• HABARI MPYA

    Wednesday, December 05, 2012

    KIIZA: BOCCO ATAKUTANA NA UKUTA WA ZEGE

    Kiiza

    Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
    MSHAMBULIAJI wa Uganda, Hamisi Kiiza ‘Diego’ amesema John Raphael Bocco ‘Adebayor’ wa Tanzania Bara ni mkali, lakini ajue The Cranes ina ukuta ambao haujaruhusu hata bao moja, hivyo asitarajie kufunga bao kesho katika Nusu Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana, Uwanja wa Mandela, Namboole, Kiiza alisema kwamba anamfahamu Bocco na kwenye Challenge ya mwaka huu anang’ara sana, lakini kesho atakutana na ukuta wa wanaume wa shoka.
    “Tunaiheshimu Tanzania ni timu nzuri, na zaidi mfumo wao wanaocheza hivi sasa ni mzuri sana, lakini hata sisi ni wazuri, hiyo mechi itakuwa kali sana,”alisema mshambuliaji huyo wa klabu ya Yanga SC ya Dar es Salaam.
    Kiiza alisema mbali na Bocco, Tanzania Bara ina mchezaji mwingine hatari, Mrisho Ngassa lakini wote wajue kwamba watakutana na ukuta wa Uganda, ambao katika mechi nne haujaruhusu hata bao moja.
    Uganda jana ilifuzu kuingia Nusu Fainali ya Challenge, baada ya kuifunga Ethiopia mabao 2-0, ambayo yalitiwa kimiani na Geoffrey Kizito dakika ya nne na Robert Ssentongo dakika ya 60.
    Kwa ushindi huo, Uganda itamenyana na Tanzania Bara katika Nusu Fainali Alhamisi usiku, mchezo ambao utatanguliwa na Nusu Fainali nyingine kati ya Kenya na Zanzibar, itakayoanza saa 10:00 jioni.
    Kenya ilifuzu Nusu Fainali jana, baada ya kuifunga Malawi 1-0, bao pekee la Mike Barasa dakika ya 56.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: KIIZA: BOCCO ATAKUTANA NA UKUTA WA ZEGE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top