![]() |
| Hamisi Kiiza ataiongoza Yanga dhidi ya Prisons leo Sokoine |
Na Mahmoud Zubeiry
LIGI Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara inaanza leo kwa timu zote 14 kujitupa kwenye viwanja saba
tofauti, kuwania pointi za kuanza vema msimu mpya.
Mabingwa
watetezi Simba wataikaribisha African Lyon kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam. Mjini Morogoro, Polisi Dodoma watakuwa wenyeji wa Mtibwa Sugar kwenye
Uwanja wa Jamhuri wakati jijini Tanga, Mgambo JKT ambayo imepanda daraja msimu
huu itaumana na Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
Tanzania
Prisons ambayo nayo imerejea VPL msimu huu itaialika Yanga kwenye Uwanja wa
Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya. JKT Ruvu na Ruvu Shooting zitapambana
kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam huku Azam ikiwatembelea
Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Katiba.
![]() |
| John Bocco 'Adebayor' ataiongoza Azam dhidi ya Kagera Kaitaba leo |
Uwanja wa
CCM Kirumba jijini Mwanza utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Toto Africans dhidi
ya Oljoro JKT. Mechi zote zitaanza saa 10.30 jioni.
Wakati msimu
huo unaanza leo, bado Simba, ambao ni mabingwa watetezi, Azam washindi wa pili
na Yanga washindi wa tatu zinapewa nafasi kubwa ya kuendelea kutawala kwenye
ligi hiyo- kwa kifupi Ligi Kuu itakuwa mbio za farasi watatu, wengine
wanatarajiwa kuwa wasindikizaji.
Kocha Mkuu
wa Azam FC, Mserbia Boris Bunjak amesema timu yake ipo tayari kwa Ligi Kuu,
lakini tu amehadharisha marefa wachezeshe kwa haki.
Bunjak
alikerwa mno na marefa waliochezesha mechi ya Ngao ya Jamii Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam juzi kwamba waliwabeba wapinzani wao Simba SC.
Mechi hiyo
ilichezeshwa na Martin Sanya, aliyeisaidiwa na Omar Kambangwa na Ephron Ndissa,
wakati refa wa akiba alikuwa Oden Mbaga na Kamisaa Omary Kasinde.
Bunjak
alisema kwamba marefa hao walionyesha mapungufu makubwa kwa kuwapendelea wazi
wazi Simba na hata wakafanikiwa kutoka nyuma kwa mabao 2-0 na kushinda 3-2.
“Nafikiri
tulicheza mechi nzuri, tukaongoza 2-0, baada ya hapo tukapoteza nafasi nzuri za
kufunga, lakini siamini kwa nini refa alitoa penalti dakika ya mwisho(kipindi
cha kwanza), kwa sababu ule mpira ulikuwa kwenye himaya ya wachezaji watatu
kutoka nyuma, unaweza kuonaje nani aliucheza kwa mkono.
Bao la pili,
pia ulikuwa msaada mkubwa, niliandaa timu yangu kucheza dhidi ya wachezaji 10,
siyo wachezaji zaidi, mimi si kocha nayeandaa timu kucheza dhidi ya wachezaji
wengi, naweza kufanya nini, tulicheza vizuri, tulipoteza nafasi, refa
alitunyima penalti mbili, asilimia 100, naweza kufanya nini, labda hii ni soka
ya Tanzania tu.
![]() |
| Mrisho Ngassa ataiongoza Simba dhidi ya African Lyon leo |
Nitafanya
nini, huu ni uzoefu wangu wa kwanza ofisini tena, lakini nimeshangazwa sana,
Simba ni timu kubwa, Simba ni timu nzuri, lakini leo Azam imecheza vizuri, Azam
ilistahili kushinda taji,”alisema.
Kocha huyo
alionyeshwa kuridhishwa na bao moja tu la Simba, la tatu ambalo alisita
kulizungumzia kabisa katika malalamiko yake.
Nayo Simba,
inayofundishwa na Mserbia Profesa Milovan Cirkovick, itashuka dimbani kumenyana
na Lyon, ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Azam FC na kutwaa
Ngao ya Jamii, kwa mara ya pili mfululizo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
Jumanne wiki hii.
Shujaa wa
Simba siku hiyo alikuwa ni kiungo Mwinyi Kazimoto aliyefunga bao la ushindi
dakika ya 78 kwa shuti kali la mbali baada ya kumchungulia kipa wa Azam, Deo
Munishi ‘Dida’ amekaaje.
Hadi
mapumziko, Azam walikuwa mbele kwa mabao 2-1, yaliyotiwa kimiani na John
Raphael Bocco ‘Adebayor’ na kipre Herman Tchetche, wakimtungua kipa namba moja
Tanzania, Juma Kaseja.
