• HABARI MPYA

    Wednesday, August 08, 2012

    UBISHI NA UJUAJI WA WAKUBWA TFF, FAIDA ZAKE NDIO HIZI...


    WIKI iliyopita, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilitangaza mashindano mapya ya Bank ABC Sup8r, ambayo yalianza Agosti 5, mwaka huu na yanatarajiwa kufikia tamati Agosti 189, mwaka huu yakishirikisha timu nane, nne za Zanzibar na nne za Bara.
    Na Mahmoud Zubeiry
    Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema kwamba timu tatu zilizoshika nafasi za juu katika Ligi Kuu zote mbili zitaingia moja kwa moja, wakati timu moja kila upande iliyoongoza katika kampeni ya kupanda Ligi Kuu, zitashirikishwa pia.
    Alisema timu hizo zitakuwa katika makundi mawili na hakutakuwa na mechi ya kusaka mshindi wa tatu zaidi ya kuwepo kwa zawadi kwa timu itakayotwaa ubingwa tu na tayari wameshaziandikia barua za kuzitaarifu kuhusiana na michuano hiyo.
    “Nadhani hii ni nafasi nyingine kwa timu kuonyesha ushindani katika michuano hii, pia pamoja na kujiandaa kwa msimu mpya wa ligi, makocha wa timu shiriki wataweza kujua kiwango kilichopo kwenye timu zao na kama kuna kasoro warekebishe kabla ya kuanza kwa ligi,”alisema.
    Bank ABC ambayo imedhamini michuano hiyo kwa miaka mitatu, kupitia kwa Mkurugenzi wake Mkuu Boni Nyoni alisema wameamua kuandaa michuano hiyo ili kuunga mkono jitihada za maendeleo ya soka hapa nchini.
    Niliwapongeza TFF kwa kufanikiwa kupata mwekezaji wa kudhamini mashindano haya, nikiamini wachezaji wetu kutokuwa fiti kwa angalau asilimia 70, kunatokana na kukosa mechi za kutosha za ushindani, kwani wengi wao zaidi ya Ligi Kuu hawana sehemu nyingine ya kuongeza uzoefu wao kiuchezaji.
    Kwa hivyo ujio wa mashindano kama haya, ambayo nilitarajia yangepata maandalizi mazuri, yangekuwa ya ushindani, hivyo lingekuwa jambo la kufurahia na kwa hivyo niliona ni vema kuwapongeza TFF na kuwaomba watanue zaidi wigo wa kutafuta wadhamini kwa ajili ya mashindano mengine muhimu.
    Muda mrefu sijamuona Mkurugenzi wa Masoko wa TFF, Jimmy Kabwe akijitokeza kifua mbele, kwa sababu vyombo vya habari vimekuwa vikimnyooshea sana vidole juu ya utendaji wake, kiasi cha kutilia shaka uwezo wake na uzoefu katika jukumu alilopewa.
    Zaidi ya kumuona katika utiaji saini wa mkataba wa udhamini wa timu ya taifa, Taifa Stars na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), ndio nilimuona tena nyota huyo wa filamu ya Secret katika kutangazwa kwa Sup8r ya Bank ABC.
    Nampongeza Jimmy na sasa aelewe, kama atatekeleza wajibu wake vizuri, baadala ya kukaa mezani na kuchati kwenye tweetter na facebook, kila mmoja atakuwa rafiki yake, kwani shida yetu ni kuona ufanisi katika soka yetu na kila mmoja anatekeleza wajibu wake mzuri.
    Kwa sasa tunaona kabisa shirikisho linakabiliwa na mzigo mzito- mashindano ya Kombe la FA hayapo, yanataka kurudi ha hayana udhamini hadi sasa, tunahitaji kuwa na Ligi madhubuti ya timu za vijana za klabu za Ligi Kuu, lakini bila udhamini haiwezekani.
    Timu zetu zote za taifa hazina udhamini, ukiondoa ule wa timu ya wakubwa. Bado soka haitumiki ipasavyo hapa nchini katika kampeni za kibiashara kama ilivyo nchi za wenzetu- tunataka kuona wachezaji wa timu ya taifa wanaingia mikataba mikubwa ya madau makubwa ya matangazo ya biashara. Kwa kweli Jimmy anatakiwa kujua, ana kazi kubwa bado ya kufanya ili kutimiza wajibu wake vema.
    Lakini pamoja na ukweli kwamba ujio wa michuano hii ni habari njema kwa soka ya Tanzania, kuna mambo niliyaona mapema na nikatoa angalizo, kwamba muda ambao TFF wanataka kuendesha mashindano haya, si mwafaka.
    Yalikuja wiki moja tu baada ya kumalizika kwa michuano ya Klabu Bingwa ya soka Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame na Kocha wa Yanga, Tom Saintfiet raia wa Ubelgiji alikuwa wa kwanza kuonyesha hayuko tayari kuingiza timu yake kwenye michuano hiyo kwa sababu anaamini itawaumiza wachezaji wake.
