• HABARI MPYA

    Wednesday, September 19, 2012

    KLABU LIGI KUU ZATAKA KUKAA MEZA MOJA NA VODACOM

    Ofisa Mkuu wa Biashara wa Zantel, Sajid Khan akimkabidhi jezi, Mkurugenzi wa Michezo, Leonard Thadeo kwa niaba ya klabu ya African Lyon ya Dar es Salaam, katika hoteli ya Hyatt Regency (zamani Kilimanjaro), Dar es Salaam wakati wa kutangaza kuingia mkataba wa kudhamini klabu hiyo kwa miaka mitatu. Wanaomfuatia Thadeo ni Meneja Mkuu wa African Lyon, Rahim Kangezi ‘Zamunda’ na Charles Otieno, Mkurugenzi wa Ufundi wa African Lyon. Kulia kabisa ni mchezaji chipukizi wa Lyon, Jarufu Magesa, ambaye anapelekwa na klabu Marekani kusoma na Kocha Muargentina wa African Lyon, Pablo Ignacio Velez. 

    Na Prince Asia
    KLABU za Ligi Kuu ya Vodacom zimekubaliana kukutana na mdhamini (kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom) kuzungumzia kipengele cha mkataba wa ligi hiyo kinachozuia kampuni nyingine za mawasiliano kudhamini timu zinazocheza Ligi Kuu.
    Maazimio hayo yalifikiwa jana (Septemba 18 mwaka huu) katika kikao kati ya klabu hizo na Kamati ya Ligi kilichofanyika ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) chini ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo Wallace Karia.
    Wengine waliohudhuria kikao hicho ni Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah na Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura.
    Maazimio mengine ya kikao hicho ni TFF kuiandikia barua African Lyon ambayo itaipeleka kwa mdhamini wake (Zantel) ikielezea hatua hiyo ili kusimamisha udhamini huo wakati ikisubiri matokeo ya mazungumzo kati ya klabu hizo na mdhamini wa Ligi Kuu juu ya kipengele cha kuzuia washindani wa Vodacom.
    Katika mkutano huo, watendaji wawili wa Kamati ya Ligi ambayo iko katika kipindi cha mpito kuelekea kuundwa kwa Bodi ya Ligi walitambulishwa kwa klabu hizo. Watendaji hao ni Silas Mwakibinga ambaye ni Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) na Joel Balisidya ambaye ni Ofisa wa Ligi (LO).
    Hatua hiyo inafuatia African Lyon kuzuiwa kuweka mabango yake kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wala kuvaa jezi zenye nembo ya mdhamini wao, kampuni ya simu ya Zantel katika mchezo wa leo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Simba SC Jumamosi.
    Tukio hilo, lilikuja saa chache baada ya Ofisa Mkuu wa Biashara wa Zantel, Sajid Khan kutangaza kampuni yake kuingia mkataba wa miaka mitatu kuidhamini Lyon, mbele ya Mkurugenzi wa Michezo, Leonard Thadeo katika hoteli ya Hyatt Regency (zamani Kilimanjaro), Dar es Salaam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KLABU LIGI KUU ZATAKA KUKAA MEZA MOJA NA VODACOM Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top