Mwenyekiti wa Azam FC, Mzee Said Mohamed Said (kushoto) akimtambulisha kwa Waandishi wa Habari, kocha Bunjak leo |
Na Mahmoud Zubeiry
AZAM FC, washindi wa Medali tatu za Fedha, Ligi Kuu msimu
uliopita, Kombe la Urafiki na Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la
Kagame, leo wamemtambulisha kocha wao mpya kutoka Serbia, Boris Bunjak ambaye
atarithi mikoba ya Muingereza Stewart Hall aliyefukuzwa wiki iliyopita.
Mwenyekiti wa Azam FC, amewaambia Waandishi wa Habari leo
mchana kwamba, wameingia mkataba wa miaka miwili na Bunjak, ambaye anatua katika
klabu hiyo kwa msaada wa kocha wa Simba, Milovan Cirkock ambaye alimuunganisha
na wamiliki wa klabu hiyo.
Bunjak mwenye leseni ya Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA), anatua
Azam, akitokea FC Damac ya Saudia Arabia aliyoanza kuifundisha mwaka jana na
kabla ya hapo alifunisha klabu za kibao, zikiwemo FK Sloga Kraljevo, FK Javor
Ivanjica, Crvena Zvezda Gnjilane, FK Radnicki Nis, FC Uralan Elista, FK Mladi
Radnik, FK Crvena Zvezda Beograd, Al-Shaab, FK Hajduk Kula na Al-Nasr.
Awali, Bunjak aliyezaliwa Novemba 17, mwaka 1954 ( miaka 57),
alicheza soka katika klabu za FK Sloga (Kraljevo), FK Vozdovac (Beograd), FK Radnicki
(Kragujevac), FK Olimpia (Ljubljana), FK Sumadija (Arandjelovac), FK Sloga (Kraljevo),
FK Borac (Cacak) na FK Sloga (Kraljevo).
Kwa kuajiriwa kocha huyo, Vivek Nagul kutoka India,
aliyekuwa anakaimu nafasi ya Stewart, ambaye aliletwa na Muingereza huyo
anarejea kwenye majukumu ya kufundisha timu za vijana, wakati Kocha Msaidizi
ataendelea kuwa Kali Ongala.
Stewart kabla ya kuja Tanzania mwaka juzi, akianza
kufundisha timu ya taifa ya Zanzibar, aliwahi kufanya kazi India kwa miaka
miwili.
Akiwa India ndipo alikutana na Vivek na wakafanya naye kazi
pamoja na akaridhishwa na utendaji wake, hasa katika eneo la vijana na ndio
maana alipotua Azam FC akamleta aje kumsaidia katika eneo hilo.
Vivek amekuwa Kocha Mkuu wa Azam Academy tangu mwaka jana,
akisaidiwa na Iddi Cheche na Philipo Alando.
Stewart alifukuzwa Jumatano iliyopita kwa kosa la kukaidi
maagizo ya Bodi ya Ukurugenzi ya klabu hiyo, kumpanga Mrisho Khalfan Ngassa
katika mechi ya fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la
Kagame dhidi ya Yanga.
Kikao cha Jumatano hiyo pamoja baina ya Bodi ya Ukurugenzi
ya Azam FC, Mwanasheria wa kampuni na kocha Stewart kiliafiki kuvunjwa kwa ndoa
hiyo na Azam FC ikawa chini ya Nagul, akisaidiwa na Kali Ongala.
Baada ya mechi ya Nusu Fainali ya Kagame, kati ya Azam na AS
Vita ya DRC, Stewart aliitwa na kuambiwa asimtumie tena Ngassa kwa kitendo cha
mchezaji huyo kwenda kuibusu na kuivaa jezi ya Yanga, baada ya kufunga bao la
ushindi. Ngassa ameuzwa Simba SC, baada ya sakata hilo.
Lakini Stewart katika kikao hicho, kwanza alimtetea Ngassa
kutokana na kufunga bao la ushindi na kumuelezea kama mchezaji muhimu kwake,
lakini msimamo wa bodi ulikuwa ni asipangwe tena.
