• HABARI MPYA

    Tuesday, September 18, 2012

    MTAKATIFU TOM AMTEMA TEGETE KIKOSI CHA KUIVAA MTIBWA

    Wachezaji wa Yanga

    Na Mahmoud Zubeiry
    KOCHA Mkuu wa Yanga SC, Mbelgiji Tom Saintefiet amembeba Haruna Niyonzima ingawa ni mgonjwa katika kikosi chake cha wachezaji 18 wanaondoka leo saa 8:00 mchana kwa basi kwenda Morogoro, kwa mchezo wa kesho wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, dhidi ya wenyeji Mtibwa Sugar, kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro na amemuacha mshambuliaji Jerry Tegete.
    Wachezaji anaokwenda nao Moro leo ni makipa; Yaw Berko, Ally Mustafa ‘Barthez’, mabeki Shadrack Nsajigwa, Juma abdul, Godfrey Taita, Mbuyu Twite, Kevin Yondan,  Nadir Haroub ‘Cannavaro’, David Luhende, Oscar Joshua na Stefano Mwasyika.
    Aliwataja viungo ni Athumani Iddi ‘Chuji’, Haruna Niyonzima, Frank Domayo, Nizar khalfan, Shamte Ally na Simon Msuva, wakati washambuliaji ni Didier Kavumbangu, Said Bahanuzi na Hamisi Kiiza, wakati wanaobaki walikuwa ni kipa Said Mohamed, mabeki Ladislaus Mbogo, Job Ibrahim, viungo Rashid Gumbo, Juma Seif ‘Kijiko’, Salum Telela, Omega Seme, Nurdin Bakari, Idrisa Assega, Issa Ngao wa Yanga B anayekomazwa kikosi cha kwanza na mshambuliaji Tegete.
    Huo utakuwa mchezo wa pili kwa Yanga katika ligi hiyo, baada ya awali kulazimishwa sare ya bila kufungana na Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya Jumamosi.
    Saintfiet jana aliwaomba radhi mashabiki wa Yanga kwa sare ya Jumamosi kwenye Uwanja wa Sokoine na akawatupia lawama viongozi wa klabu hiyo, kwa maandalizi mabovu.
    Saintfiet alilalamikia kulala kwenye hoteli mbaya, yenye vitanda vichache na vidogo, vilivyosababisha watu wakalala mzungu wa nne, na chakula kibaya na kwa ujumla alisema hawakuwa vizuri kabla ya mechi hiyo.  Alisema yeye alilala kitanda kimoja na Louis Sendeu na Mbuyu Twite alibanana na Didier Kavumbangu na hoteli haikuwa na mabomba vyooni wala bafuni, hivyo kulazimika kuingia na ndoo na kuogea kata.
    Alisema pia hoteli hiyo ilikuwa katikati ya mji na karibu na stendi ya mabasi, kila alfajiri kelele nyingi na kwa ujumla timu iliingia uwanjani ikiwa haiku vizuri.
    “Mimi kwa mfano sijaoga siku mbili, kwa kweli tulikuwa katika mazingira magumu na wapinzani wetu walicheza soka ya kuudhi tangu mwanzo, kupoteza muda, na marefa hawakuchukua hatua, tulipoteza nafasi kupitia kwa Kiiza (Hamisi) na Msuva (Simon), siwezi kulaumu mchezaji wangu yeyote, lakini hiyo ndiyo hali halisi,”alisema Saintfiet.
    Baada ya mazoezi ya asubuhi kwenye Uwanja wa sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam na saa 8:00 mchana watasafiri kwa njia ya barabaraba kwenda Morogoro ambako wakifika watatafuta hoteli nzuri mapema.
    Alisema anajua hata Uwanja wa huko, Jamhuri si mzuri na mechi itakuwa ngumu kwa sababu Mtibwa Sugar nao walitoka sare ya bila kufungana na Polisi katika mchezo wao wa kwanza Jumamosi na anaiheshimu timu hiyo kama moja ya timu tano kubwa Tanzania, pamoja na Simba, Azam na Coastal Union.
    “Lakini pamoja na kwamba Simba wamependelewa kupangiwa ratiba ya kuanza kucheza nyumbani mechi tano mfululiuzo, nakuambia Mei mwaka 2013 Yanga ndio itavishwa taji la ubingwa wa Ligi Kuu, acha wafurahie sasa hivi, watalia mwisho,”alisema Mtakatifu Tom.

    REKODI YA SAINTFIET YANGA
    1.     Yanga Vs JKT Ruvu             (Kirafiki)              2-0
    2.     Yanga Vs Atletico (Burundi, Kagame)               0-2
    3.     Yanga Vs Waw Salam (Sudan, Kagame)           7-1
    4.     Yanga Vs APR (Rwanda, Kagame)                   2-0
    5.     Yanga Vs Mafunzo (Z’bar, Kagame)                 1-1 (5-3penalti)
    6.     Yanga Vs APR (Rwanda, Kagame)                   1-0
    7.     Yanga Vs Azam (Kagame)                                2-0
    8.     Yanga Vs African Lyon (Kirafiki)                      4-0
    9.     Yanga Vs Rayon (Kirafiki, Rwanda)                  2-0
    10.                        Yanga Vs Polisi (Kirafiiki, Rwanda)          2-1
    11.                        Yanga Vs Coastal Union    (Kirafiki)         2-1
    12.                        Yanga Vs Moro United      (Kirafiki)         4-0
    13.                        Yanga Vs Prisons    (Ligi Kuu)                  0-0 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MTAKATIFU TOM AMTEMA TEGETE KIKOSI CHA KUIVAA MTIBWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top