• HABARI MPYA

    Monday, December 10, 2012

    UGANDA ONE ATUA LEO DAR KUMALIZANA NA SIMBA SC

    Dhaira

    Na Mahmoud Zubeiry
    MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema kwamba, kipa namba moja wa Uganda, Abbel Dhaira anatua leo Dar es Salaam kwa ajili ya kusaini mkataba wa kuanza kuitumikia klabu hiyo.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana, Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) aliyepigana vita dhidi ya Uganda, alisema kwamba baada ya kumalizana na kipa huyo, watahamia kwenye suala la mshambuliaji Brian Umony pia wa Uganda. 
    Hata hivyo, mapema juzi akizungumza na BIN ZUBEIRY, Dhaira alisema kwamba anataka Simba wamtume mtu Kampala, Uganda na fedha ili asaini akiwa huko.
    Dhaira alisema kwamba hawezi kujihesabu kama tayari yeye ni kipa wa Simba hadi hapo watakaposaini mkataba, kwani kwa sasa wamezungumza na kufikia makubaliano, ila ikitokea timu nyingine ya kumaliza naye haraka, hatasita kufanya hivyo.
    “Simba wamezungumza na mimi ndio, lakini hatujamalizana, wao wakituma mtu kuja huku tukasaini, hapo ndio nitakuwa nimejifunga, ila kwa sasa kama ipo timu nyingine hata huko Tanzania inanitaka, milango bado iko wazi,”alisema Dhaira.
    Dhaira alisema kimsingi yeye yuko tayari kujiunga na Simba kwa kuwa ni klabu kubwa Afrika na inacheza Ligi ya Mabingwa Afrika na angependa kuungana na Mganda mwenzake, Emmanuel Okwi huko.
    Tayari Simba SC imefikia makubaliano na kipa huyo namba moja wa Uganda, aliyemaliza mkataba wake na klabu ya I.B.V FC ya Iceland na amekubali kusaini mkataba wa miaka miwili kwa dau ambalo halijafahamika.
    Dhaira alisema kwamba amefikia makubaliano na Simba kusaini mkataba wa miaka miwili kuja kuanza maisha mapya Dear es Salaam.
    Dhaira ambaye aliibukia Express ya hapa mwaka 2006 kabla ya 2008 kuhamia U.R.A. pia ya hapa, ambayo aliichezea hadi 2010 alipohamia Ulaya atatua Dar es Salaam Jumatatu kumaliza kila kitu Simba.
    Ikimpata Dhaira, Simba SC itakuwa imepata kipa wa uhakika wa kusaidiana na kipa wake wa kwanza, Juma Kaseja ambaye amekuwa akisotoshwa peke yake bila kupumzika. Na hiyo inafuatia makipa wengine, Wilbert Mweta na Hamadi Waziri kushindwa kuonyesha uwezo wa kumsaidia Kaseja.
    Katika mechi za mwishoni za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara, Kaseja alionekana kuchoka na kudaka chini ya kiwango chake, jambo ambalo lilisababisha mashabiki wenye ‘akili mbovu’ wamfanyie fujo baada ya kufungwa mabao mawili katika mechi dhidi ya Mtibwa Sugar, Simba ikilala 2-0.
    Kwa sababu hiyo, Kaseja alikasirika na kujiengua kwenye kikosi cha timu hiyo akisema hataki tena kuchezea Simba.
    Lakini pamoja na matatizo hayo, Kaseja aliitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ambako ameendelea kufanya vizuri na kuonyesha yeye ni Tanzania One wa ukweli.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: UGANDA ONE ATUA LEO DAR KUMALIZANA NA SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top