Katika fainali, Stewart alimvalisha jezi Ngassa
akamuanzishia benchi, lakini kama ilivyokuwa kwenye Nusu Fainali alimuingiza
kipindi cha pili timu ikiwa nyuma kwa 1-0 na mwisho wa mchezo ikashinda 2-1
yeye akifunga la pili, dhidi ya Yanga pia alimuingiza timu ikiwa nyuma kwa 1-0.
Lakini Ngassa alishindwa kurudia kile alichofanya kwenye
mechi na AS Vita na Yanga ikashinda 2-0.
Mserbia huyo anakuwa kocha wa tano Azam, ndani ya miaka
minne tangu ianze kucheza Ligi Kuu, 2008 baada ya Stewart, Mbrazil Neider dos
Santos, Sylvester Marsh na Itamar Amorin, Mbrazil mwingine.
Lakini ni Stewart angalau anaacha kumbukumbu ya taji na
Medali Azam, baada ya kuiwezesha kutwaa Kombe la Mapinduzi Januari, kushika
nafasi ya pili katika Ligi Kuu Aprili, kabla ya kushika nafasi ya pili Kombe la
Urafiki na Kagame mwezi uliopita.
Stewart ana sifa ya kutokuwa mbinafsi na mwenye kuwaamini
watu wa chini yake, kwa mfano namna ambavyo amekuwa akimpromoti Kali Ongala.
Alimkuta Kali kama mchezaji, lakini kwa sababu ya umri kumtupa mkono,
akashauriana naye awe Kocha Msaidizi na mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga,
akakubali.
Chini ya Stewart, Kali alikuwa akiachiwa timu aiongoze ili
kumjengea kujiamini zaidi na mwezi uliopita aliachiwa timu kwenye Kombe la
Urafiki, akaifikisha fainali, ambako ilifungwa na Simba kwa penalti kufuatia
sare ya 2-2 ndani ya dakika 90.
Wachezaji wa Azam na makocha wapya wa klabu hiyo, pamoja na
baadhi ya maofisa wa klabu hiyo, waliangua vilio, wakati wakimuaga Stewart.
Wachezaji walioongoza kwa kilio Uwanja wa Chamazi Ijumaa
iliyopita, ni Luckson Kakolaki, Ibrahim Mwaipopo, Ramadhan Chombo ‘Redondo’,
Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Hajji Nuhu na Erasto Nyoni, wakati kwa maofisa,
aliyeongoza ni Vivek Nagul.
Stewart mwenyewe pia alibubujikwa machozi wakati anaagana na
familia yake, aliyoishi nayo kwa zaidi ya mwaka kwa furaha, amani, upendo na
mafanikio.
WASIFU WA BORIS
BUNJAK:
JINA KAMILI: Boris Bunjak
KUZALIWA: Novemba 17, 1954 (Miaka 57)
KLABU ALIZOCHEZEA:
1967- 1975: FK Sloga (Kraljevo)
1975- 1978 FK Vozdovac
(Beograd)
1978- 1979 FK Radnicki (Kragujevac)
1979- 1980 FK Olimpia
(Ljubljana)
1980- 1981 FK Sumadija (Arandjelovac)
1981- 1985 FK Sloga (Kraljevo)
1985- 1986 FK Borac (Cacak)
1986- 1990 FK Sloga (Kraljevo)
KLABU ALIZOFUNDISHA:
1990-1993: FK Sloga (Kraljevo)
1995-1996: FK Javor (Ivanjica)
1996-1997: Crvena
Zvezda (Gnjilane)
1999: FK Radnicki (Nis)
2000: FC Uralan Elista (Urusi)
2000-2002: FK Mladi (Radnik)
2002-2004: FK Crvena
Zvezda (Beograd)
2004: Al-Shaab (UAE)
2005: FK Hajduk (Kula)
2006-2007: Al-Nasr (Oman)
2009: Al Oruba Sur (Oman)
2011: FC Damac
(Saudi
Arabia)
2011: AL
NASER (Oman)
0 comments:
Post a Comment