Na Princess Asia
KAMPUNI ya Airtel Tanzania kupitia mpango wake maalum wa kuvumbua
na kukuza vipaji vya soka nchini ujulikanao kama Airtel Rising Stars leo
wametangaza kikosi cha wachezaji 16 watakaoiwakilisha Tanzania kwenye
mashindano ya kimataifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Airtel
yatakayofanyika Nairobi kuanzia Agosti 19 hadi 25, mwaka huu.
Wachezaji hao walichaguliwa na jopo la makocha kwa
kushirikiana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Chama cha Soka Dar es Saalam
(DRFA), wakati wa fainali za Taifa za Airtel Rising Stars zilizofanyika kwenye
Uwanja wa Karume, Dar es Salaam Juni na
kushirikisha timu kutoka mikoa ya Lindi, Mbeya, Arusha,
Ilala, Temeke na Kinondoni.
Akizungumza na Waandishi wa Habari katika ofisi za TFF jana,
Ofisa Maendeleo wa Soka wa TFF, Salum Madadi aliwataja vijana watakaowakilisha
Tanzania kuwa ni Denis Richard, Juma Hamza, Abdul Selemani, Ishaka Shekolowa na
Bakari Ally kutoka mkoa wa kisoka wa Temeke.
Wengine ni Abdulatif Mohamed, George Joseph na Badilu Said
(Lindi), Said Kassim, Amos Ikungula, Paul Balama na Goodluck Mabiku (Ilala), Joel
Kasimula na Ibrahim Mtenga (Mbeya), Sntkony Angelo na Suleiman Yunus (Arusha).
Mashindano hayo yanayotarajiwa kuwa na ushindani mkali
yatashirikisha wachezaji wengine nyota wa ARS kutoka nchi za Kenya, Uganda,
Malawi, DRC, Congo Brazzaville, Nigeria, Ghana, Zambia, Niger, Gabon, Burkina Fasso,
Sierra Leone, Chad, Madagascar na Tanzania.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel Tanzania, Beatrice
Singano Mallya, amesema kuwa lengo la mashindano hayo ya kimataifa ni kuwapa
vijana fursa zaidi ya kuendeleza vipaji vyao na kupata uzoefu. “Vile vile Airtel
Rising Stars inatoa nafasi kwa wanasoka hawa chipukizi kuweza kupanua jiografia
yao na kujenga urafiki na vijana wenzao kutoka nchi
mbali mbali”, alisema Singano.
Michuano hiyo itafuatiwa na kliniki ya soka ya kimataifa
ambayo pia itafanyika Nairobi chini ya walimu wa soka la vijana kutoka klabu maarufu
duniani ya Manchester United ya Uingereza. Kliniki kama hii ilifanyika mwaka
jana kwenye uwanja wa kisasa wa soka jijini Dar es Salaam na kushirikisha
vijana kutoka Kenya, Malawi, Sierra Leone na wenyeji Tanzania.
Katika kliniki ya mwaka huu, Tanzania itawakilishwa na
wachezaji sita miongoni mwao ni wavulana watatu na wasichana watatu ambao
walioibuka kuwa wachezaji bora wakati wa fainali za Taifa jijini Dar es Salaam mwezi
Juni.
Airtel Rising Stars ni mpango kabambe wa kuibua na kukuza
vipaji vya wanasoka wanaochipukia barani Afrika. Walengwa ni wavulana na wasichana
wenye umri chini ya miaka kumi na saba ambao watapata fursa ya pekee ya
kuonyesha vipaji vyao mbele ya waatalum wa mpira wa miguu wa kitaifa na
kimataifa.
0 comments:
Post a Comment