• HABARI MPYA

    Saturday, September 15, 2012

    KARIBU MSIMU MPYA LIGI KUU, ZITAKUWA MBIO ZA FARASI WATATU?

    Simba SC; Mabingwa watetezi

    Na Mahmoud Zubeiry
    HATIMAYE michuano mikubwa kabisa ya soka nchini, ijulikanayo kama Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inarejea tena kwa mara ya 49 tangu ilipoanzishwa mwaka 1965 kwa wigo finyu na hali dunia kabisa, ikishirikisha klabu za Dar es Salaam pekee. Aliyekuwa kocha wa timu ya taifa ya Tanganyika kutoka Yugoslavia, Milan Celebic, aliposhauri kuwapo kwa michuano ya kusaka klabu bingwa ya taifa, ili kujenga mazingira ya kupata wachezaji wazuri zaidi wa timu ya taifa.
    Alisema kama kutakuwa na ligi, ina maana wachezaji watakuwa wamepata mazoezi ya muda mrefu katika kujiandaa na ligi, hivyo kuwa rahisi kwake kama mwalimu wa taifa wakati huo kuona wachezaji walio fiti na kuwachukua kwenye timu ya taifa.
    FAT ilikubali ushauri huo na kuanzisha Klabu bingwa ya taifa, ambayo ilifanyika kwa mara ya kwanza mwaka 1965, ikishirikisha timu sita tu zilizoteuliwa ambazo ni TPC ya Moshi, Sunderland (sasa Simba SC), Yanga na Tumbaku ya Kurasini, Dar es Salaam, Coastal Union na Manchester United, zote za Tanga.
    Michuano hiyo ya kwanza ilifanyika katika viwanja vya Ilala (sasa Karume) na Manispaa wa Tanga, sasa Mkwakwani na tatizo kubwa lililojitokeza na viongozi wa klabu, wachezaji na hata viongozi wa FAT, ni kutozielewa vyema kanuni na sheria za mchezo, hata ikasababisha Yanga wakajitoa na ubingwa ukatolewa kwa Sunderland (Simba) walioweka historia ya kuwa mabingwa wa kwanza nchini.
    Lakini awali ya hapo, historia inasema kwamba ligi ilikuwa inachezwa Dar es Salaam pekee tangu mwaka 1929, ikishirikisha timu za Cosmopolitan, Battalion King's African Rifles (KAR), Gymkhana Club, Tanganyika Territorial Police, Tanganyika Railways, Government School na Government Services.
    Kwa muhtasari hivyo ndivyo ilivyoanzishwa Ligi Kuu ya nchi hii, ambayo ilianza kwa mfumo wa mtoano hadi 1982 ilipoanza kuchezwa kama Ligi Daraja la Kwanza na mwaka 1996 ikabadilishwa na kuwa Ligi Luu.
    Mwaka 1997 ilipata udhamini wa kwanza wa Safari Lager Beer hadi 2001 na tangu mwaka 2002 imekuwa ikidhaminiwa na Vodacom Tanzania. BIN ZUBEIRY inakuletea wasifu wa timu 14 zinazoshiriki ligi hiyo kwa muhtasari.

    AZAM FC:
    Ilipanda Ligi Kuu kwa mara ya kwanza mwaka 2008 na moja kwa moja kuwa moja ya timu za ushindani katika ligi hiyo, msimu uliopita ikiipiku Yanga na kushinda nafasi ya pili hivyo kujikatia tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.
    Linapokuja swali nani atatwaa ubingwa wa Ligi Kuu, timu zitakazotangulizwa, mbali na ‘wenye ligi yao’ Simba na Yanga, Azam itafuatia na hilo limetokana mwendelezo mzuri wa timu hiyo katika kutoa ushindani kwenye ligi hiyo.
    Mafanikio mengine makubwa kwa Azam msimu uliopita, mbali na kutwaa Medali ya Fedha katika Ligi Kuu, ni kutwaa Kombe la Mapinduzi na kushika nafasi ya pili katika Kombe la Urafiki na Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
    Azam FC
    Msimu huu itakuwa chini ya kocha Mserbia, Boris Bunjak aliyerithi mikoba ya Muingereza Stewart John Hall aliyefukuzwa baada ya Kombe la Kagame, Julai, mwaka huu. 

