BINAFSI
nawaheshimu sana kampuni ya Vodacom Tanzania kwa mchango wao mkubwa katika
maendeleo ya soka ya nchi hii, kwani sijui bila ya wao kujitokeza kuichukua
Ligi Kuu mwaka 2002, hali ingekuwaje.
![]() |
| Na Mahmoud Zubeiry |
Tulipotoka,
soka ilikuwa haina thamani kabisa mbele ya makampuni nchini- ulichukuliwa kama
mchezo wa vurugu, migogoro ambao ungeharibu hadi sifa ya kampuni, ambayo
ingejitokeza kuudhamini.
Makampuni
hayakujali ni mamilioni ya watu wangapi wanavutiwa na soka ya Tanzania,
hawakujali ni mamilioni ya watu wangapi wanapenda Simba na Yanga. Hawakujali
kama wapo watu hufikia hadi kujiua kwa ajili ya Simba na Yanga, ambazo ndizo
zinabeba msisimko wa soka ya nchi hii, waliogopa tu ni mchezo wa vurugu na
migogoro, basi- na hawakuutaka.
Waliona
bora kuwekeza kwenye michezo mingine, ambayo hata kama haina wapenzi wengi,
lakini tu haina vurugu wala migogoro.
Ilichukua
muda sana, tangu mwaka 1965 ilipoanzishwa Ligi Tanzania hadi mwaka 1996
alipopatikana mdhamini wa kwanza wa ligi hiyo, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL),
kupitia bia ya Safari Lager.
Lakini
udhamini huo ulidumu kwa takriban miaka minne tu na hali ilikuwa tete mwaka
2001, baada ya TBL kujitoa kudhamini Ligi Kuu ya Tanzania Bara ghafla. Bingwa
wa mwaka 2001, Simba SC alitoka mikono mitupu, baada ya TBL waliokuwa
wakiidhamini ligi hiyo kupitia bia ya Safari
Lager ‘kuimwaga’.
Kisa
nini? Kapuya huyo! Aliyekuwa Waziri wa iliyokuwa Wizara ya Kazi, Maendeleo ya
Vijana na Michezo, Profesa Juma Athumani Kapuya, ‘aliwaboa’ wadhamini hao kwa
kujiamulia tu kuongeza timu katika Ligi Kuu, kinyume na makubaliano yao na
Chama cha Soka Tanzania (FAT), sasa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
TBL
wakaona ligi haina kanuni, utaratibu wala kuheshimu vipengele vya mikataba ya
udhamini, ndiyo yale yale, mchezo wa kihuni, mchezo wa vurugu na usiofaa, wakaitema.
Wengi miongoni mwa wapenzi wa soka Tanzania waliingiwa hofu juu ya mustakabali
wa ligi hiyo, kwani walijua itarudi kwenye enzi zile za kucheza kwa ajili ya
mapato ya milangoni tu.
Udhamini
unaongeza ladha ya ligi kwa sababu timu zinawania zawadi, mbali na kombe,
zinapata vifaa vya michezo kutoka wadhamini sambamba na kiasi cha fedha za
gharama kama za usafiri na kadhalika, hivyo kujitoa kwa wadhamini- maana yake
ligi ingekuwa chungu kwa klabu.
Akaibuka
mkombozi, kampuni iliyokuwa mpya kabisa ya huduma za simu za mikononi Tanzania,
Vodacom Tanzania na kuingia mkataba wa udhamini wa ligi hiyo na FAT, kuanzia
msimu wa 2002.
Taratibu
hali imekwenda ikibadilika na sasa makampuni yanajitokeza kuwekeza kwenye soka,
baada ya kuuelewa vema mchezo huo, kwamba unafaa na zaidi hicho wanachoogopa
wao, vurugu na migogoro ni msisimko wa kishabiki na demokrasia, mambo ambayo ni
ya kawaida katika vitu vinavyogusa hisia za watu wengi. Hiyo ndiyo soka.
Kujitokeza
kwa wawekezaji kwenye soka, kumesababisha hadi vyama na klabu zianze kuondokana
na woga na sasa haki zaidi inatafutwa.
