• HABARI MPYA

    Friday, August 10, 2012

    MAJERUHI MWINGINE YANGA

    Nurdin Bakari
    Na Prince Akbar
    MIKOSI imeendelea kumuandama kiungo wa Yanga, Nurdin Hamadi Bakari baada ya kuumia tena, hivyo kuendelea kuwa nje ya Uwanja.
    Nurdin hajagusa mpira tangu aumie akiwa kwenye kambi ya timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars miezi mitatu iliyopita na ameshindwa kuichezea Yanga kwenye Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame mwezi uliopita.
    Kocha wa Yanga, Mbelgiji Tom Saintfiet aliiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba, ‘wadi’ yake ya majeruhi imepata mgeni mwingine, ambaye ni Nurdin, anayeungana na Juma Abdul.
    Yanga inaendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Loyola, Mabibo, Dar es Salaam kujiandaa na Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ikitoka kutwaa Kombe la Kagame.
    Yanga ilitwaa Kombe la Kagame kwa mara ya pili mfululizo wiki mbili zilizopita, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa kuifunga Azam FC mabao 2-0, ambayo yalitiwa kimiani na Hamisi Kiiza ‘Diego Milito’ na Said Bahanuzi ‘Spider Man’.
    Hiyo kwa ujumla ilikuwa mara ya tano mfululizo, Yanga inatwaa Kombe hilo, baada ya awali kuchukua mwaka jana, wakiifunga Simba katika fainali bao 1-0, Uwanja wa Taifa mfungaji Kenneth Asamoah ambaye ametemwa, ingawa siku hiyo Kiiza pia alifunga bao safi, ambalo refa alilikataa.
    Yanga ilichukua kwa mara ya kwanza Kombe hilo, mwaka 1975 ikiifunga tena Simba katika fainali, mabao 2-0 wafungaji Sunday Manara ‘Computer’ na Gibson Sembuli (sasa marehemu) Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
    Ikachukua tena mwaka 1993, Uwanja wa Nakivubo, Kampala, Uganda kwa kuifunga SC Villa mabao 2-1, yaliyotiwa kimiani na Said Nassor Mwamba ‘Kizota’ (sasa marehemu) na Edibily Jonas Lunyamila.
    Ilichukua tena mwaka 1999, ikiifunga tena SC Villa, Uwanja wa Nakivubo, kwa penalti 5-3, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 120, Yanga ikisawazisha bao kupitia kwa Lunyamila, baada ya Hassan Mubiru kutangulia kuifungia Villa, siku hiyo Manyika Peter akicheza penalti mbili za Waganda.   
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAJERUHI MWINGINE YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top