    KAGERA SUGAR:
    Hii ni timu imara na yenye sifa tatu za kipekee- inazalisha vipaji vingi ambavyo vinachukuliwa na timu kubwa, haijawahi kushuka daraja tangu ipande mwaka 2005 na ni timu pekee, inayohofiwa na “Top Three’ wote wa Ligi Kuu, Simba, Azam na Yanga, iwe kwa mechi za nyumbani au ugenini, Kagera Sugar ni wazuri.
    Mafanikio makubwa zaidi kwa Kagera Sugar yalikuja msimu wa 2006, ilipoweza kutwaa Kombe la Tusker, linaloshirikisha timu za Afrika Mashariki, ikiifunga Simba kwenye fainali mabao 2-1, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambao sasa umebadilishwa jina na kuwa Uhuru na wakati wote imekuwa na kocha mmoja anayefanya kazi chini ya makocha wakuu, winga wa zamani wa Simba, Mrage Kabange.
    Kagera Sugar
    Msimu uliopita Kabange alifanya kazi chini ya Mganda, Mayanja Jackson, lakini msimu huu atakuwa chini ya mshambuliaji bora wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Abdallah ‘King’ Kibadeni, babu mmoja mtaalamu sana na mwenye kuijua soka ya Tanzania kinagaubaga, lakini anatolewa dosari chache tu za kibinadamu.

    MTIBWA SUGAR:
    Ngumu kujua kuna tatizo Mtibwa Sugar hata imeondoka katika orodha ya timu za upinzani Ligi Kuu na kubaki washiriki wa kawaida tu, wanaocheza ili kutoshuka daraja. Inatoa wachezaji wazuri kila msimu ambao wanapapatikiwa na timu kubwa, lakini imeshindwa kabisa kurejesha makali yake iliyoingia nayo kwenye soka ya Tanzania.
    Hii ni timu pekee nje ya Simba na Yanga kuwahi kutetea ubingwa wa Ligi Kuu msimu wa 1999 na 2000, ambayo pia imewahi kuiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya Afrika, lakini kwa sasa imekuwa ya kufungwa hadi na Simba B kwenye fainali ya Kombe. Kuna nini pale Manungu?
    Mtibwa Sugar
    Pamoja na yote, Mtibwa inabakia kwenye orodha ya timu zenye heshima katika Ligi Kuu na kulingana na mabadiliko ya benchi la ufundi iliyofanya msimu huu, Nahodha wake wa zamani, Mecky Mexime akipewa Ukocha Mkuu- badala ya Mkenya Thom Olaba, kuna matarajio mapya.

    TOTO AFRICAN:
    Sifa kubwa ya Toto African katika Ligi Kuu ni kuitoa nishai Simba, ingawa msimu uliopita ‘waliwachenjia’ hadi baba zao, Yanga SC. Hawa ndio wakombozi wa soka ya Mwanza kwa sasa, ambao kwa muda mrefu ilikuwa inabebwa na Pamba FC ‘TP Lindanda’, iliyopotea kabisa katika ramani ya soka ya Tanzania.
    Kitu kimoja tu, Toto haijafikia makali ya Pamba na ina kazi kubwa ya kupambana kufikia heshima hiyo, jambo ambalo ukiitathmini kwa kina timu hiyo, unagundua inaweza iwapo itaamua, kwa maana ya kujipanga vizuri.
    Mwanza ni mkoa ambao una matajiri wengi ambao kama wangeamua kuwekeza kwenye timu hiyo, ingekuwa tishio, ila katika hilo, kikwazo kinatajwa kuwa ni ‘Uyanga wao’. Ndio, Uyanga- kwa sababu timu hiyo inamilikiwa na tawi la Yanga mkoani Mwanza, liliopo Mtaa wa Kishamapanda, ingawa Yanga yenyewe haina msaada wowote wa maana kwa timu hiyo.
    Toto African
    Msimu huu, Toto itaendelea kuwa chini ya kocha John Tegete ambaye msimu uliopita alipitia wakati mgumu sana akiwa na timu hiyo kutokana na matokeo mabaya, yaliyofanya iponee chupuchupu kushuka daraja.    

