumenyana
na waliowahi kuwa mabingwa wa Kenya, Sofapaka FC, Uwanja wa Taifa.
Simba,
ambayo mara ya mwisho Simba ilicheza Dar es Salaam Agosti 8, na kufungwa mabao
3-1 na City Stars ya Nairobi, Kenya Uwanja wa Taifa, kwa zaidi ya mwezi mmoja
ilikuwa kambini Arusha ikijifua vikali kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara, ambao wao ni mabingwa watetezi.
Kwa sasa
kiwango cha Simba, inayofundishwa na Mserbia, Profesa Milovan Cirkovick,
akisaidiwa na Mganda, Richard Hamatre, kipo vizuri na timu inaonekana iko
tayari kwa Ligi Kuu. Pamoja na Jumapili kulazimishwa sare ya 1-1 na Sony Sugar
ya Kenya, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, lakini Simba ilicheza soka
safi na washambuliaji wake walikosa mabao ya wazi zaidi ya matano.
Lakini hata
hali mbaya ya Uwanja wa Sheikh Amri Abeid katika eneo la kuchezea inachangia kupunguza
idadi ya mabao kwa Simba. Katika mechi tatu ambazo Simba imecheza kwenye Uwanja
huo, imevuna mabao matano na kufungwa matatu, na kikwazo kimekuwa kikionekana ni
hali ya eneo la kuchezea.
Katika
mchezo wa Jumapili, bao la Simba lilifungwa na Daniel Akuffo, wakati Komabil
Keita alijifunga katika jitihada za kuokoa na kuwapa Wakenya bao la kuongoza. Awali,
Simba ilicheza mechi mbili Arusha, dhidi ya Mathare United ya Kenya na JKT
Oljoro ya Arusha, ambazo zote ilishinda 2-1, mshambuliaji mpya Daniel Akuffo
kutoka Ghana akifunga bao moja kila mechi, Kiggi Makaasy na Mrisho Ngassa
wakifunga mabao mengine.
Kitu kimoja
tu ambacho Milovan anapaswa kuendelea kufanyia kazi ni makosa ya safu ya ulinzi
na mawasiliano duni na makipa wao.
Ilivyo sasa
kipa yeyote anayesimama kwenye lango la Simba SC, kabla ya kuchunga wachezaji
wa timu pinzani, anakuwa na jukumu la kwanza la kujihadhari na mabeki wake
wasimfunge, kwani mabeki wawili wa kati wa timu hiyo wamekwishaonyesha
‘kipaji cha kujifunga’ katika mechi za karibuni,
Juma Nyosso na Komabil Keita.
Simba
inajiandaa na mechi ya Ngao ya Jamii Septemba 11, mwaka huu, Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam dhidi ya Azam FC, ambayo kihistoria hiyo itakuwa mechi ya tano ya
Ngao ya Jamii kuchezwa nchini na ya pili kukutanisha timu nje ya wapinzani wa
jadi wa soka ya Tanzania, Simba na Yanga.
Mtibwa
ilicheza na Yanga mwaka 2009, baada ya Simba kugoma na ikashinda mabao 2-1 na
kutwaa Ngao, wakati kabla ya hapo, mwaka 2001, Ligi Kuu ya Tanzania ikiwa bado
inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Safari Lager,
ilichezwa mechi ya kwanza ya Ngao kihistoria.
Katika mechi
hiyo, Yanga ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Simba na mwaka juzi Yanga iliifunga
tena Simba kwa penali 3-1 kufuatia sare ya 0-0 na mwaka jana, Simba ilitwaa
Ngao ya kwanza katika historia yake, kwa kuifunga Yanga mabao 2-0.
MABINGWA WA MECHI ZA NGAO YA JAMII:
Mwaka Mshindi Matokeo
2001 Yanga 2-1 Simba
2010 Yanga 0-0 Simba (3-1penalti)
2011 Simba 2-0 Yanga
0 comments:
Post a Comment