![]() |
| Kikosi cha Yanga |
YANGA SC, asubuhi ya leo kwenye Uwanja wa sekondari ya
Loyola, Mabibo, Dar es Salaam, inacheza mechi ya kujipima nguvu na timu yake ya
vijana chini ya umri wa miaka 20, iliyo chini ya kocha Salvatory Edward
aliyekuwa akiitwa Doctor enzi zake anacheza soka.
Kocha Mbelgiji, Tom Saintfiet anataka kuutumia mchezo huo
kuangalia hali ya kikosi chake, baada ya takriban wiki mbili za mazoezi tangu
wachezaji warejee kutoka likizo fupi, kufuatia kutwaa taji la Klabu Bingwa ya
soka Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
Tom aliiambia BIN ZUBEIRY kwamba nia yake ni
kuleta mataji zaidi katika klabu hiyo, likiwemo taji la ubingwa wa Afrika,
ambalo hakuna timu katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati, imewahi
kulitwaa.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY katika mahojiano maalum,
Mtakatifu Tom alisema kwamba akipewa muda na ushirikiano wa kutosha anaweza
kutimiza ndoto zake hizo.
“Mimi ni mshindi na nimekuja Yanga kushinda mataji, na
nitaleta mataji mengi zaidi na makubwa kuliko hili, nitaleta hadi Kombe la
Afrika,”alisema kocha huyo, ambaye kutokana na kazi yake nzuri alipokuwa
Ethiopia, alipachikwa jina Mtakatifu Tom.
Akiwa anaingia mwezi wa pili tangu aanze kazi Yanga, tayari
Tom amekwishaweka Kombe moja kwenye kabati la mataji la Yanga, ambalo ni la
Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
Yanga ilitwaa Kombe la Kagame kwa mara ya pili mfululizo
wiki mbili zilizopita, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa kuifunga Azam FC
mabao 2-0, ambayo yalitiwa kimiani na Hamisi Kiiza ‘Diego Milito’ na Said
Bahanuzi ‘Spider Man’.
Hiyo kwa ujumla ilikuwa mara ya tano mfululizo, Yanga
inatwaa Kombe hilo, baada ya awali kuchukua mwaka jana, wakiifunga Simba katika
fainali bao 1-0, Uwanja wa Taifa mfungaji Kenneth Asamoah ambaye ametemwa,
ingawa siku hiyo Kiiza pia alifunga bao safi, ambalo refa alilikataa.
Yanga ilichukua kwa mara ya kwanza Kombe hilo, mwaka 1975
ikiifunga tena Simba katika fainali, mabao 2-0 wafungaji Sunday Manara
‘Computer’ na Gibson Sembuli (sasa marehemu) Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Ikachukua tena mwaka 1993, Uwanja wa Nakivubo, Kampala,
Uganda kwa kuifunga SC Villa mabao 2-1, yaliyotiwa kimiani na Said Nassor
Mwamba ‘Kizota’ (sasa marehemu) na Edibily Jonas Lunyamila.
Ilichukua tena mwaka 1999, ikiifunga tena SC Villa, Uwanja
wa Nakivubo, kwa penalti 5-3, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 120, Yanga
ikisawazisha bao kupitia kwa Lunyamila, baada ya Hassan Mubiru kutangulia
kuifungia Villa, siku hiyo Manyika Peter akicheza penalti mbili za
Waganda.
Aidha, kwa kutwaa Kombe hilo chini ya Mbelgiji huyo, Yanga
imeendeleza rekodi yake ya kutwaa mataji ya michuano hiyo, chini ya makocha wa
kigeni baada ya mwaka 1975 kuchukua chini ya Tambwe Leya aliyekuwa raia wa
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kabla ya kuchukua uraia wa Tanzania,
(sasa marehemu), 1993 chini ya Nzoyisaba Tauzany aliyekuwa raia wa Burundi
kabla ya kuchukua uraia wa Tanzania, mwaka 1999 chini ya Raoul Shungu wa DRC na
mwaka jana chini ya Mganda, Sam Timbe.



.png)
0 comments:
Post a Comment