    POLISI MOROGORO:
    Tangu kupotea kwa zama za utawala wa Reli katika soka ya Morogoro, Polisi ilikuwa timu nyingine rasmi iliyorithi joho hilo, lakini bado imekosa msingi imara wa kuifanya iwe timu ya kudumu katika ligi hiyo.
    Polisi imerejea msimu huu katika ligi hiyo, baada ya kushuka misimu miwili iliyopita na ikiwa chini ya kocha mkongwe, John Simkoko ambaye aliipa Mtibwa Sugar ubingwa wa Ligi Kuu msimu wa 1999/2000 na yeye mwenyewe alitwaa ubingwa huo kama mchezaji mwaka 1975 akiwa na Mseto FC ya Morogoro.
    Kwa kuwa Simkoko ni mtaalamu wa kufundisha soka ya kitabuni, hapana shaka Polisi itakuwa kivutio katika ligi, haswa ikiongozwa na mfungaji bora wa zamani wa Ligi Kuu, Abdallah Juma inatarajiwa kabisa kutoa ushindani.


    JKT MGAMBO:
    Hii ni timu mpya kabisa katika historia ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ambayo inatarajiwa kuleta changamoto mpya katika ligi hiyo.
    Kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu, Tanga itakuwa na timu mbili tena katika Ligi Kuu tangu kutoweka enzi za Coastal Union na African Sports.
    Tofauti tu ni kwamba, safari hii timu moja inatoka nje ya mji, wilaya ya Muheza, Mgambo JKT na wengine, Coastal wapo barabara ya 13 Tanga mjini.
    Mgambo inafundishwa na kocha maarufu wa timu za Jeshi la Wananchi, Matata Steven aliyewahi kuinoa Transit Camp katika Ligi Kuu miaka minne iliyopita, Steven Matata.

    JKT OLJORO:
    Inaingia katika msimu wake wa pili kwenye Ligi Kuu tangu ipande, ikiibeba soka ya Arusha kwa sasa baada ya AFC, zamani Ndovu kufulia.
    Msimu uliopita Oljoro ilitisha kidogo baada ya kuanza vizuri mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, lakini mzunguko wa pili ikapoteza makali yake na kumaliza ligi kwa kusuasua.
    Ni kama wamejipanga upya hivi, na msimu huu ikiwa chini ya kocha mpya, kipa wa zamani wa Yanga na Tukuyu Stars ya Mbeya, Mbwana Makatta, Oljoro inatarajiwa kufanya vizuri.

    JKT RUVU:
    R.I.P. Jackson Lema, Meja wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) aliyeipandisha JKT Ruvu na kuunda timu imara, ambayo ilizaa timu nyingine ya Ligi Kuu, Ruvu Shooting, enzi zake JKT ilikuwa inatisha katika soka ya Tanzania.
    Lakini tangu kufariki kwa Meja Lema timu hizo zote za JKT zimepoteza makali yake- japokuwa zimeendelea kuzalisha wachezaji bora, wanaopapatikiwa na timu kubwa, mfano kiungo chipukizi Frank Domayo aliyesajiliwa Yanga msimu huu.
    JKT Ruvu
    Labda msimu huu, JKT inayofundishwa na mchezaji wa zamani wa Yanga, Charles Kilinda itabadilika na kuonyesha ushindani katika ligi hiyo.  


