• HABARI MPYA

    Friday, September 14, 2012

    KIBOKO YA RAGE APEWA KAZI NYINGINE NZITO YANGA DHIDI YA SIMBA

    Bin Kleb

    Na Mahmoud Zubeiry
    ABDALLAH Ahmad Bin Kleb amekuwa ‘supa staa’ baada ya kumfanya vibaya Mwenyekiti wa Simba, tena Alhaj, Ismail Aden Rage, pia Mbunge na mwenye vyao vingine kibao, katika usajili wa Mbuyu Twite, beki kutoka APR, nani asiyejua hilo?
    Basi huyo kijana ndiye Yanga imempa Uenyekiti wa Kamati ya Mashindano, ambayo jukumu lake ni kubeba mataji kuanzia la Ligi Kuu, ambalo linashikiliwa na Simba SC.
    Habari za ndani kutoka Yanga, ambazo BIN ZUBEIRY imezipata zimesema kwamba Kamati mpya ya Mashindano bosi wake ni kiboko ya Rage. Bin Kleb ataondoka kesho asubuhi kwenda Mbeya, kusaka pointi tatu za awali za Ligi Kuu katika mechi dhidi ya Prisons ya Mbeya Jumamosi, wakati Rage anaanza African Lyon Jumamosi pia Dar es Salaam.
    Mtu mzima Rage, alilalamika hadi kutoa machozi mjini Dodoma, wakati akizungumzia sakata la Mbuyu Twite akidai eti kuna mtoto wa kigogo aliingilia kati na ndio maana mchezaji huyo akabadilisha uamuzi wake na kwenda Yanga.
    Rage alidai kumsaini kwanza Twite, huku akinywa kahawa mjini Kigali na akadai wakati anamsaini na kumpa dola za Kimarekani 30,000 Yanga wakapiga simu na mchezaji huyo akawajibu amekwishamalizana na watu wa Simba.
    Lakini baadaye Twite akaibuka akisaini Yanga na kurudisha fedha za Wekundu hao wa  Msimbazi. Kleb, ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, alimsuta Rage kwamba anajikosha kwa wanachama wa Simba kwa kupakazia kuna mtoto wa kigogo aliingilia usajili wa Mbuyu Twite.
    “Rage ni muongo, ile vita ilikuwa kati yangu mimi na yeye, nadhani yeye alikuja Kigali kupiga picha na yule mchezaji, baada ya kushindwa kufanya hivyo alipokuwa Dar es Salaam, maana yake alikuja haraka haraka akazungumza na kiongozi mmoja wa FERWAFA (Shirikisho la Soka Rwanda), akapiga picha na Twite akaondoka.
    Karudi Dar es Salaam kwenye Mkutano Mkuu anasema amemsajili Twite, baada ya mimi kuonyesha vielelezo vya kumsajili huyo mchezaji kama mikataba na picha akiwa anasaini na kukabidhiwa jezi, akaanza kusema kuna mtoto wa kigogo, huyo mzee vipi? Mbona anakuwa muongo namna hii. Yeye aseme kweli tu, hana uzoefu na mambo haya, yeye ni mtu wa kuropoka tu, hawezi kazi,”alisema Bin Kleb.
    Pamoja na hayo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeitaka Yanga kuirudishia Simba SC fedha ambazo beki wao Twite alipewa na Rage.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KIBOKO YA RAGE APEWA KAZI NYINGINE NZITO YANGA DHIDI YA SIMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top