Bocco
alitangulia kufunga dakika ya tano ya mchezo huo, baada ya kupigiwa kona fupi
na Abdi Kassim ‘Babbi’, akatoa pasi kwa Abdulhalim Humud ambaye alimrudishia
mfungaji huyo akafumua shuti kali la chini likajaa nyavuni pembezoni mwa lango
kulia.
Bocco ambaye
aliendekea kuwa mwiba mchungu kwa safu ya ulinzi ya Simba SC, alimtoka Amir
Maftah upande wa kulia wa Uwanja na kuingia ndani kabla ya kutoa krosi fupi kwa
Kipre aliyemtungua Kaseja na kuipatia Azam bao la pili dakika ya 35.
Simba
ilipata bao lake la kwanza dakika ya kwanza ya muda wa nyongeza, baada ya
kutimu kwa dakika 45 za kipindi cha kwanza, mfungaji Daniel Akuffo kwa penalti,
baada ya Said Mourad kuunawa mpira kwenye eneo la hatari.
Kipindi cha
pili Simba walirudi na nguvu zaidi na kuamua kushambulia kwa mipira ya pembeni,
ikiwatumia Mrisho Ngassa na Emanuel Okwi ambao walikuwa wakibadilishana
reli.
Kwa staili
hiyo, haikushangaza Simba ilipotumia dakika 45 za mwisho kwa kufunga mabao
mawili yaliyowatoa nyuma kwa 2-1 na kuibuka kidedea kwa ushindi wa 3-2.
Emanuel Okwi
alimchambua kama karanga Erasto Nyoni na kuingia ndani kabisa akiwatoka mabeki
wengine wa Azam, kabla ya kuujaza mpira nyavuni kwa shuti kali na Kazimoto
akamaliza kazi dakika ya 78.
Kwa ujumla
katika mchezo huo, Azam ilitawala kipindi cha kwanza na ilikosa mabao mawili
zaidi ya wazi kupitia kwa Himid Mao na Kipre, lakini kipindi cha pili Simba
walitawala mchezo na kama wangekuwa makini, nao wangeweza kuvuna mabao
zaidi.
Kocha Mkuu
wa Yanga, Mbelgiji Tom Saintfiet amesema kwamba mechi dhidi ya Prisons itakuwa
ngumu kwa sababu anaamini wapinzani wao watakamia na watasaidiwa na kucheza
nyumbani.
Lakini pia,
Saintfiet alisema Prisons haina presha ya kufungwa na Yanga kwa sababu ni timu
kubwa, hivyo watacheza kwa utulivu, wakipata sare ni safi, wakifungwa hakuna
tatizo na wakishinda kwao itakuwa ‘sikukuu’.
Mtakatifu
Tom ametua Mbeya na wachezaji 22 kwa ajili ya mechi hiyo ambao ni makipa; Yaw
Berko, Ally Mustafa ‘Barthez’, mabeki Shadrack Nsajigwa, Juma abdul, Godfrey
Taita, Mbuyu Twite, Kevin Yondan, Nadir
Haroub ‘Cannavaro’, David Luhende, Oscar Joshua na Stefano Mwasyika, viungo ni
Athumani Iddi ‘Chuji’, Haruna Niyonzima, Frank Domayo, Rashid Gumbo, Nizar
khalfan, Shamte Ally na Simon Msuva na washambuliaji ni Jerry Tegete, Didier
Kavumbangu, Said Bahanuzi na Hamisi Kiiza.
Jumamosi
iliyopita Yanga ilicheza mechi ya mwisho ya kujipima nguvu kabla ya kuanza kwa
Ligi Kuu na kushinda mabao 4-0 dhidi ya Moro united, Mrundi Didier Kavumbangu
akifunga mawili, mengine beki Juma Abdul na kiungo Shamte Ally.
Saintfiet alitaka
mechi moja dhidi ya timu inayocheza kama wapinzani wao wa kwanza katika Ligi
Kuu, Prisons na pia katika Uwanja mbaya kama ambao atachezea mechi ya kwanza ya
ligi hiyo, Sokoine mjini Mbeya na ndiyo maana timu hiyo ilicheza na Moro United
Uwanja wa Shule ya Msingi Kijitonyama.
Hiyo ilikuwa mechi ya 11, Saintfiet anashinda
Yanga katika mechi 12 tangu ajiunge nayo miezi miwili iliyopita, mbali ya ziwe
za mazoezini dhidi ya Sinza Stars na Kijitonyama Stars.
Ndani ya mechi hizo kuna mechi sita za
Klabu Bingwa ya soka Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, ambalo
aliiwezesha Yanga kutwaa ubingwa wa tano wa michuano hiyo, ikipoteza mechi moja
tu ya kwanza dhidi ya Atletico ya Burundi, kwa kufungwa 2-0, mabao yote ya
Kavumbangu, ambaye baadaye ikamsajili.





.png)
0 comments:
Post a Comment