    RUVU SHOOTING:
    Msimu uliopita kidogo ilisisimua katika Ligi Kuu kutokana na kuonyesha soka safi na ushindani pia, ingawa iliishia kuchezea kubaki Ligi Kuu.
    Hii ni timu ambayo ilitoka ubavuni mwa JKT Ruvu enzi za Meja Jackson Lema, ambaye baada ya kuna wachezaji wengi, akaamua kuunda timu B, ambayo baadaye iliingia kwenye ligi na kuopanda hadi Ligi Kuu.
    Kwa sasa timu hii inafundishwa na Nahodha wa zamani wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa ambaye misimu mitatu iliyopita alishindwa kutekeleza majukumu yake vizuri jeshini kutokana na majukumu ya timu ya taifa ya wanawake, Twiga Stars.
    Ruvu Shooting
    Lakini Mkwasa amebwaga manyanga Twiga Stars, maana yake sasa anapata muda wa kutosha wa kuiandaa Ruvu Shooting na pia kuifanya iwe ya ushindani Ligi Kuu.

    AFRICAN LYON:
    Ni timu yenye historia ya kusimulika ingawa haijawahi kutwaa taji lolote, kutokana na hadi sasa kuwa imepitia mikononi mwa wamiliki watatu, wafanyabiashara wa soko la Mbagala, Mbunge Mohamed Dewji na sasa Rahim Kangezi ‘Zamunda’, ambaye inadaiwa anapewa sapoti na Seattle Sounders FC ya Marekani.
    Kwa mara ya kwanza, African Lyon itakuwa chini ya kocha wa kigeni, Muargentina Pablo Ignacio Velez, ambaye kihistoria anakuwa Mzungu wa pili tangu, Mreno Eduardo Arroja Almeida aliyeletwa na Mo Dewji mara timu hiyo ilipopanda tu Ligi Kuu mwaka 2009.
    African Lyon
    Msimu huu, Lyon imekuja na sera mpya ya kutumia vijana zaidi, na imefukuza wachezaji wengi wakongwe, ili kujenga msingi mpya. Zamunda ni mtu mwenye mipango mingi sana na kama ataendelea hivyo, iko siku Lyon itakuwa ‘habari nyingine’.

    COASTAL UNION:
    Siyo Coastal ile walioizoea wengi, tarajia Coastal mpya kabisa msimu huu, ikiwa inajivunia udhamini wa Nassor Bin Slum na Simba Cement, imewekeza mno kwa ajili ya msimu huu wa Ligi Kuu.
    Kwanza, Coastal imesajili mseto mzuri wa wachezaji, wakongwe na chipukizi, wakiwemo hata kutoka nje ya nchi.
    Na hata katika maandalizi, Coastal ilikuwa na maandalizi mazuri na itakumbukwa ilikwenda Kenya, Morogoro, Dar es Salaam na kumalizia na Zanzibar, ikicheza mechi zisizopungua 10 za kujipima nguvu.
    Coastal Union
    Ikiwa chini ya Kocha Mkuu, mshambuliaji wake wa zamani, Juma Mgunda, anayesaidiwa na Habib Kondo, beki wa zamani wa Pan African, Coastal inatarajiwa kuingilia kati anga za Azam, Simba na Yanga pale juu.

    PRISONS:
    Imerudi Ligi Kuu baada ya kupotea kwa misimu mitatu na kutokana na jinsi ilivyosota kurejea kwenye ligi hiyo, hapana shaka Prisons wamejipanga ili kutorudia makosa.
    Prisons ilikuwa tishio miaka ya 1990 hadi mwanzoni mwa Milenia mpya, lakini taratibu makali yake yalienda yakipungua na zaidi ilitokana na kila ilipozalisha wachezaji wazuri, walikuwa wakichukuliwa na timu kubwa.
    Hilo lilikuwa shamba zuri sana la mavuno ya wachezaji kwa Simba na Yanga enzi hizo na kama itarudi Ligi Kuu kwa mtazamo huo huo, dhahiri Prisons itarejesha hadhi yake haraka iwezekanavyo.
    Safari hii Prisons inarudi Ligi Kuu ikiwa chini ya kocha mzoefu, Jumanne Challe, kiungo wa zamani wa kimataifa Tanzania, ambaye msimu uliopita aliifundisha African Lyon.

