![]() |
Wachezaji wenzake wakisikitika |
![]() |
Morosini akiwa amebebwa kwenye machela |
MECHI za mwishoni mwa wiki
nchini Italia zimefutwa Jumamosi, kufuatia kifo cha kiungo wa klabu ya Livorno,
Piermario Morosini uwanjani.
Mchezaji huyo mwenye umri wa
miaka 25 aliyekuwa akicheza kwa mkopo kutoka klabu ya Serie A, Udinese, alizimia
wakati wa mechi ya Ligi Daraja la Pili huko Pescara na baadaye ikatangazwa
amefia hospitali.
Huo ni mfululizo wa majanga
kihistoria katika familia yao, kwani hata wazazi wake Morosini walifariki
wakati akiwa mdogo, wakati kaka yake pia aliuawa.
Alikuwa anaishi na dada yake tu.
Kifo cha Morosini kinakuja ndani
ya mwezi mmoja, baada ya kiungo wa Bolton Wanderers ya England, Fabrice Muamba apatwe
matatizo ya moyo na kuzimia uwanjani katika Robo Fainali ya Kombe la FA na Tottenham,
ingawa amenusurika baada ya kutibiwa.
Meneja Mkuu wa Shirikisho la
Soka Italia, Antonello Valentini alichukua hatua kufuatia tukio hilo kwa
kusimamisha mechi zote za wikiendi hii jana, kuanzia mechi ya Serie A kati ya
AC Milan na Genoa.
Mechi hiyo ilitarajiwa kuanza
saa 3:00 usiku na tayari mashabiki walikuwa wamekwishaingia kwenye Uwanja wa
San Siro, ingawa tangazo hilo lilizomewa na watu wengine.
Rais wa Kamati ya Olimpiki ya Italia,
Giovanni Petrucci baadaye alifanya kikao na bodi zote za michezo nchini humo
kuagiza kutoa dakika kadhaa za kuomboleza kifo cha Morosini.
Morosini alipatwa na mshituko wa
moyo katika kipindi cha kwanza cha mechi hiyo kabla ya kuzimia na pamoja na
kupatiwa huduma ya kwanza uwanjani, ilibidi achukuliwe na gari la wagonjwa
kukimbizwa hospitali ya Civile Santo Spirito, Pescara kwa matibabu zaidi.
Lakini mchezaji huyo wa zamani
wa timu ya taifa ya Italia chini ya umri wa miaka 21, baadaye ilitangazwa
amefariki dunia.
Lakini Polisi wameshushiwa
lawama kwa kifo cha mchezaji huyo kutokana na kuchelewa kuifungulia milango
gari ya wagonjwa wakati inaondoka baada ya kumchukua kumuwahisha hospitali.
Mamlaka za Italia zimeanzisha
uchunguzi juu ya tukio hilo, lakini wataalamu wa moyo wamesema ucheleweshaji
haujasababisha tofauti.
"Dakika moja mbele au nyuma
ndani ya ambulance isingeweza kufanya kitu chochote," alisema Daktari
mtaalamu wa moyo, Dk Paloscia.
"Moyo wake ulisimama na mapigo
yasingeweza kufanya kazi tena. Tulijaribu kuokoa maisha yake kwa saa nzima na
nusu, lakini ilishindikana."
Vyombo vya habari Italia
vilishitukia kifo cha Morosini mara baada ya kuanza kusikia vilio kutoka kwa
wachezaji wenzake waliokuwa hospitali.
Polisi walianza kuwatawanya
Waandishi wa Habari, lakini taarifa rasmi ilifuatia baadaye.
Rais wa FIFA, Sepp Blatter ni
miongoni mwa wanaotarajiwa kuhudhuria mazishi ya Morosini.
Muamba alizimia Machi 17, mwaka
huu na akazua hofu kwamba angeingia kwenye orodha ya wanasoka waliofia
uwanjani, mtu anayekumbukwa zaidi akiwa ni Marc-Vivien Foe.
Akiwa ana umri wa miaka 28,
kiungo huyo wa zamani wa Cameroon aliyezichezea klabu za West Ham United,
Manchester City na Lyon, alifariki dunia baada ya kuanguka na kuzimia katika
mechi ya Kombe la Mabara Nusu Fainali, dhidi ya Colombia mjini Lyon, Ufaransa
Juni mwaka 2003.
0 comments:
Post a Comment