Tazama,
timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ambayo haikuwahi kuwa na mdhamini tangu
soka ianze kuchezwa nchi hii, kabla ya Uhuru hadi mwaka 2006, lakini mwaka huu
imegombewa na kampuni mbili katika kutaka kuidhamini na mwishowe TBL waliizidi
kete Kampuni ya Bia ya Serengti (SBL) iliyokuwa ikiidhamini timu hiyo. Tumetoka
mbali.
Lakini
pamoja na yote, soka sasa ni mchezo ambao umewekewa misingi mizuri ya sheria na
kanuni chini ya Shirikisho la Kimataifa la mchezo huo (FIFA) na ina mfumo bora
wa utawala wenye mamlaka yenye kujitosheleza.
Masuala
ya soka sasa hayafiki Mahakamani, kutokana na huo mfumo bora wa kiutawala,
sheria na kanuni na hilo limepitishwa na wanachama wake dunia nzima na yeyote
atakayethubutu kupeleka suala la soka kwenye dola, kwanza atakuwa amejiengua
kwenye familia ya kandanda, mengine yatafuata, ikiwa ni pamoja na FIFA
kupambana naye kizimbani.
Lakini
pamoja na ukweli huo, kwa Tanzania bado usimamizi wa sheria na kanuni ni tatizo
jambo ambalo limesababisha sasa hakuna nidhamu kabisa katika mfumo wa utawala
na uendeshwaji wa soka katika nchi hii kwa ujumla.
Ushabiki
wetu wa Simba na Yanga umepita kiwango na hatujali unaathiri vipi maendeleo ya
soka ya nchi hii, ambayo mara ya kwanza na ya mwisho ilicheza Fainali za Kombe
la Mataifa ya Afrika mwaka 1980.
Wizi,
rushwa na kwa ujumla kuweka mbele maslahi binafsi kwa pamoja na upeo wetu mdogo
na ujuaji, hawa ni maadui wakubwa wa soka yetu. Siku zote nasema, tuna safari
ndefu sana kufikia matamanio, maana hatuna malengo, zaidi ya kuwamezea mate
wenzetu na kutamani siku moja tuwe kama wao.
Jana
kimetokea kituko Uwanja wa Taifa, ambacho ni mwendelezo wa hayo mapungufu
niliyoyaelezea hapo juu.
Klabu
ya African Lyon ilizuiwa kuweka mabango yake kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam wala kuvaa jezi zenye nembo ya mdhamini wao, kampuni ya simu ya Zantel
katika mchezo wa leo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Simba SC.
Mapema
jana mchana, Lyon ilitangaza kuingia mkataba wa udhamini na Zantel wa miaka
mitatu na ilitarajiwa kuanza kuutumikia katika mchezo wa jana wa ufunguzi wa
Ligi Kuu dhidi ya Simba.
Meneja
Mkuu wa Lyon, Rahim ‘Zamunda’ Kangezi, alisema msimamo huo wa kuzuiwa kuvaa
jezi za mdhamini wao na kuweka mabango kama ungeendelea, basi wao wasingecheza
mechi hiyo. Nilijuwa hawawezi kuacha kucheza na walicheza wakafungwa mabao 3-0.
“Katika
maboresho ya mkataba wa udhaimini wa Ligi Kuu wa Vodacom, hili
limekwishazungumzwa na limerekebishwa kwamba klabu zitaruhusiwa kuingia mkataba
na kampuni nyingine za simu.
Pia,
leo (jana) katika kikao cha kabla ya mechi tulipeleka jezi hizi na
zikapitishwa, sasa iweje tunaambiwa hatuwezi kuvaa, sisi hatukubali, kama
hatuvai na hatuchezi,”alisema Zamunda.
Mapema
jana mchana, Ofisa Mkuu wa Biashara wa Zantel, Sajid Khan alitangaza kampuni
yake kuingia mkataba wa miaka mitatu kuidhamini Lyon, mbele ya Mkurugenzi wa
Michezo, Leonard Thadeo katika hoteli ya Hyatt Regency (zamani Kilimanjaro),
Dar es Salaam.
