Na
Princess Asia
KOCHA wa Mtibwa Sugar
ya Morogoro, Mecky Mexime ameshauri vyombo vya habari nchini viache kushobokea
wachezaji wa kigeni, badala yake visaidie kupromoti wachezaji wa nyumbani,
ambao anaamini wana uwezo mkubwa kuliko hata hao wageni.
Akizungumza mjini Dar
es Salaam jana, Nahodha huyo wa zamani wa timu ya taifa, Taifa Stars, alisema
kwamba hapendi kuona wachezaji wa kigeni wanashobokewa kupita kiasi wakati
Tanzania kuna wachezaji wazuri.
“Tumeona vijana wadogo
wa Simba wakicheza soka nzuri na kuifunga Azam iliyokuwa na wachezaji wa kigeni
na kocha wa kigeni pia. Lakini pia mfano mwingine ni sisi Mtibwa, tunatumia
wachezaji wa kigeni na kila mwaka Simba na Yanga zinakuja kwetu kuchukua
wachezaji kule,”alisema beki huyo wa zamani hodari nchini.
Mexime alimtolea mfano
mshambuliaji Said Bahanuzi, akisema kwamba kijana huyo ametokea Mtibwa kwenda
Yanga ambako moja kwa moja ameibuka mfungaji bora wa Klabu Bingwa Afrika
Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
Maxime juzi
aliiwezesha Mtibwa Sugar kutinga Fainali ya michuano ya BankABC Sup8R kwa kishindo,
baada ya kuinyuka Jamhuri ya Pemba, mabao 5-1, ambayo yalitiwa kimiani na Babu
Ally Seif dakika ya 15, Salvartoy Ntebe dakika ya 17, Mfaume Shaaban
aliyejifunga dakika ya 38, Vincent Barnabas dakika ya 43 na Awadh Juma dakika
ya 85 wakati la kufutia machozi la Jamhuri lilifungwa na Mbarouk Chande dakika
ya 62.
Mtibwa ambayo itacheza na Simba SC kwenye fainali kesho, ndio
timu pekee ambayo haijapoteza pointi hata moja kwenye mashindano hayo baada ya
kushinda mechi zake zote tatu za Kundi B, 2-1 dhidi ya Polisi Moro, 2-0 dhidi
ya Azam na 5-0 dhidi ya Super Falcon na jana 5-1 dhidi ya Jamhuri katika Nusu
Fainali.
Simba B yenyewe ilitoa sare moja tu ya kufungana 1-1 na
Jamhuri katika mchezo wa kwanza, lakini mechi zake nyingine ilizifunga 2-0 kila
timu, Mtende na Zimamoto ya Zanzibar.
0 comments:
Post a Comment