• HABARI MPYA

    Saturday, September 15, 2012

    AFRICAN LYON WATIMULIWA TAIFA NA JEZI NA MABANGO YAO YA ZANTEL, WATISHIA KUGOMEA MECHI NA SIMBA

    Ofisa Mkuu wa Biashara wa Zantel, Sajid Khan (kulia) akiwa na Mkurugenzi wa Michezo, Leonard Thadeo na Meneja Mkuu wa African Lyon, Rahim Kangezi ‘Zamunda’ wakati wa kutangaza dili la oleo mchana.


    Kutoka kushoto ni Kocha Muargentina wa African Lyon, Pablo Ignacio Velez, Ofisa Mkuu wa Biashara wa Zantel, Sajid Khan, Mkurugenzi wa Michezo, Leonard Thadeo na Meneja Mkuu wa African Lyon, Rahim Kangezi ‘Zamunda’.
    Na Mahmoud Zubeiry
    KLABU ya African Lyon imezuiwa kuweka mabango yake kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wala kuvaa jezi zenye nembo ya mdhamini wao, kampuni ya simu ya Zantel katika mchezo wa leo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Simba SC.
    Mida hii, BIN ZUBEIRY imeshuhudia kasheshe baina ya wafanyakazi wa Uwanja wa Taifa, dhidi ya viongozi wa African Lyon.
    Ikumbukwe leo mchana, Lyon imetangaza kuingia mkataba wa udhamini na Zantel wa miaka mitatu na inatarajiwa kuanza kuutumikia katika mchezo wa leo wa ufunguzi wa Ligi Kuu dhidi ya Simba, utakaonza saa 10:30 jioni.
    Meneja Mkuu wa Lyon, Rahim ‘Zamunda’ Kangezi amesema msimamo huo wa kuzuiwa kuvaa jezi za mdhamini wao na kuweka mabango utaendelea, basi wao hawatacheza mechi hiyo.
    “Katika maboresho ya mkataba wa udhaimini wa Ligi Kuu wa Vodacom, hili limekwishazungumzwa na limerekebishwa kwamba klabu zitaruhusiwa kuingia mkataba na kampuni nyingine za simu.
    Pia, leo katika kikao cha kabla ya mechi tulipeleka jezi hizi na zikapitishwa, sasa iweje tunaambiwa hatuwezi kuvaa, sisi hatukubali, kama hatuvai na hatuchezi,”alisema Zamunda.
    Alipoambiwa kuhusu kanuni zitawahukumu wasipocheza kwa kushushwa Daraja, Zamunda alisema hawagomei mechi, bali wanagoma kucheza kwa sababu ya kuzuiwa, hivyo haoni ni vipi kanuni hiyo itawahukumu, zaidi wao watapambana kupata haki yao na sana mechi hiyo itachezwa siku nyingine, ambayo TFF watakuwa tayari kuiruhusu Lyon kuvaa jezi za mdhamini wao.
    Mapema leo mchana, Ofisa Mkuu wa Biashara wa Zantel, Sajid Khan alitangaza kampuni yake kuingia mkataba wa miaka mitatu kuidhamini Lyon, mbele ya Mkurugenzi wa Michezo, Leonard Thadeo katika hoteli ya Hyatt Regency (zamani Kilimanjaro), Dar es Salaam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AFRICAN LYON WATIMULIWA TAIFA NA JEZI NA MABANGO YAO YA ZANTEL, WATISHIA KUGOMEA MECHI NA SIMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top