Na Ally Mohamed, Zanzibar
LIGI Kuu ya
Zanzibar, maarufu Zanzibar Grand Malt Premier League, leo imeingia katika
mzunguko wa pili kwa kushuhudia michezo miwili katika viwanja viwili tofauti, kwenye
Uwanja wa Amaan, Mabaharia wa KMKM wakiibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya
Malindi.
Malindi,
ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao sekunde ya 57 lililofungwa na mshambuliaji,
Issa Hamad ambaye ameandika histotia kwa kufunga bao la mapema zaidi tangu ligi
hiyo kuanza wiki iliyopita. Bao hilo lilidumu hadi mapumziko na kipindi cha
pili KMKM iliwachukua dakika mbili tu tangu KMKM kusawazisha kupitia kwa Mudrik
Muhib.
KMKM
wakiendelea kulisakama lango la Malindi hatimaye juhudi zao zikazaa matunda
katika dakika ya 90 kufuatia bao la pili na la ushindi lililofungwa na Maulid
Kapenta.
Katika mchezo
mwingine uliopigwa kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba Super Falcon ambao ni
wawakilishi wa Zanzibar katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika walikubali
kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Duma, mabao yote mawili ya Duma yakifungwa na
Vuai Abdallah katika dakika ya 55 na 66, huku bao pekee la Super Falcon
likifungwa na Mohammed Salum.
Ligi hiyo
itaendelea tena kesho kwa michezo miwili, ambapo katika uwanja wa Amaan kisiwani
Unguja, Mafunzo wataikaribisha timu ya Bandari iliyopanda daraja msimu huu, na
huko kisiwani Pemba, Chipukizi watacheza na washindi wa pili wa ligi iliyopita
klabu ya Jamhuri ambao wana tiketi ya kushiriki katik kombe la Shirikisho hapo
mwakani mechi itakayochezwa katika uwanja wa Gombani.
Wakati huo
huo: Wadau wa soka visiwani Zanzibar wamepata mashaka juu ya ushiriki wa klabu
ya Super Falcon ambayo itaiwakilisha Zanzibar katika Ligi ya Mabingwa mwakani
kutokana na kiwango kibovu kinachooneshwa na timu hiyo katika mechi zake za
hivi karibuni.
Itakumbukwa
kuwa mpaka sasa klabu ya Super Falcon, ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu
ya Zanzibar, wameshacheza mechi saba
bila kupata pointi hata moja, wakipoteza mechi zote tatu za hatua ya makundi ya
michuano ya BancABC Super8, kabla ya kufungwa 3-1 na Jamhuri katika mechi ya
kuwania Ngao ya Jamii, kabla ya kufungwa mabao 2-0 na Coastal Union katika
mechi ya kirafiki kujiandaa na ligi kuu ya Zanzibar, wakifungwa mabao 2-0
katika mechi yao ya kwanza ya Ligi Kuu ya Zanzibar na leo wakilala mabao 2-1
kutoka kwa Duma.



.png)
0 comments:
Post a Comment