    SIMBA SC:
    Hawa ni mabingwa watetezi wa ligi hiyo ambao wakati tunaingia kwenye msimu mpya wanajivunia kuanza kama walivyouanza msimu uliopita, kwa ushindi wa Ngao ya Jamii. Msimu uliopita mabao ya Haruna Moshi ‘Boban’ na Felix Sunzu yaliipa Simba ushindi wa 2-0 dhidi ya Yanga katika mechi ya Ngao na msimu huu tena, mabao ya Mghana Daniel Akuffo, Mganda Emanuel Okwi na mzalendo Mwinyi Kazimoto, yaliitoa Simba nyuma kwa 2-0 na kushinda 3-2 dhidi ya Azam Jumanne wiki hii, hivyo kutwaa Ngao.
    Hakuna shaka katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu, Simba SC ni miongoni mwa farasi wanaotarajiwa kuwa na kasi nzuri kwenye marathoni ta taji. Ikiwa inaendelea kuwa chini ya kocha wake Mserbia, Profesa Milovan Cirkovick, Simba iliyofanya usajili baab kubwa, inatarajiwa kutetea taji pamoja na upinzani unaotarajiwa kutoka kwa Yanga na Azam.
    Simba SC

    YANGA SC:
    Hawa ni mabingwa wa kihistoria wa Ligi Kuu, wakiwa wanaongoza kutwaa mara nyingi zaidi taji hilo, ambao msimu huu wanaonekana kabisa kujipanga vema, baada ya majanga ya msimu uliopita, yaliyowafanya wakose hata tiketi ya kucheza michuano ya Afrika.
    Yanga, inaingia katika msimu mpya kama ambavyo iliingia kwenye msimu uliopita, ikitoka kutwaa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, lakini tofauti tu msimu huu hadi sasa hakuna dalili za mgogoro.
    Ikumbukwe msimu uliopita, Yanga ilipitia katika mgogoro mkubwa, ambao hasara zake ni matokeo mabaya katika Ligi Kuu, ikiwemo kipigo kinachoingia kwenye historia cha mabao 5-0 kutoka wapinzani wa jadi, Simba SC.
    Lakini baada ya kupata safu mpya ya uongozi chini ya Mwenyekiti msomi na tajiri, Yussuf Manji, Yanga iliyoajiri pia kocha mpya, Mbelgiji, Tom Saintfiet ambaye anaonekana ni mwajibikaji mzuri, msimu huu inatarajiwa kufanya vizuri katika Ligi Kuu.
    Yanga SC

    MABINGWA WA JUMLA LIGI KUU:
    1965 : Sunderland (Dar es Salaam)
    1966 : Sunderland (Dar es Salaam)
    1967 : Cosmopolitans (Dar es Salaam)
    1968 : Yanga
    1969 : Yanga
    1970 : Yanga
    1971 : Yanga
    1972 : Yanga
    1973 : Simba
    1974 : Yanga
    1975 : Mseto SC (Morogoro)
    1976 : Simba
    1977 : Simba
    1978 : Simba
    1979 : Simba
    1980 : Simba
    1981 : Yanga
    1982 : Pan African
    1983 : Yanga
    1984 : Simba
    1985 : Yanga
    1986 : Tukuyu Stars (Mbeya)
    1987 : Yanga
    1988 : Coastal Union (Tanga)
    Nahodha wa Yanga, Nsajigwa Shadrack akiwa
    na Kombe la ubingwa wa Ligi Kuu 2011
    1989 : Yanga
    1990 : Simba 
    1991 : Yanga
    1992 : Yanga
    1993 : Yanga
    1994 : Simba
    1995 : Simba
    1996 : Yanga
    1997 : Yanga
    1998 : Yanga
    1999 : Mtibwa Sugar (Morogoro)
    2000 : Mtibwa Sugar (Morogoro) 
    2001 : Simba
    2002 : Yanga
    2003 : Simba
    2004 : Simba
    2005 : Yanga
    2006 : Yanga
    2007 : Simba (Ligi Ndogo)
    2008 : Yanga
    2009:  Yanga  
    2010: Simba SC
    2011: Yanga SC
    2012: Simba SC
    2013: ???????
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KARIBU MSIMU MPYA LIGI KUU, ZITAKUWA MBIO ZA FARASI WATATU? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top