![]() |
Sunzu wa kwanza kushoto, katikati ni marehemu Patrick Mafisango na kulia ni Emmanuel Okwi |
Na Prince Akbar
SIMBA SC jana ilifanya mazoezi yake jioni kwenye Uwanja wa Kinesi, Manzese eneo la Urafiki, Dar es Salaam na Felix Sunzu alionyesha yeye ni mkali katika jitihada zake za kumshawishi kocha Milovan Cirkovick ampange kwenye mechi ya kesho, ingawa hilo linaonekana kuwa gumu.
Sunzu alijituma sana mazoezini jana- ingawa Daniel Akuffo na Abdallah Juma naop walifanya kazi nzuri ya kumvutia kocha Milo, ambaye kesho anatarajiwa kuiongoza Simba SC katika mchezo wa pili wa Ligi Kuu dhidi ya JKT Ruvu.
Mazoezi ya leo jioni ambayo yatakuwa ya mwisho kabla ya mechi ya kesho, yanatarajiwa kuwa matamu zaidi kwa wachezaji kuonyesha uwezo wao kumshawishi kocha awape nafasi- kumbuka kuna ushindani zaidi kwenye nafasi ya kiungo.
Jana Milo, alikaririwa na BIN ZUBEIRY akisema kwamba anamuhitaji Sunzu, ambaye ni mchezaji ghali katika timu yake, lakini anaweza kucheza bila yeye.
Milo alisema kwamba Sunzu hakumtumia kwenye mechi ya kwanza ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya African Lyon kwa sababu alichelewa kurudi Dar es Salaam kutoka kwao Zambia. “Ilikuwa kila siku anasema atakuja kesho, kesho, haji,”alisema.
Sunzu aliyetua Dar es Salaam siku moja kabla ya mechi na Lyon, katika kipindi cha takriban wiki tatu hakuwa na timu, kwanza akienda kwenye msiba wa dada yake Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na aliporejea akaomba ruhusu ya kwenda kwao Zambia.
Alipoulizwa kama mchezaji huyo anayelipwa mshahara mkubwa zaidi kuliko wachezaji wote wa klabu hiyo, dola 3,500 kwa mwezi, zaidi ya Sh. Milioni 5 za Tanzania, ni muhimu kwa sasa kwenye kikosi chake, Mserbia huyo alisema; “Ndiyo, ni muhimu, namuhitaji, lakini naweza kucheza bila yeye,”alisema.
Inaonekana sasa Milo anatiwa jeuri na washambuliaji wake wapya, Mghana Daniel Akuffo, Abdallah Juma, Salim Kinje, Mrisho Ngassa na wengine ambao yupo nao tangu msimu uliopita akina Emmanuel Okwi, pamoja na viungo wenye uwezo wa kufunga kama Mwinyi Kazimoto, Haruna Moshi na wengineo.
Awali ya hapo, Milo kwa sasa hawatumii mabeki wake wapya, Komabil Keita kutoka Mali na Paschal Ochieng kutoka Kenya, kwa sababu anataka kwanza waone timu hiyo inavyocheza wakiwa nje, ili wajifunze.
Profesa huyo wa Kiserbia alisema kwamba mabeki hao wawili wa kati wanahitaji muda kabla ya kuanza kucheza kwa mfumo wa Simba, ingawa amewasifia wote ni wazuri.
Alisema wakati wowote wanaweza kurudi uwanjani, iwe kwa pamoja au kupangwa na wachezaji wengine na inawezekana hata kwenye mechi ijayo, Jumatano dhidi ya JKT Ruvu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Aidha, Milovan aliwapongeza wachezaji wake kwa ushindi huo wa juzi na kusema kwamba hiyo ni zawadi kwa mashabiki wa klabu hiyo. Milo aliwapongeza Lyon pia kwa kucheza vizuri kwenye safu ya ulinzi na kiungo kidogo na kusema sasa anajipanga kwa ajili ya mechi ijayo ya ligi hiyo.
Lakini Mserbia huyo hakusita kuelezea namna alivyokunwa na beki wa kati wa Lyon, Benedictor Mwamlangala, kwa kucheza kwake vizuri kwenye mechi hiyo.
Simba SC Jumamosi ilianza vema kampeni za kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya kuichapa mabao 3-0 African Lyon katika mchezo wa ufunguzi wa ligi hiyo, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Milovan akiwatumia Juma Nyosso na Shomary kapombe katika beki ya kati.
Hadi mapumziko, tayari Simba SC walikuwa mbele kwa mabao 2-0 yaliyotiwa kimiani na Emanuel Okwi dakika ya 33 baada ya kuwatoka mabeki wa Lyon na Nassor Masoud ‘Chollo’ dakika ya 36 akiunganisha krosi ya Mrisho Ngassa.
Lyon walikosa penalti dakika ya 35, baada ya mkwaju wa Sunday Bakari kupanguliwa na Juma Kaseja, kufuatia Mwinyi Kazimoto kuunawa mpira kwenye eneo la hatari.
Kipindi cha pili, Lyon kidogo walirekebisha makosa yao, lakini bado Simba iliendelea kutawala mchezo na dakika ya 56, Danniel Akuffo aliifungia timu yake bao la kuhitimisha ushindi kwa mkwaju wa penalti, baada ya Emmanuel Okwi kuangushwa kwenye eneo la hatari.
0 comments:
Post a Comment