    Alisema kwamba baada ya mashindano ya Kagame, klabu yake ikitetea taji, ni vema wachezaji wakapewa muda wa kupumzika, badala ya kupewa adhabu nyingine.
    Simba na Azam wameshiriki, wakitumia wachezaji wa timu zao za vijana kwa wingi na nafasi ya Yanga imechukuliwa na Mtibwa Sugar, ambao wana kiu ya mashindano, kwani baada ya kufulia kisoka, zaidi ya Ligi Kuu hawana mashindano mengine.
    Niliwashauri TFF, kutokana na ugumu wa mashindano haya kufanyika mwezi huu, hakuna haja ya kulazimisha, ili tuwe na mashindano bora, yenye msisimko na faida kwa pande zote mbili, soka yetu na mwekezaji, basi yasogezwe mbele.
    Timu tatu za Bara, Simba mabingwa, Azam washindi wa pili na Yanga wa tatu zimetoka kwenye Kombe la Kagame na wachezaji wao wengi wamechoka, wameumia kwenye mashindano hayo, kutokana na kuingia kwenye michuano hiyo wakiwa hawako fiti kimazoezi.
    Tenga amecheza mpira, atakuwa anajua. Hata Angetile huwa anasema alicheza na marehemu Saidi Mwamba Kizota huko Tabora, basi atakuwa anajua pia- lakini Sunday Kayuni ni mwalimu anajua nina hakika na kwa kuwa ninamjua ni mtu wa misimamo sijui ingekuwaje kama yeye ndiye angekuwa kocha wa Simba, halafu TFF inataka kumburuza namna hii.
    Ligi yetu inaanza mwishoni mwa mwezi huu na Novemba tutamaliza mzunguko wa kwanza- Desemba kutakuwa kuna Kombe la Challenge kabla ya kurejea kwa Ligi Kuu Januari na Februari klabu nne kati ya nane zinazotarajiwa kushiriki mashindano hayo zitaingia kwenye michuano ya Afrika.
    Nikawashauri TFF, waangalie kuanzia Desemba, wapi wayachomeke mashindano haya, ili yawe na maana halisi ya maandalizi ya msimu mpya. Maana japokuwa sisi ligi yetu inaanza Agosti, lakini utaona tunahitaji kuwekeza zaidi katika maandalizi ya mwishoni mwa mwaka, kwa sababu ndio tunaelekea kwenye mashindano makubwa, yakiwemo ya Afrika na lala salama ya Ligi Kuu.
    TFF wakapuuza na mashindano yakaanza na matokeo yake yamekosa msisimko unaostahili na mbaya zaidi, imefikia hadi timu zinazuiwa kuingia kwenye viwanja kucheza.
    Mechi zilipangwa kufanyika katika viwanja vinne, Taifa, Dar es Salaam, Amaan Zanzibar, Kirumba Mwanza na Sheikh Amri Abeid Arusha, lakini sasa si hivyo tena.
    Mtibwa Sugar na Polisi Morogoro walizuiliwa getini Uwanja wa Amri Abeid wakiwa wanataka kuingia kucheza, baada ya wamiliki wa Uwanja huo kusema hawana taarifa za mashindano hayo.
    Soka ya Tanzania iko katika mfumo mzuri sawa na serikali yetu na inatawalika, kwa sababu ina uongozi kuanzia ngazi ya Wilaya, Mkoa hadi Taifa sasa ajabu Mkoa wa Arusha hauna mawasiliano na TFF, tena kuhusu mashindano makubwa kama haya. Hii ni fedheha.
    Haya, Yanga ambayo ina mashabiki wengi, ambayo kama ingeshiriki mashindano yangekuwa na msisimko zaidi, haimo wakati Azam na Simba wameshirikisha vijana kwa wingi.
    TFF lazima watambue, kupata mdhamini si jambo jepesi na ndio maana wao wanasotea udhamini. Mashindano ya Kagame, mwaka huu yalimpoteza mdhamini wake mmoja Castle Lager na yakabebwa na Azam Cola. Banc ABC kama wawekezaji wengine wowote duniani, wanadhamini mashindano ili pamoja na kuchangia maendeleo, lakini na wao wanahitaji faida ili kutangaza biashara yao. Faida kubwa ya mdhamini ni mashindano kuwa na msisimko, ili afikishe ujumbe wake kwa jamii aliyoilenga.
    Lakini hadi sasa kulingana na mwenendo wa mashindano yenyewe, Banc ABC wana lipi la kuwashawishi na mwakani pia wachome zaidi ya Sh. Milioni 300 kudhamini mashindano haya? Tutafakari mara mbili. Ramadhan Mubarak.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: UBISHI NA UJUAJI WA WAKUBWA TFF, FAIDA ZAKE NDIO HIZI... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top