• HABARI MPYA

    Friday, September 14, 2012

    LIGI INAANZA KESHO, KLABU, MAREFA HAWAJAPEWA NAULI WA JEZI

    Coastal Union, wanaanza na Mgambo kesho

    Na Mahmoud Zubeiry
    WAKATI Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2012/2013 inaanza kutimua vumbi kesho, timu zote 14 zikijitupa viwanja saba tofauti, kusaka pointi- hadi unaposoma habari hii, klabu hazijapewa fedha zozote kutoka kwa wadhamini, hata za nauli na mbaya zaidi, hata vifaa vya michezo havijatolewa.
    Maana yake, timu ambayo itashindwa kufika kituoni kesho kwa kigezo cha kutokuwa na fedha ya nauli, itakuwa na haki na haitastahili adhabu yoyote, kwa sababu klabu nyingi zinazoshiriki ligi hiyo hazina vyanzo vya mapato Azam FC, Simba na Yanga zenye ‘kujiweza’.   
    Habari zaidi zinasema, hata marefa waliopangwa kuchezesha mechi za awali za ligi hiyo, hawajapewa nauli za kwenda vituoni wala fedha za kujikimu, jambo ambalo linakaribisha mazingira ya rushwa.
    Refa atafikaje kituoni? Akilini kiwachini mwake na akifika kwa hisani ya klabu atalaumiwa akilipa fadhila?
    Mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Simba wataikaribisha African Lyon kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, wakati washindi wa pili wa ligi hiyo, Azam FC watakuwa wageni wa Kagera Sugar, Uwanja wa Kaitaba, Bukoba na washindi wa tatu, Yanga watakuwa wageni wa Prisons Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
    Mjini Morogoro, Polisi Dodoma watakuwa wenyeji wa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri wakati jijini Tanga, Mgambo JKT ambayo imepanda daraja msimu huu itaumana na Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
    JKT Ruvu na Ruvu Shooting zitapambana kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam huku Azam ikiwatembelea Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Katiba.
    Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Toto Africans dhidi ya Oljoro JKT na mechi zote zitaanza saa 10.30 jioni.
    Viingilio katika mechi ya Simba na African Lyon vitakuwa sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya kijani na bluu, sh. 8,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 viti vya VIP C na B wakati VIP A itakuwa sh. 20,000. Viingilio kwa mechi nyingine vitakuwa sh. 3,000 na sh. 10,000.
    Kwa ujumla Ligi Kuu inaanza katika mazingira ya ubabaishaji wa hali ya juu- hali ambayo lazima iepukwe ili kuboresha soka yetu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: LIGI INAANZA KESHO, KLABU, MAREFA HAWAJAPEWA NAULI WA JEZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top