Hadi
sasa haieleweki kama mkataba mpya wa udhamini wa Ligi Kuu umesainiwa au la,
maana yake pamoja na TFF kusema umesainiwa, lakini hakuna picha inayoonyesha
utiwaji saini wa mkataba mpya, baada ya ule wa awali kumalizika msimu uliopita.
Na
kumekuwa na mgogoro kabla ya utiwaji saini wa mkataba huo, kubwa klabu zikitaka
sasa kama ilivyo kwa nchi nyingine nyingi wanachama wa FIFA, ziendeshe zenyewe
ligi na hilo lilipitishwa katika mkutano Mkuu uliopita wa shirikisho hilo,
ingawa utekelezwaji wake rasmi bado.
Klabu
zinadai, wakati wa matayarisho ya mkataba mpya, waliomba baadhi ya vipengele
vya mkataba huo, viboreshwe, ikiwemo kuziruhusu kampuni za simu kudhamini klabu
na inaelezwa hilo lilikubaliwa na TFF.
“Klabu
zilikubaliana kwa pamoja kuwa kipengele cha exclusivity kiondolewe kweye
mkataba na kiliondolewa... nakumbuka nilimuuliza swali Mjumbe wa Kamati ya Ligi,
Yahya kuwa, je endapo JKT Ruvu itampata Tigo kama mdhamini, je itaruhusiwa
kucheza ligi na jezi zenye nembo ya Tigo? jawabu lilikuwa ni YES... sasa
kilichotokea uwanja wa Taifa leo (jana) ni kichefuchefu,”alisema Meneja wa Azam
FC, Patrick Kahemele akilizungumzia sakata hilo.
Ukichukua
maelezo ya Kahemele na Zamunda, unaweza kugundua tatizo katika hili, lipo TFF.
Inakuwaje makubaliano yafikiwe halafu yasitekelezwe? Hizi ni vurugu zisizo za
lazima.
Nilisema,
tulipotoka mbali na tulipofikia klabu zimeanza kujiamini na zinataka haki
zaidi, ndio kama hivyo wanaomba kampuni nyingine za simu ziruhusisiwe kudhamini
klabu.
Mwaka
2002, wakati Vodacom wanaingia mkataba wa kudhamini ligi hiyo kwa mara ya
kwanza, Yanga ilikuwa inadhaminiwa na Mobitel (sasa Tigo) na kwa sababu hiyo,
Vodacom wakaiondoa Yanga kwa Mobitel na kuipa udhamini wa kampuni ya Shivacom,
waliokuwa mawakala wao.
Hata
hivyo, inaonekana ule ulikuwa mkataba wa ujanja ujanja tu wa kuifanya Yanga
iachane na Mobitel na ndiyo maana haukudumu, lakini hali imebadilika sasa na watu
wanahoji, kama Ligi Kuu ya England mdhamini wake ni Barclays na bado Liverpool
inadhaminiwa na Standard Charter, zote benki, iweje hapa Tanzania isiwe hivyo?
![]() |
| African Lyon katika mechi ya jana bila ya jezi za wadhamini wao |
Inaweza
kuwa hivyo, lakini pia si lazima iwe hivyo- ni suala la makubaliano tu na
maamuzi yake yazingatie maslahi ya pande zote.
Hatuhitaji
kupiga kura tu katika kuamua Kevin Yondan acheze timu gani, bali hata katika
suala la udhamini, klabu zingepiga kura kuamua Vodacom iendelee kudhamini Ligi
Kuu kwa kuruhusu kampuni nyingine za simu zidhamini klabu, au ijitoe.
Sasa
klabu ambazo hazina ndoto za kuwa na wadhamini na zinauhitaji udhamini wa
Vodacom zingeamua sakata hilo- lakini kitendo cha klabu kukubaliwa ziingie
mikataba ya udhamini na kampuni nyingine za simu, halafu zinazuiwa kuutumikia
ni vurugu ambazo zinaepukika. Lakini kwa nini madudu haya katika soka yetu?
Inakera!





.png)
0 comments:
Post a Comment